Kuanzishwa kwa TANU katika Majimbo

Wasomi wa Makerere, ambao Mwangosi aliwaamini sana katika kuunda TANU, walipopata habari kuhusu mkasa wa Taratibu na DC, Bwana Smith, waliogopa. Waliamua kujiweka mbali kabisa na mambo ya siasa na kuendelea na kazi yao ya kufundisha. Haruna Taratibu na Omari Suleiman sasa waliamua kugeuza mbinu, waliitisha mkutano wa siri usiku nyumbani kwa Swedi bin Athumani.

Mkutano huu uliamua kuwa Taratibu lazima aende makao makuu ya TANU Dar es Salaam akazungumze na Nyerere ana kwa ana kuhusu matatizo yaliyokuwa yakiikabili TANU Dodoma. Mahdi Mwinchumu aliyekuwa mwanachama wa TANU Dar es Salaam alijitolea kufuatana na Taratibu hadi makao makuu ya chama Dar es Salaam kwa kuwa alikuwa akijuana na viongozi wa TANU. Said Mussa mjumbe mwingine wa ile kamati ya siri alijitolea vilevile kufuatana na Taratibu na Mwinchumu hadi Dar es Salaam.

Siku ya kuondoka Job Lusinde alikwenda stesheni ya gari moshi kuagana na ule ujumbe uliokuwa ukielekea Dar es Salaam, makao makuu ya TANU. Lusinde aliuambia ule ujumbe kuwa jamaa wa Makerere wanaunga mkono maamuzi yote yatakayoamuliwa na ile kamati ya siri.

Kwa bahati nzuri katika gari moshi lile lile ambamo Taratibu na wenzake walikuwa wakisafiri kulikuwa na wajumbe wa TANU kutoka Kigoma, Bukoba na Mwanza wakisafiri kwenda Dar es Salaam kuhudhuria mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka wa TANU.

Wahudumu ndani ya gari moshi walipofahamu kuwa walikuwa na wajumbe wa TANU kwenye gari moshi lile, waliwafanyia heshima kubwa. Mmoja wa wahudumu wale alijitolea kumpa malazi Salum Mussa nyumbani kwake Dar es Salaam. Mahdi Mwinchumu aliwapeleka Haruna Taratibu na Said Mussa makao makuu ya TANU New Street ambako walifanya mazungumzo na Nyerere pamoja na Rupia. Uongozi wa makao makuu ulielezwa kwa ufupi matatizo yaliyokuwa yakikabili Dodoma katika kufungua tawi la TANU. Papo hapo Nyerere alimwalika Taratibu kuhudhuria mkutano mkuu Hindu Mandal Hall kama mjumbe wa Jimbo la Kati. Mkutano ule ulimchagua Taratibu kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU. Taratibu na ujumbe wake walirudi Dodoma washindi, walikwenda Dar es Salaam watu wasiojulikana na walirudi nyumbani wakifuatana na mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa wa TANU, chombo cha juu kabisa katika chama. Nyerere alimpa Taratibu dafari ya tasjili ya wanachama, kadi mia moja hamsini za uanachama wa TANU na nakala hamsini za Bill of Rights.

Kazi ya kuwahamasisha na kuwaingiza watu TANU alipewa Omari Suleiman, na fundi cherahani mwingine aliyejulikana kwa jina la Abdu Mohamed Mkamba. Mara tu baba mwenye nyumba wake alipopata habari za kuwa mpangaji wake, Haruna Taratibu alikuwa mwanachama wa TANU, alimfukuza kutoka kwenye nyumba yake.

Baada ya kupata kikundi kidogo cha wanachama, Taratibu alipiga simu makao makuu ya TANU na kuzungumza na kaimu katibu, Elias Kissenge akaomba ruhusa ya kufanya uchaguzi. Kissenge hakuweza kutoa uamuzi wowote wa maana kuhusu tatizo la uongozi wa TANU Dodoma.

Taratibu alifanikiwa kumpata Kambona ambae aliidhinisha uchaguzi ufanyike kwa shuruti moja la kuwa Hassan Suleiman na Ali Ponda waruhusiwe kushiriki na kugombea uongozi wa chama. Kusisitiza kwa Kambona juu ya uongozi wa zamani wa TAA kuongoza chama kipya huenda kulishawishiwa na mafanikio ya zamani ya uongozi wa Hassan Suleiman mbae alimfahamu huko Dodoma wakati Kambona alipokuwa mwalimu akifundisha Kikuyu Secondary School.

Kwa bahati mbaya, wanachama wa TANU waliokuwa wanainukia na chama pale mjini Dodoma waliwaona Hassan Suleiman na Ali Ponda kama wasaliti kutokana na kutokushirikiana na wenzao katika kuanzisha TANU.

Wakati ametatizwa na tatizo la uchaguzi wa TANU, Taratibu alijulishwa na makao makuu kuwa makamo wa rais, John Rupia, atapita Dodoma kwa gari moshi akiwa njiani kwenda Tabora kushughulikia mambo ya chama. Gari moshi liliposimama Dodoma Rupia alishangazwa kuona kundi la wananchama wa TANU wakimsubiri katika kituo cha gari moshi wakimtaka avunje safari waende mjini kujadili na kutatua tatizo la uchaguzi. Rupia aliwaeleza wanachama wa TANU wa Dodoma kuwa yeye hakuwa na idhini kutoka makao makuu kufanya shughuli yoyote ya chama mjini Dodoma. Wanachama wa TANU hawakutaka kusikia lolote na walimwambia Rupia kuwa wamechoshwa na makao makuu kwa kushindwa kwake kutoa uamuzi wa tatizo la uchaguzi. Mizigo ya Rupia ilishushwa chini kutoka kwenye gari moshi na Rupia akawa hana khiyari isipokuwa kuwafuata wale wanachama wa TANU hadi mjini.

Ghafla mji mzima ukavuma tetesi kuwa makamu wa rais wa TANU, John Rupia, yupo mjini kufungua tawi la TANU. Rupia alimwita Hassan Suleimna na akamtaka alete hati ya tasjili ya TANU Hindu Mandal siku inayofuata, mahali ambako mkutano utafanyika. Hassan Suleiman hakutokea mkutanoni lakini alimtuma mtu apeleke ile hati. Ali Ponda alihudhuria mkutano ule. Rupia alikuwa mwenyekiti wa mkutano na TANU ikafanya uchaguzi wake wa kwanza. Alexander Kanyamara alichaguliwa Rais; Haruna Taratibu Makamu wa Rais, Abdu Mohamed Mwamba, Katibu na Omari Suleiman Mweka Hazina.

Miongoni mwa wanachama waasisi alikuwa mwanamke mmoja wa Kimanyema, Binti Maftah Karenga; wengine walikuwa Bakari Yenga, Maalim Khalfan, mwanachuoni wa Kiislamu aliyekuwa akiheshimawa sana, Idd Waziri na Said Suleiman. Wale wasomi wa Makerere hata mmoja hakujitokeza kwenye mkutano huu wa kuasisi TANU. Ali Ponda, mwanasiasa mkongwe alipuuzwa na hakuchaguliwa kushika wadhifa wowote. Walipoona hawakupewa wadhifa wowote katika TANU, Ali Ponda na Hassan Suleiman walijiunga na UTP kuipinga TANU.

Baada ya uchaguzi huo, wale mafundi cherahani wawili, Abdu Mohamed Mkamba na Omari Suleiman, walianza kuhamasisha wananchi wazi wazi kujiunga na TANU ili wapiganie uhuru wa Tanganyika.

Tawi la TANU la Dodoma baada ya kujizatiti pale mjini, lilituma wanaharakati kuwahamasisha watu wa Kondoa ili wafungue tawi la TANU katika wilaya hiyo. Abdallah Jumbe alizipenyeza kadi za TANU na kuzipeleka kwenye wilaya hiyo kwa siri akaanza kuandikisha watu.

D.C. wa Singida alikuwa jeuri sana kiasi kwamba ni baada ya Mkutano Mkuu wa Tabora wa mwaka 1958 ndipo Abdallah Jumbe aliweza kufanikiwa kufungua tawi mjini Singida. Wakati huo TANU ilikuwa na nguvu sana ikiwa na wajumbe wake katka Baraza la Kutunga Sheria. Kwa ajili hii hakuna Mzungu aliyethubutu kuwa fedhuli kwa TANU na kuwabughudhi wanachama wake.

Jimbo la Kusini, 1955

TAA mjini Lindi ilikuwa chini ya uongozi wa Suleiman Masudi Mnonji aliyekuwa Rais na Katibu wake alikuwa Mohamed Waziri. Mnonji alikuwa fundi cherahani na Waziri alikuwa mchoraji wa ramani za nyumba. TAA ilichelewa kuanza mjini Lindi. TAA ilianzishwa Lindi mwaka 1953 wakati uongozi wa TAA mjini Dar es Salaam si tu ulikuwa unaigeuza TAA kuwa chama cha siasa bali ulikuwa ukifanya mipango kumpeleka mjumbe wake Umoja wa Mataifa kudai uhuru. Masudi Mnonji alikuwa na uzoefu wa kutosha katika siasa.

Baada ya Vita Kuu ya Pili alikuwa amejaribu kuanzisha vyama vya wafanyakazi katika mashamba mbalimbali ya mkonge kusini mwa Tanganyika. Vilevile aliwakusanya wapishi na madobi mjini Lindi waanzishe umoja wao. Ilikuwa kupitia juhudi zake binafsi TAA ijapokuwa ilichelewa, ilikuja kuanzishwa mjini Lindi na Mnonji alijitolea nyumba yake katika mtaa wa Makonde kama ofisi ya chama. Mnonji kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uongozi ulioelimika vizuri, alimleta Nangwanda Sijaona kutoka Nachingwea aje aishauri TAA jinsi ya kufanya mambo kwa utaalamu.

Wakati huo mjini Lindi kulikuwa na chama cha wafanyakazi bandarini Dockworkers' Union chini ya uongozi wa Mussa Athumani Lukundu, chama ambacho kwa kiasi chake kilianzisha vuguvugu la siasa za vyama vya wafanyakazi.

Ingawa vyama hivi viwili, yaani TAA na Dockworkers' Union vilikuwepo katika mji mmoja, siasa za hiki chama cha pili cha wafanyakazi bandarini hazikupitia TAA kama ilivyokuwa mjini Dar es Salaam. Hii kidogo ilidhoofisha mwamamko wa siasa kwa wananchi. Jimbo la Kusini lilikuwa katika usingizi mzito wakati sehemu nyingine Tanganyika zilikuwa zikipiga hatua kwenda mbele zikiandaa vita dhidi ya utawala wa kikoloni. Chanzo cha usingizi huu mzito huko kusini ulikuwa na asili yake katika historia ya Tanganyika.

Vita vya Maji Maji vilipoanza kusini ya Tanganyika mwaka 1905 kwa nia ya kuwafukuza Wajerumani kutoka Tanganyika, zile sehemu zenye Wakristo wengi zilikataa kujiunga na vita na badala yake wakajiunga na majeshi ya Wajerumani na kupigana bega kwa bega na dhidi ya wazalendo. Hii ilitokana na sababu ya kuwa uasi dhidi ya dhulma wa Wajerumani ulianza katika maeneo yenye Waislamu wengi na vita vikachukua sura ya vita vya Kiislamu dhidi ya Wazungu ambao dini yao ni Ukristo. Kwa kuwa wamishonari walikuwa washirika wa wakoloni, walichukuliwa kama maadui na hivyo ikawa vituo vyao vinashambuliwa na wapiganaji wa Maji Maji. Kutokana mashambulizi haya, Wakristo walivichukua Vita Vya Maji Maji kama vita dhidi ya Ukristo.

Harakati za Maji Maji zilishindwa na Wajerumani walifanya fisadi kubwa dhidi ya wananchi na viongozi wao. Jambo hili liliacha kovu kubwa katika fikra za wananchi na kwa upande wa Wakristo ambao walinusurika na ghadhabu ya Wajerumani, wengi wao wakajiweka mbali na aina yoyote ya kupinga ukoloni.

Kufuatia historia hii Waafrika waliokuwa kusini ya Tanganyika sasa wakiwa chini ya utawala wa Waingereza na kuwa chini ya himaya ya wamishonari walipupazwa kiasi kiasi kwamba waliogopa siasa.

Baada ya Waafrika kushindwa vita kwa silaha kali za Wazungu sasa Kanisa likaona ndani ya fadhaa ile fursa yao kutawala sehemu hiyo kwa kutoa vishawishi kama vile shule na hospitali. Kwa hiyo Wamishionari na Waingereza walionekana kama mabwana wema wenye kuwajali raia zao kinyume na serikali katili na ya kidhalimu ya Wajerumani.

Vuguvugu la siasa kama ilivyokuwa Vita vya Maji Maji, lilianza katika maeneo ya Waislam kufuatia mfumo ule ule kama ilivyokuwa katika upinzani wa ukoloni wa Wajerumani. Wakristo katika Jimbo la Kusini waliiona TANU kama walivyoviona Vita Vya Maji Maji, kama harakati nyingine za Waislam zilizokuwa zikija tena kwa mara ya pili kuvuruga amani na utulivu. TANU ilipoanza ikawa inavuma kuwa safari hii Waislam walikuwa wamemua kuanzisha vita dhidi ya Waingereza kama walivyoanzisha vita na Wajerumani.

TANU ilipoanzishwa mjini Dar es Salaam na hisia za utaifa zilipokuwa zikipanda pole pole katika fikra za wananchi katika sehemu nyingi za Tanganyika, Jimbo la Kusini lilikuwa bado usingizini likiishi katika zama za kale. Mnonji na Waziri, kwa sababu ya utu uzima wao, daraja yao katika jamii na hasa kutokana na kuhusika kwao katika siasa za pale mjini, walikuwa na nguvu kubwa katika TAA. Wakati TANU imeshachukua nafasi ya TAA, uongozi wa TAA Lindi haukutaka kufungua tawi la TANU.

Mtu wa kwanza kuutanabaisha uongozi wa TAA mjini Lindi juu ya mageuzi yaliyokuwa yakitokea Tanganyika na kuanzishwa kwa chama kipya cha siasa mjini Dar es Salaam alikuwa Abdallah Juma Makopa, kijana kutoka Tanga akifanya kazi ya ukarani Posta ya Lindi. Makopa aliwaendea Mnonji na Waziri na kuwajulisha kuhusu kuanzishwa kwa TANUmjini Dar es Salaam na aliwashauri waanzishe TANU pale Lindi. Jambo hilo lilipingwa moja kwa moja na Mnonji, Waziri, Said Nassoro, Abdallah Mhuji na wanachama wengine wa TAA.

Chama cha Waafrika ambacho kilianzishwa siku nyingi mjini Lindi na kwa hakika ndicho kilikuwa chama cha pekee kushughulikia maslahi ya Waafrika sehemu za kusini kilikuwa African Welfrare Association ambacho mlezi wake alikuwa John Nevi, Mjaluo kutoka Kenya na katibu wake alikuwa Casian Njunde, Mngoni wa Songea. Makopa aliposhindwa kukishawishi kile kikundi cha wazee wa TAA aliwaendea Yusufu Chembera na Rashid Salum Mpunga. Chembera alikuwa na umri wa miaka thelathini na nne na Mpunga alikuwa kijana wa miaka ishirini na saba. Chambera alikuwa amesoma hadi shule ya msingi na Mpunga alikuwa amemaliza madras. Chembera alikuwa akifanya kazi katika kantini ya Lindi Welfare Centre, wakati Mpunga alikuwa dereva wa lori aliyeajiriwa na mfanyabishara wa Kihindi. Makopa aliwashauri Chembera na Mpunga juu ya uwezekano wa kuwahamasisha wananchi wawaunge mkono ili tawi la TANU lifunguliwe pale mjini. Aliwaambia alitaka sana kufanya hivyo yeye mwenyewe lakini asingeweza kwa sababu yeye alikuwa mtumishi wa serikali na hakuwa akifahamika sana mjini. Uongozi kama wao ndiyo ungeweza kuaminiwa na wananchi na usingetiliwa mashaka. Makopa, Chembera na Mpunga walikubaliana kuwa kabla ya kuanza kufanya kampeni waziwazi kwa ajili ya TANU, lazima wawaandikishe wanachama wachache kama waasisi wa chama. Mpunga na Chembera walimwandikisha kijana mmoja akiitwa Abdallah Faraj na katika muda mfupi waliweza kuwapata takriban
 
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook