BARUA
 
Kura ni silaha, usipumbazwe

Ndugu Mhariri

SOTE Watanzania tuko hadhiri na hali inayoendelea hivi sasa hapa nchini kwetu. Na kila mmoja wetu anatambua ni nini tunachotakiwa kukifanya mwaka huu mnamo Oktoba 29.

Nafikiri wote mtakubaliana na mimi kuwa hii ni fursa muhimu mno kwetu kwa mustakabali wa maisha yetu kama Watanzania.Ni fursa ya kuchagua viongozi. Viongozi hao watatufanya tuendelee kuishi maisha duni au tuondokane na uduni tulio nao na udhalili mkubwa unaotukabili kama Watanzania.

Ikumbukwe kuwa babu zetu walipofanya jitihada na kujitoa muhanga wa mali na nafsi hawakufanya hayo hivi hivi bali walikuwa wanajivua katika makucha ya mkoloni na walitarajia kuwa pindi wapatapo uhuru wataondokana na unyonge uliokuwa unawakabili.

Kinyume na matarajio yao mara baada ya kupata uhuru hali ilizidi kuwa duni kwa Watanzania pengine tunaweza kudiriki kusema kuliko ile ya wakati wa mkoloni.

Ukitembelea mikoa ya kusini mwa Tanzania, hali inatisha. Maji hakuna na ili mwanamke wa Kitanzania aweze kupata maji inabidi aamke saa 10 alfajiri kwenda kutafuta maji na kupata ndoo moja itamgharimu kuanzia masaa mawili hadi manane. Barabara ni mbovu na zinapitika kwa msimu. Ikinyesha mvua tu imeshakuwa tabu watu wa kusini wanakuwa tayari washawekwa kisiwani.

Yote haya hayatokei kwa sababu nyingine bali kwa namna moja au nyingine yanayosababishwa na sera mbovu zilizowekwa na viongozi walioko madakarani. Sera ambazo hazijalenga kumnufaisha Mtanzania bali zimelenga kuwanufaisha watu fulani fulani binafsi. Haziangalii maslahi ya taifa bali zinaangalia maslahi ya matumbo ya watu.

Katika hali kama hii, Watanzania hatuna budi kuitumia fursa hii tuliyonayo mwaka huu kuamua watu gani watatuondolea adha na kero hizi.

Inashangaza sana kuona katika wakati kama huu wanatokea watu kuwataka waumini wao wasijiandikishe na wala wasipige kura.

Tujiulize watu kama hawa je, ni kweli wanaitakia mema nchi hii? Je wanawatakia kheri waumini wao? Au ndio wao katika wale wachache waliofaidi matunda ya uhuru na hivyo hawaoni sababu ya kurekebisha hali mbaya iliyopo nchini. Lazima tuwe macho na watu kama hawa wasiotutakia mema, wasiotujali wala kujali maslahi yetu.

Kinachofurahisha ni kuwa Watanzania wengi sasa wameelewa na hawakubali tena kudanganywa na propaganda za viongozi waharibifu.

Nawaasa vijana wenzangu wote, kutokubali kuburuzwa na viongozi wasiolitakia mema taifa letu na wajitoe muhanga katika kusimamia haki na uadilifu katika nchi yetu.

Fatma Mussa,
Dar es Salaam.


Woga ni adui wa maendeleo

Ndugu Mhariri

MWAKA huu ni mwaka wa uchaguzi nchini kwetu, uchaguzi mkuu wa pili wa vyama vingi utakaowachagua Rais, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Bara na upande wa visiwani utawachagua Rais wa Zanzibar na wa Muungano, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

Uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu sana katika maendeleo yetu Watanzania. Ni wakati ambao watu watapimwa kwa mara ya pili ni jinsi gani wamepevuka, wana upeo kiasi gani katika maisha na maendeleo ya nchi yao na utambuzi wao.

Huu ni wakati muafaka kwa wale wote wenye sifa za kupiga kura kuona hali ya nchi kimaendeleo ikoje, hali yake na familia yake na ndugu zake iko vipi, ni wakati wa kufanya tathmini ya maisha yetu na ufumbuzi wake, kwa wale wasiokuwa na sifa za kupiga kura ujue kuwa wanakutegemea wewe uwape zawadi iliyobora katika maisha yao ya baadaye ambayo msingi wake ni kura yako.

Ni wazi kuwa wapo baadhi yetu wanapewa visenti ili wamchague fulani ni sawa lakini angalia shilingi 2000 itaweza kutuletea maendeleo ya miaka mitano, au kiroba cha unga ulichopewa kinaweza kutuondolea njaa ya miaka mitano?

Wakati tulionao si wakati wa ushabiki wa vyama, ni wakati wa kutulizana na kuamua kilicho bora, maamuzi yawe huru yatakayokunufaisha wewe na kizazi chako bila kuangalia nami alinipa kiroba cha mchele au shilingi 2000 au doti ya Khanga.

Wakati huu wa uchaguzi mengi yatasemwa na watu halikadhalika na vyombo vya habari.

Ningependa kuwatahadharisha wananchi wakati huu wa wa kampeni kuelekea uchaguzi wawe makini na vyombo vya habari vya hapa nchini. Kwani kama ilivyo kawaida yao waandishi wengi wanaonekana kukisapoti chama tawala.

Kwa shinikizo au utashi binafsi na chuki za asili miongoni mwao wanataka siku zote na janja mbalimbali wawe wanaowataka wao.

Kwa muda mrefu wapenzi wa timu Yanga walikuwa wakishangilia CCM...CCM viogozi walionekana kuuridhia ushangiliaji huo. Lakini hivi majuzi wapenzi na mashabiki hao walishangilia ngangari... ngangari..ngangari...jino kwa jino, viongozi wake walihofu na kutetemeka na haikutosha hiyo walikanusha kuwa hawana uhusiano na vyama vya kisiasa wakati hakuna aliyewauliza mambo ya siasa.

Lakini hofu hii inatoka wapi? Lazima tuelewe kwa sababu bado tunatawaliwa kifikira, hatuko huru kabisa katika maisha yetu ya kila siku.

Mawazo kama hayo ndiyo yamejaa polisi, kwenye vyombo vya habari, makazini na watu wenye vyeo vikubwa kwenye mashirika mengi hapa nchini pamoja na Masheikh wetu.

Watu wengi wanaogopa kujionyesha kuwa wana mageuzi kwa kuogopa kufukuzwa kazi, kutishwa au kutengwa au kufungiwa biashara zao.

Kuna redio moja binafsi baada ya kuogopa sana kulitumia neno Ngangari, hivi sasa inajiita Ngangari na hakuna kilichotokea. Hii yote ni hofu tuliyojengewa na utawala wa nchi hii kwa manufaa ya watu wachache, lakini historia inajirudia.

Yusuf Ng'ombo,
Dar es Salaam.
 
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook