NILIZINDUKA majira ya saa nne usiku nikiwa nimelala chali. Macho yangu yalitua juu ya dari nyeupe. Baada ya muda mfupi nikagundua kwamba juu yangu kuliuwa pangaboi na taa kali ikimulika. Nilijua kwamba hapa sio nyumbani. Nipo wapi basi? Nikajaribu kujivuta kidogo ili kutaka kujua habari zaidi. Hapo ndipo nilipohisi kwamba nilikuwa taabani maumivu makali yalinipata mwilini. Ukwenzi mkali wa kuonyesha maumivu ulinitoka.
Baada ya kushindwa kujifaragua nikaamua kuangaza pembeni yangu. Kivuli cha mtu kilikuwa kimejinamia. Alipohisi kwamba ninamtizama naye alinyanyua macho yake. Macho yetu yakakutana. Dalili ya machozi haikujificha kwenye macho yake. Nilianza kumwonea huruma. Ni kaka yangu mwenyeji wangu hapa Zanzibar.
"Hadi lini tutaepukana na dhiki hii?" alinung'unika.
Sikuwa na jibu bali niendelea kumwangalia kwa muda huku machozi yakinibubujika kama mvua. Hatimaye niligeuza uso na kuangalia juu. Sikuwa nimevutiwa na chochote darini bali mawazo yangu yalikwenda mbali, mbali sana. Sio umbali wa siku nyingi bali matokeo mengi ya huzuni na sio wingi mkubwa, bali uchungu wake unaumiza sana sana. Unakata maini, unachefua moho, kichwa kinakaribia kupasuka, ulimi unakaribia kuacha kazi. Kila kitu sasa waweza kukiona kichungu kuliko.
Mara baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza kwamba wanafunzi sasa itawabidi warudi kujiandikisha kwao walikotoka, nilisema nitakwenda. Niliwakuta watu wamo katika kujiandikisha. Malalamiko kila mahala, shutuma kushutumiana, matusi kutukanana. Nikasema ah, ndio jino kwa jino". Nikajijibu mwenyewe... "Pengine ... lakini
Sikuchelewa kujua sababu yake. Au niseme sikuchelewa na mimi kuingia ngomani. Nami sikukosa wa kumtukana bila kujijua. Labda ni kweli aliyosema mhariri wa gazeti moja litolewalo kila wiki "ni ulevi wa Kipemba".
Basi siku ya pili yake nilichukua cheti changu cha kuzaliwa. Nikajisogeza kwenye foleni mara tu baada ya kuswali swala ya asubuhi. Tukasubiri saa mbili. Tulikuwa tunaongea, tulicheka na kufyonya. Hayakuwa mazungumzo ya kufurahisha. Lakini uchungu unapozidi binadamu hana budi kucheka.
Kila mtu alikuwa akizungumzia sababu ya kuitoa CCM madarakani. Aliyenyimwa nafasi ya masomo kiroho mbaya. Aliyezuliwa kufanya biashara kubwa ya kuagiza mchele... Aliyekosa ajira kwa kufukuzwa kwa vile ni Mpemba... Anavyosota kusubiri kiinua mgongo kwa kuwa hana jamaa. Maana mambo yenyewe kama huna jamaa, ujitegemee. Ndio sera ya CCM - Ujamaa na Kujitegemea. "Rasilimali yangu ni kura tu ili nijitegemee... Hata nikishinda hapo mwezi mzima...kama si vile virungu vya usiku jana. Ningelala hapa hapa... Sote tulicheka... "Ohoo, ulevi wa Kipemba huo". Nilijisemea.
Sasa saa mbili inakaribia mtu wa mbele sasa hataki tena mazungumzo. Macho mbele tu... Ghafla akalazimika kugeuza uso kwani watu walianza kuguna mm! Mm! Bismillahir! Uso kwa uso na "Mahita" (askari polisi mmoja kule Kusini Pemba huitwa "Mahita" kwa uhodari wake wa kuwafundisha CUF ngangari). Gari la KMKM likiwa na wazamiaji kibao waliteremka. Kwanza ni bambasanchi. Utadhani watuhumiwa wa wizi, mabegani, tumboni, mifukoni mat.. ni... Baadaye amri moja.
Kaa chini! Tukakaa "Mahita" na Diwani (mgombea) wa CCM wakaanza kuopoa wakereketwa wa CCM. Baada ya hapo amri nyingine. "Rudi nyuma" Tukarudi. Wakereketwa wa wakereketwa wakawekwa mbele..!! Donge zito la mate machungu likajilazimisha kudidimia tumboni. "Kileo cha Kipemba". Na hakika na wenzangu walikunywa kileo hicho.
Yule jamaa aliyekuwa mbele aligeuka nyuma kwa uchungu mdomo wazi. Najua tuliekeana sawa sawa lakini sidhani kama alikuwa akiniona. Dakika tano zilipita (sikuwa na saa) katika hali ile. Machozi yalikuwa yakimchuruzika. Oh maskini bahati yake hakuwa amesimama.
Filimbi ikaanza, foleni ikaanza kusogea haraka haraka utadhani sio wale waandishi wa jana. Leo kama wote mabingwa wa malaria (madaktari wakikutazama wanakujua kama unaumwa malaria). "Nenda dirishani". Oh maskini. Mtanzania nchi yako ndio maskini ya kutupwa, pamoja na utajiri wa amani. Hayo namwachia Lipumba labda naye amekunywa "ulevi wa Kipemba".
Basi wasikia sana. Ilipofika saa tano. Mtu mmoja alitoka ndani pamoja na "Mahita" akatwambia "wazee itabidi tusubiri "stika" kwani zimetuishia. Lisilo budi hutendwa, tufanyeje na walipindua ili watu..." watukomboe. Hayaa.
Basi baba tukasubiri, tukasubiri, tukasubiri.... Hadi adhana ya laasiri tukaambiwa sasa "stika" tayari. Tume bwana haina mchezo kwa kazi! Haya foleni ikasogea na mimi sikuwa mbali nikapata nafasi ya kuingia ndani.
Kabla ya kukaa kitako Sheha (wakala wa Tume, nasikia) akamaka "huyo hana kura huyo". "Mimi, mimi" nikajibu kwa kigugumizi. "Mimi nimemaliza F II mwaka jana hapa". Nikajitetea. Nasema hakai hapa huyo, kashahama. Kuona hivyo wakala wa CUF akanitetea, "lakini sheria ndivyo isemavyo. Vijana wanaosoma nje ya majimbo yao wajiandikishe kwao. "Wee! Utakwenda ndani sasa hivi usifanye fujo hapa", "Mahita" alimng'akia wakala wa CUF baada ya kuona "ulevi wa Kipemba" unaanza kumpanda mwana ngangari.
Kuona vile nikaona sina budi nikimbie kulala jela. Machozi huku yakinibubujika. Ni lazima nipige kura kwa maisha yangu... CCM imetandika mfumo wa kibaguzi... Mimi Mpemba sina langu, sina haki, katika nchi hii... Loh! Aliyeninyima kupiga kura ... Siendi mazikoni kwake... simpi maji hata akiwa na kiu ya kufa... kiwanda kizima cha matusi kilikuwa kimejenga kwenye ulimi wangu. yaliyonitoka kimoyomoyo, yakinitoka njiani, yakinitoka ninapokula, yakinitoka usingizini Loh! Maskini ulevi wa Kipemba".
Baada ya kuona sina jimbo. Labda Msomalia au Mhutu au sijui... Nikaamua kupanda meli kurejea Unguja. Nikabaki kuulizia Nani kapigwa... Nani katiwa pingu... Nani yuko rumande.
Mara Radio One, mara radio Kifua alimradi nimo mashakani, roho yangu imekuwa kiwanda cha matusi. Na chuki kwa nini lakini nisichukie?
Hadi ilipokuwa siku ya mwisho ya kupiga kura. Kaka yangu alikuwa amekataliwa kupiga kura. Kwa sababu eti sio mkazi wa pale. Bwana Sheha, hamjui, hayumo ndan ya madaftari yake. Sikushangaa kuona hana raha, nafsi yake imekuwa nzito sana kwake. Hana hamu ya kufanya kazi. Amebaki kukuna kichwa. Mwaka wa kumi sasa anaishi hapa. Kazini alifukuzwa kwa vile tajiri wake anaogopa kumwajiri kwa vile yeye ni Mpemba. Angepoteza haiba mbele ya wenzake. Sasa anaishi kwa kubabaisha tu.
Usiku kuamkia siku ile tulikaa nyumbani kutafakari hali halisi. Mtu mmoja alitwambia kwamba askari kutoka bara walikuwa wakiandikishwa kupiga kura. Wengine hawajawa raia wa Zanzibar. Wengine hawajatimiza sharia za ukaazi... Katika maongezi mtu mmoja alitudokeza kwamba wengi wa askari hupewa kadi ya kumchagua Rais wa Muungano tu. Tulipofika hapo mawazo yakatujia, kama ni hivyo basi sisi tuna haki zaidi ya kupewa kumchagua Rais wa Muungano na wa Zanzibar pia. Tukaazimia kesho yake kwenda kubahatisha.
Siku ya mwisho ya uandikishaji kulikuwa na watu wengi kituoni, kama kawaida. Ni dhahiri watu wasingemalizika. Tume iliamua watu wapewe risiti badala ya kutumia muda mrefu kuwapa kadi. Ili baadae watambulikane wote waliojitokeza wapewe kadi zao za kupigia kura. Uandikishaji ulikwenda vizuri zaidi alipowasili kiongozi mmoja mkubwa wa serikali. Kila mtu alikuwa na tamaa ya kuwahi ingawa wengine tulitegemea pingamizi.
Ilipofika saa tano mchana, mara tu baada ya kuondoka yule mkuu hali ilibadilika. Makundi ya askari wa kuzuia fujo, FFU yalivivamia vituo karibu vyote ya ng'ambo mjini. Watu waliokuwa foleni wakapigwa marungu ili waondoke. Watu wengi waliumia. Gari la polisi lililetwa kuwasomba majerhi. Mimi nilikuwa miongoni mwa watu tuliopata virungu ingawa nilikuwa nimeumia sana lakini nilifaulu kukimbia hadi uchochoroni. Kaka yangu yeye hakujeruhiwa. Tulikimbia pamoja kwa hatua chache. Nilianza kunyong'onyea. Kugundua hali hiyo, kaka yangu akanibeba. Kulikuwa na sababu ya kufanya hivyo. Watu waliopigwa bila kosa lolote baadaye kupelekwa hospitali, bali walipelekwa rumande bila matibabu wakisubiri kubambikizwa mashitaka ya kufanya fujo kituoni. Mungu tuhurumie waja wako.
Baada ya muda mfupi nilipoteza fahamu nimeletwa hapa ili kupata matababu. Bali hapa nisalama zaidi kuliko hospitali. Kwanza nisingetibiwa kwa vile singepata fomu ya polisi PF 3. Ndivyo tunavyotakiwa. Tunaambiwa tumelewa, tumepagawa kwa kutaka ukubwa na uroho wa madaraka Akutukanae hakuchagulii tusi.
Baadaye kituo 'wana maskani'. Wakaendelea kuandikana tena na tena. Ole wako ufunue domo lako, utakung'utwa virungu ushike adabu yako.Nani kakuambia ulete
Ulevi wako wa Kipemba. Ulevi huu mbaya jamani.Lakini wanywaji watakosekanaaje
|
|