Lipumba kuzushiwa kesi
ZIPO taarifa kwamba ipo kamati ya watu watano ambao kazi yao ni kuleta farka na fitna kati ya wapiga kura na vyama vyao.

Aidha, kamati hiyo, habari zimedai kuwa inaandaa mipango ya kuwazushia kesi baadhi ya wagombea kwa maslahi ya chama chao.

Katika hatua ya awali watu hao wameandaa 'jungu' la kuwafitini Waislamu na Prof. Lipumba. Inasemekana wameghushi maandiko wanayodai ni makubaliano ya CUF na Waislamu.

Habari zinasema kuwa watautumia waraka huo kudai kuwa CUF imewasaliti Waislamu kwa kumpokea Christopher Mtikila.

Aidha, watadai kuwa Amir Mbukuzi kama kiongozi wa Shura ya Maimamu amevunja makubaliano hayo.

Kamati hiyo ya watu mashuhuri, imedaiwa pia kupika mgogoro kati ya CHADEMA na CUF. Japo haijafahamika mkakati gani watatumia, lakini inasemekana watayatumia makundi ya vijana ndani ya vyama hivyo.

Habari za ndani kutoka ofisi vinapofanyikia vikao hivyo, zimeeleza kuwa upo mkakati pia wa kuvitumia baadhi ya vyombo vya habari kutekeleza dhamira zao.

Habari hizo zinaeleza kuwa vyombo hivyo vitanunuliwa ili viache utaalamu wao visambaze habari za fitna na farka dhidi ya baadhi ya wagombea na vyama vyao.

Habari hizo zimeelezwa kuwa ni pamoja na zile zitakazojenga chuki na kufarakana baina ya watu dini wa tofauti katika baadhi ya vyama wanavyovipiga vita.

Baadhi ya Waislamu waliokwisha zipata habari hizi wameeleza masikitiko yao juu ya fitna hizo walizodai zisizojenga bali kubomoa maslahi ya nchi.

Wamesema dhana ya waraka huo wa kughushi ni kuwa Waislamu wao hawana haki wala uhuru wa kuingia siasa ila kwa kutumiwa.

Kwa dhana hiyo wanajenga fitna wahamie kwao wapate kuwatumia wao.

Wamesema, dhana hiyo ni ya kuwadhalilisha Waislamu na kwamba haina budi ikomeshwe.

"Lazima tufanye juhudi tuwajue watu hawa wafitna, tuwahoji ni wapi hasa wanataka kuipeleka nchi hii kwa fitna zao", amesema muumini mmoja.

"Fitna haijengi bali hubomoa, wakiachiwa wataiharibu nchi", alimalizia maoni yake.

Habari tulizozipata tukienda mitamboni zimedai kuwa baadhi ya watu walimpigia simu Amir Mbukuzi wakidai kuwa kamtumia 'fax' Lipumba akidai kajitoa yeye na Waislamu.

Watu hao waliojitaja kama waandishi wa habai walidai kuwa wana nakala za fax hizo wakidai zina sahihi ya Mbukuzi.

Sheikh Mbukuzi mwenyewe amekanusha habari hizo na kusema ni mbinu zile zile za kuwatukana Waislamu.

Sheikh Mbukuzi amewatahadharisha wananchi kuwa madhalimu wa haki zao watatumia kila mbinu hata zile za kughushi sahihi za watu.

Amewataka wasizugwe na hadaa hizo bali wawe makini kuwatambua na kuwapiga pande.

Amesema, kwa vile madhalimu hawataki haki watatumia hata mbinu za kughushi shahada.


Shemejie Mkapa anadiwa kanisani

MGOMBEA Ubunge (CHADEMA) jimbo la Moshi mjini, Philemon Ndesamburo amesema, CCM na mgombea wake haiuziki kwa wananchi.

Kwa ajili hiyo amesema, imeamua kumuuza mgombea wake Ubunge ndani ya Makanisa.

Mgombea Ubunge wa CCM jimbo la Moshi mjini ni Bibi Mary Minde aliye, shemejiye Rais Mkapa.

Bw. Ndesamburo katika mkutano wake wa kampeni huko Pasua mwishoni mwa wiki ameilalamikia Tume ya Uchaguzi kuhusu hatua ya CCM kumnadi mgombea wake ndani ya Makanisa.

Habari kutoka Moshi mjini na Hai zimeeleza kuwa viongozi wa CCM mkoa wamekuwa wakiwatambulisha wagombea wake kabla ya misa.

Jumapili iliyopita, mgombea Ubunge Mama Minde na mgombea Udiwani kata ya Majengo walitambulishwa kwa waumini katika kanisa la Majengo.

Hali imeelezwa kuwa ni hiyo hiyo huko Hai ambapo CCM inaonekana kuwa na hali ngumu.

Mapema wiki hii mgombea Ubunge wa CCM alifanya mkutano wake kata ya Bondeni ambapo wahudhuriaji walikuwa watoto na watu wazima wachache wenye sare za CCM.

Kata hiyo ya Bondeni imekuwa ikijulikana kama ngome ya CCM.

Hata hivyo siku iliyofuatia CHADEMA na CUF nao walifanya mkutano wao hapo hapo.

Mkutano huo wa kumnadi mgombea wao Ndesamburo ulifurika watu jambo lililotafsiriwa kuwa ni ishara ya kuvunjika ngome hiyo ya CCM.

Hali hiyo imeleta mtafaruku ndani ya timu ya kampeni ya CCM ambapo vijana kadhaa wamejitoa.

Katika mkutano huo Bw. Philemon Ndesamburo alisema kuwa Bondeni ndio kata pekee katika mji wa Moshi iliyotoa mchango mkubwa wakati wa kupigania uhuru.

Wakati TANU inapigania uhuru, Mwalimu Nyerere akija Moshi alikuwa akipokelewa na kulala Bondeni.

Hata hivyo Ndesamburo amesema ni kata hiyo imeachwa bila maendeleo ikilinganishwa na kata nyingine.

Imeachwa na barabara mbovu na kuwa kata pekee isiyo na shule hata moja.

Bw. Ndesamburo amewataka wananchi wa kata hiyo wampe kura kuwaletea barabara nzuri, huduma za afya na elimu.

Amesema yeye hagombei Ubunge kutafuta ajira wala gari zuri kwani vyote hivyo anavyo tayari.


Sheria kutofahamika ni hatari katika utoaji haki - Jaji Mkuu

SHERIA zinazotumika katika vyombo vya sheria hazijulikani kwa wananchi kwa viwango vinavyofaa dosari ambayo ni hatari katika utoaji wa haki.

Katika hali hiyo ipo hatari ya wananchi kutoweza kupima vilivyo iwapo vyombo vya sheria vinatekeleza wajibu ipasavyo au la.

Hayo yamesemwa na Mheshimiwa Jaji Mkuu, Barnabas Samatta katika sherehe ya uzinduzi wa Kitabu "Mashtaka ya jinai na utetezi" kilichoandikwa na mwanasheria maarufu nchini Dk. Abdallah Saffari.

Sherehe hiyo iliyoandaliwa na umoja wa wachapishaji Tanzania (UWAVITA) ilifanyika katika ukumbi wa maktaba kuu jumanne wiki hii.

Jaji Mkuu alisema ili wananchi waweze kujua taratibu zitumikazo mahakamani, hapana budi wanasheria kuandika vitabu kwa lugha asili vitakavyowasaidia kuwa na uelewa wa mambo muhimu ya sheria zinazohusu maisha yao na yanayohusu uendeshaji serikali kwa ujumla.

Amemtaja Dk. Saffari, kwa kuandika kitabu hicho, kuwa ni mmoja wa watu waliotoa sehemu ya msaada katika kuwawezesha wananchi kuwa na ufahamu wa mambo yanayohusu sheria.

"Hii ni hatua muhimu katika juhudi za kuwawezesha wananchi kuelewa kwa kiwango kinachotakiwa sheria tatu ambazo zinatumika karibu kila siku mahakamani", alisema Jaji Samatta.

Alizitaja sheria hizo kuwa ni kanuni ya Adhabu(Penal Code), sheria ya mwenendo wa jinai (Criminal Procedure Act) na sheria ya ushahidi (Evidence Act) ambazo amesema Dk. Saffari amezielezea kwa kina na kwa lugha ya kawaida na nyepesi katika kitabu hicho.

"Dk. Saffari ametoa sehemu ya msaada ambao wananchi wanahitaji katika kutekeleza wajibu wao katika kuendeleza ujenzi wa demokrasia na utawala wa sheria nchini", Jaji mkuu aliwaambia waliohudhuria hafla hiyo.

Aidha alisisitiza kuwa kitabu cha Dk. Saffari manufaa yake hayatakuwa tu kwa wananchi wasio weledi wa sheria bali pia kwa watumishi wa vyombo vya sheria na utoaji haki, jeshi la polisi na kwa wakufunzi wa sheria.

"Ni kitabu ambacho nitashangaa kikikosekana kwenye maktaba za vyuo vinavyoendesha masomo ya sheria, kwenye maktaba za mahakama, jeshi la polisi na zile za jeshi la magereza", Jaji mkuu alisema.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo mwandishi wa kitabu hicho Dk. Abdallah Saffari alisema aliamua kukiandika kitabu hicho ili pamoja na kuwaelimisha wananchi juu ya mambo yanayohusu sheria, kufuta dhana potofu ya baadhi ya watu kuwa kiswahili hakijaweza kujitosha kuweza kutumika katika taaluma mbali mbali Sheria ikiwa miongoni mwa hizo.


Ni Waislamu wanaodumisha amani- Sheikh

IMEELEZWA kuwa hali ya amani na utulivu ambayo ipo nchini inadumishwa na kuendelezwa na Waislamu na sio kweli kwamba inadumishwa na chama tawala cha Mapinduzi (CCM) kama viongozi wa chama hicho na serikali wanavyojinadi.

Hayo yameelezwa na Sheikh Zuberi Yahya Mussa katika khutba ya Ijumaa Msikiti wa Kwa Mtoro uliopo Kariakoo Jijini Dar esSalaam Ijumaa iliyopita.

Sheikh Zuber alisema kuwa Waislamu ndio wenye kudumisha amani na utulivu uliopo nchini kwa vile ni wavumilivu na wanyenyekevu licha ya madhila waliyonayo hapa nchini.

"Tusidanganyane, Uislamu na Waislamu kwa ujumla ndio wanaodumisha amani na utulivu huo uendelee kudumu na sio kweli kama kuna wanaodumisha zaidi yetu na iwapo tutachoka nayo hakuna atakayeweza kuitunza na kuidumisha", alisema Sheikh huyo.

Alisema kuwa pamoja na maonevu, dhulma na kila aina ya kero wanayopata na kufanyiwa Waislamu wanavumilia na kuyapuuza, lakini siku wakichoka hao wanaojipitisha na kujitapa wataumbuka kwa vile hakuna atakayewatuliza Waislamu.

"Waislamu siku wakichoka na kutaka kujitetea hakuna chombo chochote au kikundi fulani kitakachoweza kuwatuliza lakini kwa vile Waislamu ni wapole na wanyenyekevu wanaendelee kuvumilia kwa kutambua umuhimu wa amani nchini na sio chama fulani ndicho kinachodumisha amani hiyo", Sheikh alisisitiza.

Kwa muda mrefu kumekuwa na propaganda ambazo hutolewa na chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa chama hicho ndicho kinachodumisha amani iliyopo na kutahadharisha kuwa watakaoichezea watakiona cha moto ingawa ndani ya chama hicho kupitia serikali yake ndio huwa wa kwanza kutaka kuleta vurugu na kuchafua amani hiyo.

Mfano wake ni kitendo cha askari polisi kuwaua Waislamu katika vurugu za Msikiti wa Mwembechai na matamshi ya kuwaita Waislamu wahuni na wauza madawa ya kulevya.

Sio hayo tu bali pia vitendo vya kukamatwa na kuteswa kwa viongozi wa Kiislamu kwa tuhuma mbalimbali za kupakaziwa ni hali ambayo iwapo Waislamu wataamua kujitetea basi hakuna shaka amani itatoweka.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook