CCM msije Lukanga
Hamna cha kutueleza

WAKAZI wa kijiji cha Mkola kata ya Lukanga wilayani Mkuranga wamewataka wagombea wa CCM wa ngazi zote kutojisumbua kwenda kijijini hapo kuomba kura.

Aidha wameishutumu serikali ya CCM kwa kushindwa kujenga shule kijijini hapo hivyo kuifanya Mkola kutokuwa na Shule tangu nchi ipate uhuru.

Wakiongea na Mwandishi wa habari hizi, wakazi hao wamesema zaidi ya watoto mia nne hukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu kutokana na kukosekana shule.

Wakazi hao wamelalamika kuwa watoto wa kijiji hicho hulazimika kusaidia shughuli za nyumbani wanapofikia umri wa kwenda shule kutokana na kutokuwepo shule kijijini hapo.

Wamesema ili mtoto aweze kusoma hulazimika kutembea umbali wa kilometa 12 toka Mkola kwenda kijiji cha Mkwikwi iliko shule.

Wananchi hao wamemweleza mwandishi kuwa mbali ya kutokuwepo shule vile vile hakuna usafiri wala mawasiliano mengine hali ambayo wameieleleza kuwa ni ya aibu kwa nchi iliyojitawala kwa miaka 40.

Wamesema ni vigumu kwa mtoto wa miaka saba kuweza kutembea kilometa 12 kwa miguu.

Wakionesha kukerwa na kitendo cha watoto wao kukosa masomo, wamesema kuwa katika uchaguzi wa 1995 waliazimia kuisusa CCM lakini wakabadilisha uamuzi wao kutokana na CCM kumsimamisha mwalimu waliyemtaja kwa jina la Mlawa.

Wamedai kuwa walipata imani kutokana na kuwa mwalimu ni mtu anayefahamu vizuri umuhimu wa kwenda shule hivyo wakadhani angeishinikiza serikali ya chama chake kujenga Shule Mkola.

Wamesema wamegundua kuwa tatizo au ufumbuzi ndani ya CCM sio mtu bali sera zake ndizo zilizowabakisha katika hali hiyo ya kukosa elimu vijana wao.

Mwanachama mmoja wa CCM kijijini hapo ambaye ni maarufu kwa jina la mkereketwa amesema pamoja na kuwa yeye ni mwanachama wa CCM lakini atahakikisha chama hicho kinakosa ushindi jimbo la mkuranga.

Mkereketwa huyo ameazimia kuwahamasisha wanakijiji wenziwe wawape kura wapinzani ambao amesema huenda wakawakumbuka.

"Kama Serikali ya CCM imeshindwa kuwajali watoto wetu kuwapatia elimu angalau ya msingi tangu tumepata uhuru unadhani watafanya hivyo sasa wakati kila kiongozi anajali maslahi yake binafsi, amehoji mwanachama huyo wa CCM mwenye watoto wa watatu waliofikia umri wa kwenda shule lakinikutokana hali hiyo imeshindikana kusoma.


Madalali wa kura wakwama Tanga

UJUMBE wa watu wawili uliodaiwa kutumwa na chama tawala kurubuni kura za Waislamu Tanga ili wakipigie kura chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao, yasemekana kuwa umeshindwa kufanikisha azma yake hiyo.

Badala yake, imeelezwa kwamba ujumbe huo umeambiwa kuwa Waislamu ni wakombozi wa nchi hii na hivyo katu hawatoweza kuwa vibaraka wa kuwakandamiza wananchi wenzao.

Hayo yameelezwa na wananchi watatu wenyeji wa Tanga, wawili wa makamo kati ya miaka 60 - 70 na watatu akiwa kijana wa kati ya miaka 40 na 45.

Katika maelezo yao, watu hao ambao walizungumza na AN-NUUR kwa masharti ya kutotajwa majina yao na anuani zao, walisema kuwa walikutana na ujumbe huo mwanzoni mwa wiki hii mjini Tanga.

"Mabwana hao wawili kwanza walikuja nyumbani kwangu baada ya salat Asr, wote ninafahamiana nao, hata hawa wenzangu pia wanafahamiana nao", alieleza mmoja kati ya watu wale watatu waliokutana na ujumbe huo nyumbani kwake mjini Tanga.

Bwana huyo alieleza kwamba wajumbe wale walipofika nyumbani kwake walimwambia kwamba wametumwa toka kwa viongozi wa juu wa chama na serikali Dar es Salaam pasipo kuwataja viongozi hao. Aliendelea kueleza kuwa watu wale walimueleza kwamba wametumwa kuomba ushirikiano wa kazi ya kufanikisha ushindi wa chama tawala katika uchaguzi mkuu ujao.

Alieleza Bwana huyo kwamba watu wale walimtaka atafute watu wengine wenyeji wa Tanga wenye uwezo wa kuzungumza kwa fasaha na uwezo wa kushawishi ili wazungumzie kwa kirefu ujumbe waliotumwa.

"Hivyo tukakubaliana kukutana siku ile ile nyumbani kwangu jioni, baada ya swalat Al-Magharib, nami nikawaalika wenzangu hawa wawili", alieleza Bwana huyo.

Katika mkutano wao huo, alisema, wajumbe wale walieleza kwamba chama tawala kimo hatarini kushindwa katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na Watanzania walio wengi kutokipenda chama hicho kama ilivyokuwa zamani. Kwamba wananchi wanakichukia chama tawala kutokana na hotuba za Prof. Lipumba kuwa chama hicho kimeshindwa kuwaletea Watanzania maendeleo na badala yake kimeendeleza umaskini, maradhi na ujinga.

"Hivyo wakatuambia kuwa chama kimeunda ujumbe kwenda kila mkoa, kama vile wao walivyokuja Tanga na kwamba katika kila mkoa kutakuwa na kamati ndogo itakayokuwa na jukumu la kuwaendea watu muhimu kila wilaya, tarafa, kata, na hata mtaa kwa mtaa ili kushawishi wananchi kubadili muelekeo wao", alieleza Bwana huyo yale yaliyoelezwa na ujumbe ule uliodai kutumwa toka Dar es Salaam.

"Lugha ya wale mabwana ilijaa ushawishi wa kutumia pesa kuwahonga wananchi ili wakipende chama hicho na kuacha kuunga mkono hutoba za Prof. Lipumba, CUF na CHADEMA", alifafanua Bwana huyo jinsi alivyowaelewa wajumbe wale.

"Sisi tulishindwa, tuliona ni muhali na haiwezekani tutumiwe kuwashawishi wananchi wakubali kuendelea kukandamizwa na dhulma za kila aina ambazo hatukutarajia kuziona baada ya nchi yetu kupata uhuru", alisema Bwana huyo aliyeshiriki harakati za kupigania uhuru wa nchi hii. Aliyasema hayo mbele ya wenzake aliokuwa pamoja nao wakati wa mazungumzo na ujumbe ule.

Alisema, wasingelithubutu kupeleka nyuso zao mbele ya wananchi ambao wamechoshwa na dhulma hizo.

"Tuliwakumbusha kuhusu wananchi wa Ndumi jinsi walivyopigwa ovyo na kuumizwa kwa kisingizio eti cha kuzuia ukataji wa mikoko".

"Tuliwakumbusha pia jinsi wananchi wa Monga, na kwengineko ambako wavuvi walikamatwa na kulishwa pweza na samaki wabidhi eti kwa kosa la uharibifu wa mazingira".

"Tuliwakumbusha vile vile jinsi wazee wa Kigombe walivyoteswa eti kwa kuvua bila ya leseni wakati ni wao waliolazimisha wavuvi kwenda baharini na leseni ambazo ni karatasi nyepesi kulowa na kuchanika", alisema Bwana mkombozi veterani wa nchi hii.

'Veterani' huyo alimueleza mwandishi wa AN-NUUR kwamba wajumbe wale kwa kujua kuwa yeye ni msomi wa dini ya Kiislamu (alimu) walijaribu kumshawishi kuwa afanye kazi kubadili msimamo wa wananchi wa Tanga hususan Waislamu ili wakipigie kura chama tawala.

"Mimi ni Muislamu wa kweli, naipenda dini yangu na nchi yangu, siwezi kukubali kuwa kibaraka wa kutumika kuwafanya Waislamu ngazi ya kuendeleza dhulma nchini", alisema Bwana huyo.

Wamesema, hali duni ya maisha ya wananchi wengi wa Tanga ndiyo hali halisi ya mikoa mingi nchini ambapo wananchi vijijini hata mijini wanalazimishwa kulipa kodi ya maendeleo pasipo kupewa maendeleo yoyote.

Walisema kuwa waliwajibu wajumbe wale kwa kuwapa mifano ya Tanga kwa kuwa wote waliokuja walikuwa ni wenyeji wa Tanga.

Pamoja na mifano ya madhila waliyoyataja, mabwana hao walisema kuwa waliwaeleza wajumbe wale kuwa waliodhulumiwa nchini siyo Waislamu tu peke yao.

"Baada ya kubishana nao wakajidai kuwa CCM na serikali yake wapo tayari kuwasikiliza Waislamu na kuwatendea kila wakitakacho, eti Waislamu wa Tanga tuorodheshe mahitaji yetu", walisema mabwana hao katika kueleza mbinu nyingine walizokuja nazo wajumbe.

"Sisi tuliwaambia kwamba Waislamu si wajinga kiasi cha kupumbazwa na madhalimu walioua Waislamu Mwembechai kisha wakajibu kwa fedhuli", walisema Mabwana hao na kuongeza, "tuliwaambia pia kuwa waliodhulumiwa nchi hii si Waislamu tu, Tanga kwa ujumla tumeonewa zaidi".

Wakifafanua hoja hiyo, walisema kuwa kabla yauhuru Tanga iliendelea kiuchumi, kiliemu na katika nyanja mbalimbali za ustawi wa jamii. Wasomi wengi wa Kibondei ambao pia kwa idadi ni Waanglikana walikuwemo katika idara mbalimbali za serikali.

Lakini Ukatoliki ulipopewa nafasi kubwa serikalini kama ilivyoelezwa kwenye vitabu vya historia (Van Bergen na Sivalon), walisema mabwana hao, Tanga wanaathirika.

Bwana huyo wa Makamo ambaye ni alimu (msomi wa dini ya Kiislamu) na ambaye pia anafamaika mjini hapa kama mmoja wa waliokuwa vijana shupavu walioineza TANU mkoani Tanga katika miaka ya 1950, alisema kuwa watu wake wawili waliounda ujumbe ule wote ni wenyeji wa Tanga.

"Mmoja anaishi Dar es Salaam na ni mfanyakazi katika Idara ya serikali... nadhani ana cheo, na huyu mwingine yeye ni mstaafu aliyewahi kushika wadhifa mkubwa serikalini, na tunaishi nae hapa Tanga" alisema Bwana huyo alipokuwa akiwataja wajumbe wale waliomuendea, huku akisisitiza kwa mwandishi wa AN-NUUR masharti ya kutotaja majina wala anuani za wajumbe hao.


Wakatoliki waorodhesha shahada za kura

WAUMINI wa madhehebu ya wakatoliki wamedaiwa kuanza zoezi la kuorodhesha nambari za shahada za wapiga kura wao katika kipindi hiki cha kampeni.

Mmoja wa waumini wa madhehebu hayo ya kikristo anayeishi eneo la Mabibo jirani na chuo cha usafirishaji amedai kuwa jumapili iliyopita walitakiwa kupeleka shahada za kura zikaorodheshwe katika vitabu vya kanisa.

Amesema habari zinazozungumzwa makanisani hivi sasa ni juu ya uchaguzi mkuu ujao na chama kipi ambacho imeamuliwa waumini wa dhehebu hilo wakipe kura.

Amesema wametakiwa wawapigie wachamungu katika nafasi za urais na wabunge.

Muumini huyo aliyekuwa akiongea na mpasha habari wetu amesema wachamungu hao ni wagombea wa CCM walio waamini wa madhehebu hayo.

Kijana huyo aliyeonekana kutokuridhishwa na wito huo wa kanisa lake wakati akitoa taarifa hiyo amedai yeye hayuko tayari kutii hilo kwa kuwa ana uhuru wake kumchagua mtu anachoona kinafaa.

Gazeti hili lilipowasiliana na uongozi wa madhehebu hayo kuhusiana na suala hilo ilifahamishwa kuwa msemaji wa kanisa hilo aliyetajwa kwa jina la Father Pius Rutechula alikuwa safarini kikazi Arusha na simu ya jimbo kuu(113223) haikuwa na majibu.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook