Acheni propaganda tuelezeni sera za vyama

KILE kipindi muhimu cha uchaguzi wa kitaifda kimefika. Ni muhimu kwa sababu ni wakati ambapo wananchi wanapata nafasi ya kuelewa na kujua ni chama au mgombea gani atakuwa na manufaa kwao na taifa kwa ujumla. Ni wakati ambapo kila aliye mgombea anapata nafasi ya kuwaeleza wapiga kura na wananchi kwa ujumla, nini matarajio yake na ya chama chake watakachokifanya pindi wakifanikiwa kupata uongozi wa nchi.

HIKI ni kipindi muhimu kwani ni wakati pekee wananchi wanapoweza kuelewa sera za vyama mbalimbali na kuweza kulinganisha ipi iliyo bora na yenye manufaa kwao na nchi yao. Hapa siyo mahali pa mchezo au lelemama. Hivyo kila chama na wagombea wao wanatakiwa kuwa makini sana katika kuzieleza sera zao ili zipate kueleweka na wapiga kura.

Ni bahati mbaya kwa nchi yetu kipindi hiki hakitumiki vizuri, bali ni wakati wa kubaguana na kukejeliana ili tupate fundi wa kukejeli wengine na sio sera zitakazotuletea mafanikio na maendeleo ya nchi yetu. Huu wakati ndiyo unaotumiwa na vyombo vya habari kueneza propaganda na uzushi juu ya wagombea wengine na vyama vyao. Ni wakati wa kusikia vitu na maneno ya ajabu badala ya nini matarajio ya wagombea na vyama vyao. Hata wagombea wakieleza sera kwenye mikutano yao ya kampeni, utasikia vyombo vya habari vinaleta propaganda zao ili kuwababaisha wananchi wasielewe nini vyama na wagombea wanasema.

Hii hali ni msiba mkubwa sana kwa taifa letu, kwani hatutakaa tuje tupate viongozi na vyama bora kama tabia hii haitaachwa. Inatubidi ndugu wananchi tuelewe kuwa uzuri wa viongozi ni mafanikio yetu sote na taifa letu na siyo kikundi tu cha watu. Lakini hapo hapo tuelewe kuwa ubaya wa viongozi ni hasara yetu sote na sio baadhi tu ya watu.

Wale wote wanaotunyima nafasi wananchi kuwaelewa na kuwachagua viongozi wazuri hao ni maadui wakubwa wa nchi yetu, na hatuna budi kuwapiga vita ili wasiendelee kutuletea hasara ya kuwa na viongozi wabovu.

Ni jambo la kusikitisha wakati umuhimu wa uchaguzi unaeleweka na vyombo vyote vya habari, lakini ni hao hao ndiyo wanakuwa wa kwanza kuupuuza huo umuhimu. Sielewi ni kwa vipi hotuba za wagombea katika kampeni zao zisipewe umuhimu wakati huu tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi.

Kwa mwenendo mzima unavyokwenda inaelekea kweli Tanzania ina vyombo vingi vya habari kama redio, magazeti na televishni, lakini hivi vyote sio kwa faida ya kuwaletea wananchi maendeleo bali na kwa ajili ya kuupotosha umma ili taifa letu lisiweze kusonga mbele.

Nani asiyeelewa kuwa huwezi kuwa na nchi iliyo na maendeleo bila ya kuwa na uongozi ulio mzuri. Mwanzo wa uongozi mzuri ni kwenye uchaguzi. Huwezi kumchagua usiye muelewa, ndiyo maana tunahitaji vyombo vya habari ili viweze kutupaia nafasi ya kuwasikia wagombea hasa wa Urais kwani wao ndiyo wenye kubeba uzito wote wa vyama vyao. Wao ndiyo watakaotupa sera na kutuwezesha kuvielewa vyama vyao. Wao watatupa matumaini ya nini tutarajie watakapoingia madarakani.

Tabia ya kibaguzi inayofanywa na vyombo vya habari viwe vya umma au binafsi, ya kutoa taarifa za kibaguzi kwa baadhi ya vyama na vingine kutuletea ratiba zao tu bila ya nini wanasema haitusaidii sisi wananchi wala hao wenye vyombo vyao, kwani hii nchi ni yetu sote na maendeleo au kutokuwa na maendeleo sio kwa hivyo vyama tu bali ni kwa taifa letu sote.

Tumechoka kusikia propaganda toka kwa waandishi, tunataka tuwasikie wagombea wenyewe kwani sisi wananchi tuna akili ya kupima tunayoambiwa kama ni ya msingi au laa. Siyo kazi ya mwandishi wa habari kutufafanulia mawazo yake na kuyafanya kuwa ndiyo maamuzi yetu sisi wananchi. Tabia ya kututisha kwa vijambo vya mitaani kuwa ndiyo sera za vyama tumechoka kuzisikia na kuzisoma magazetini.

Kama ni wenye kupenda kweli amani na utulivu tuachieni na mtupe nafasi wananchi ya kuzisikia sera za vyama na wagombea wao ili tuje kupata viongozi walio bora na wenye faida kwetu sote.

Litakuwa ni jambo la maana sana kama waandishi mtaacha kuwafitinisha wananchi na wagombea wao kwa kutueleza habari za kusadikika kwa sababu tu mtoa habari ana chuki zake binafsi na chama au mgombea huyo. Siri ya uchaguzi ni uwe wa haki na huru, ndipo ile amani yetu itaweza kuwa ni ya kudumu. Kwani kuna gharama gani kutenda hiyo haki kwa wagombea wote ili wawe na nafasi sawa kwa wananchi wakati wa uchaguzi?

Tunachotakiwa wananchi wote na vyombo vya habari kuipenda nchi yetu kwa kutenda haki. Usipotenda haki kwa upande wako ujuwe ni sumu hiyo unayoweka kwani atakayechaguliwa usimlaumu naye akijakufanya kazi yake kwa upendeleo.

Tunaloliweza tulifanye tusingoje mpaka mambo hayaharibike na tukaja kuwa ni watu wenye kujuta.

Uhuru, Amani na Maendeleo ndicho tunachohitaji Watanzania na si vinginevyo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook