Nyerere atoa amri kwa Usalama wa Taifa kumkamata Mufti Hassan Bin Amir
Mkutano wa Taifa wa Waislamu, 1968

HII ni sehemu ya saba ya mfululizo wa makala ambazo ni sehemu ya muswada wa kitabu "Mwalimu Julius K. Nyerere, Kanisa Katoliki na Uislamu: Dola na tatizo la Udini Tanzania" kitakachotoka hivi karibuni. Kitabu hicho kimeandikwa na mwandishi maarufu wa masuala ya historia hasa ya Tanganyika BWANA MOHAMMED SAID.

TANU ilipoasisiwa, Sheikh Hassan bin Amir alikuwa akiwakatia watu kadi za TANU msikitini huku akidarsisha.

Baadhi ya wanachama shupavu wa TANU ambao Sheikh Hassan bin Amir aliwaingiza katika TANU ni Sheikh Mussa Rehani ambae alipewa kadi yake ndani ya msikiti Kigoma.

Wakati Nyerere alipokuja TAA Dar es Salaam mwaka 1953, alimkuta Sheikh Hassan bin Amir mwenyeji katika siasa. Baada ya uhuru Sheikh Hassan bin Amir alijiuzulu siasa, kutokana na kauli yake alisema kuwa, ili awatumikie Waislam vyema.

Nyerere alifahamu fika kuwa haitakuwa rahisi kwake kumweka Sheikh Hassan bin Amir kizuizini kama alivyofanya kwa Waislam wengine. Sheikh Hassan bin Amir alikuwa ndiyo Mufti wa Tanganyika na Zanzibar na kwa ajili hii alikuwa na hadhi kubwa katika umma wa Waislam. Halikadhalika haikuwa rahisi kwa yoyote kumkiuka Sheikh Hassan bin Amir na kuchukua uongozi wa Waislam.

Mkutano wa Taifa wa 'Waislam', 1968

Hadi kufikia juma la kwanza la mwezi wa Desemba, mikoa mitatu kati ya kumi na saba ilikuwa tayari imeshajitenga kutoka EAMWS. Kile kikundi cha Adam Nasibu kikaunda kamati kwa ushirikiano na Kamati ya Maulidi ya Dar es Salaam, Adam Nasib akiwa katibu na Sheikh Abdallah Chaurembo mwenyekiti. Kamati hii ikaitisha mkutano Ukumbi wa Arnatouglo tarehe 3 Desemba, 1968 kujadilia 'mgogoro'.

Aliyetumiwa kutoa tangazo lile alikuwa katibu wa Kamati ya Maulidi na Swala ya Iddi, Y. Osman. Kundi la Adam Nasib lilikuwa na mchanganyiko wa watu waliokuwa wanaungwa mkono na serikali Adam Nasib akiwa kiongozi, halikadhalika kulikuwa na Waislam waliokuwa na nafasi katika TANU kama Sheikh Abdallah Chaurembo na Juma Sued kiongozi wa TANU kutoka Bukoba. Ilikuwa wazi kuwa serikali ilikuwa inamtayarisha Sheikh Abdallah Chaurembo kuchukua nafasi ya mwalimu wake na mtu aliyemfikisha pale alipo, Sheikh Hassan bin Amir. Ikawa sasa lazima Sheikh Hassan bin Amir aondolewe na kupelekwa Zanzibar ili lile kundi la serikali chini ya Adam Nasibu liweze kuchukua uongozi wa Waislam bila ya kipingamizi chochote.

Wakati wa vurugu hizi Kamati Kuu ya TANU ilikuwa inafanya kikao chake Tanga. Sheikh Kassim Juma, Adam Nasibu, Omari Muhaji, Sheikh Abdallah Chaurembo na Saleh Masasi walipanda ndege hadi Tanga kwenda kushauriana na Kamati Kuu ya TANU jinsi ya kumaliza 'mgogoro' wa Waislamu.

Ujumbe huu ulikwenda Tanga kuonana na Nyerere huku ukiwa na orodha ya Waislamu ambao kile kikundi cha Adam Nasibu walikuwa wanataka serikali wakamatwe na kutiwa kizuizini ili msuguano upate kumalizika.

Dossa Aziz aliona Nyerere akipewa karatasi wakati kikao kikiendelea lakini hakufahamu ujumbe uliokuwamo ndani ya karatasi ile hadi hapo baadae. Alikuja kutambua habari za karatasi ile baada ya majuma mawili kupita wakati alipofatwa na jamaa yake mmoja na kumuomba aingilie kati ili rafiki yake aliyetiwa kizuizini na Nyerere aachiwe kutoka Jela ya Ukonga.

Nyerere alipofahamishwa habari zile na Dossa, alisema kuwa yeye hakufahamu kuwa rafiki yake Dossa alikuwa katika orodha ile ambayo kwa umuhimu wa jambo lile ilibidi aletewe Tanga wakati wa mkutano wa Kamati Kuu. Kwa kejeli Nyerere akamwambia Dossa kuwa yeye huwa hachukuwi tabu ya kusoma majina ya watu anaowaweka kizuizini kwa kuwa anawaamini wale wanaofanya kazi ya kumletea majina yale.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Hamza Aziz, mdogo wake Dossa alipopokea amri kutoka kwa rais kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa amkamate Sheikh Hassan bin Amir, hakuweza kuamini masikio yake. Alitaka afahamishwe sababu za kutaka kukamatwa Mufti ­ kiongozi wa juu kabisa katika safu ya uongozi wa Waislam katika Tanzania.

Alipoambiwa kuwa sababu ni kuwa anaihujumu serikali, Hamza Aziz alimwambia Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa huenda kuna makosa katika amri ile. Alimfahamisha waziri kuwa yeye binafsi alikuwa anamfahamu mzee yule toka yeye Hamza alipokuwa mtoto mdogo. Akimfahamu Sheikh Hassan bin Amir kama mwalimu na mtu aliyeshiriki katika ukombozi wa Tanganyika. Msimamo wake heshima na hadhi yake mbele ya Waislamu ipo juu kabisa. Inspekta Jenerali wa Polisi alimwambia waziri kuwa haitawezekana kwake yeye kutii amri ile kwa sababu yeye haamini kuwa tuhuma zile dhidi ya Mufti Sheikh Hassan bin Amir ni za kweli. Nyerere alifahamishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa Inspekta Generali wa Polisi, Hamza Aziz amekataa kutii amri yake ya kumkamata Mufti. Nyerere alitoa amri kwa Usalama wa Taifa kumkamata Sheikh Hassan bin Amir. Hii ilikuwa ni kinyume na utaratibu kwa kuwa Usalama wa Taifa hawana mamlaka ya kukamata watu.

Usiku wa manane siku hiyo hiyo Sheikh Hassan bin Amir alikamatwa na makachero wa Usalama wa Taifa akapelekwa uwanja wa ndege na kurudishwa Zanzibar.

Miaka mingi baadae Rashid Kawawa alisema kuwa anajuta kuunga mkono kukamatwa kwa Mufti wa Tanganyika na Zanzibar, Sheikh Hassan bin Amir akaelekeza lawama kwa wale waliomshauri kufanya hivyo.

Inaelekea kulikuwa na mpango uliokuwa umetayarishwa kabla ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar kumpokea Sheikh Hassan bin Amir. Inasemekana mara kadhaa Karume alipata kumueleza Sheikh Hassan bin Amir kuwa Nyerere alikuwa hamtaki nchini kwake na akawa anamshauri arudi nyumbani Zanzibar. Sheikh Hassan alikataa ushauri ule hadi alipokamatwa na kurudishwa kwa nguvu. Karume alimpa Sheikh Hassan bin Amir hadhi zote alizostahili kama ulamaa na akamruhusu kuendesha madras. Lakini Zanzibar ilikuwa imebadilika.Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa yameingiza katika Zanzibar fikra potofu zilizokuwa zinapinga Uislam. Karume mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kuchoma vitabu vyote vya dini. Nakala za Qur'an Tukufu zilichomwa moto pamoja na taka za mji. Muslim Academy chuo kilichokuwa kikisomesha masomo ya dini kilifungwa. Mashine za kuchapa kwa lugha ya Kiarabu zikatupwa kutoka Government Press. 61 Maulama wengi na wanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir walikuwa wamekimbia Zanzibar kwenda kuishi uhamishoni. Zanzibar haikuwa tena kitovu cha elimu na maarifa ya Kiislam. Sheikh Hassan bin Amir akawa sasa mfungwa katika nchi yake mwenyewe kwa kuwa hakuwa na ruhusa ya kuondoka visiwani hapo na kurejea Tanzania bara. Mara baada ya kukamatwa kwa Sheikh Hassan bin Amir, Adam Nasibu akatangaza kufanyika kwa mkutano ambao ulikuja kujulikana kama Mkutano wa Waislam wa Taifa. Mkutano ambao ilitangazwa utafanyika Iringa kuanzia tarehe 12-15 Desemba, 1968. Agenda kuu ya mkutano ule ilikuwa kujadili katiba kwa ajili ya jumuiya mpya ya Waislam.

Baada ya kukamatwa kwa Sheikh Hassan Bin Amir Tewa Said Tewa gazeti moja la Kiingerezalilimfuata ili afanye mazungumzo nalo. Tewa alimfahamisha mwandishi kuwa kulikuwa na hofu juu ya maendeleo yanayofanywa na Waislamu na mikutano mikubwa ya Waislam iliyokuwa ikifanyika nchi nzima. Waislamu waliokuwa na vyeo katika serikali walikataa kabisa kuisaidia Tume ya Kikwima kwa njia yeyote wakidai kuwa kufanya hivyo ni sawasawa na kuchanganya dini na siasa. Waislamu hawa walikaa pembeni kama watazamaji huku Nyerere kwa taratibu akivunja uongozi wa EAMWS na kutayarisha watu wake kuwaongoza Waislam. Kundi la Adam Nasibu lilikataa kukutana na Tume ya Kwikima. Maulamaa wa Kiislam ambao walikuwa na hadhi na uwezo wa kuleta sulhu katika sakata ile hawakuweza kufanya hivyo kwa kuwa walikuwa wanajua fika kuwa aliyekuwa akivunja EAMWS hakuwa Adam Nasibu, yeye na wenzake walikuwa wakitumiwa tu. Kundi la Adam Nasibu lilikuwa halitaki chochote ila EAMWS ivunjwe na badala yake iundwe jumuiya itakayokuwa chini ya kivuli cha serekali. 63 Vilevile kukawa na uvumi kuwa Muislam yeyote ambae atakaejejihusisha na shughuli za EAMWS atawekwa kizuizini na serekali. Tume ya Kikwima haukuweza kupuuza vitisho hivyo kwa sababu serekali ilishawahi kuwaweka vizuizini masheikh.

Tume ya Kwikima ilikuwa inafahamu lile kundi la Adam Nasibu halikuwa na nguvu wala uwezo wa kuivunja EAMWS. Kufuatia kutangazwa kwa mkutano wa Iringa wa kundi la Adam Nasibu, Tume ya Kwikima ilitoa taarifa yake tarehe 11 Desemba ­ siku moja kabla ya mkutano wa Iringa kuanza. 64 Taarifa ambayo ilitolewa kwa Waislam wote, iliitisha mkutano mkuu wa EAMWS ambao ulikuwa ufanyike mwezi Februari mwaka unaofuata kujadili na kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu 'mgogoro'. 65 Tarehe ya mkutano ilibadilishwa hapo baadae na kuwa Januari kutokana na umuhimu wa 'mgogoro' uliokuwa ukikabili EAMWS. Gazeti la TANU baada ya kusoma taarifa ya Kwikima iliamua kutoa maoni yake kuhusu taarifa ile kwa kusema kuwa haikuwa sawa.66 Huu ulikuwa mpango uliosukwa mapema kuonyesha kuwa uongozi wa EAMWS ulikuwa na ubadhirifu. Juma lile lile Aga Khan ambae ndiye aliyekuwa akishambuliwa na kundi la Adam Nasibu, baada ya kutambua kuwa EAMWS isingeweza kamwe kuokolewa, akiwa Paris, Ufaransa alijiuzulu nafasi yake kama patron wa EAMWS.

Wakati Tume ya Waislamu inasubiri mawazo ya Waislam sasa kundi la Adam Nasibu wakijionesha wazi kuwa serikali na TANU ilikuwa nyuma yao, lilikutana kwa ajili ya kile walichokiita Mkutano wa Waislamu wa Taifa ulioanza tarehe 13 Desemba, 1968. Serikali ikifanya kazi nyuma ya pazia ilijitahidi sana kuhakikisha kuwa mkutano ule unafanikiwa. Serikali ndiyo iliyotoa fedha za kufanyia mkutano ule, ukatoa vyombo vyake vya habari kwa ajili ya kuutangaza vizuri na ukatoa ulinzi kwa wajumbe wote.

Rashid Kayugwa Afisa wa Usalama Taifa, Dar es Salaam ndiye aliyepewa kazi ya kudumisha mawasiliano kati ya kundi la Adam Nasibu serikali. Kayugwa ndiye aliyekuwa akielekeza kundi la Adam Nasibu mbinu za propaganda na nini kifanyike na kwa wakati gani ili kuvunja umoja wa Waislamu. Kayugwa alikuwa amepata mafunzo yake ya ukachero Israel, Checkoslovakia na Marekani.

Katika kuhakikisha mafanikio ya mkutano wa Iringa, Kayugwa ambae ni mzaliwa wa Iringa alipendekeza mkutano wa Waislamu wa Taifa ufanyike Iringa kwa kuhofu vurugu na upinzani kutoka kwa Waislamu wa Dar es Salaam. Baada ya kusoma kitabu cha Padri John Sivalon kilichoeleza kuwa Kanisa baada ya uhuru liliendesha hujuma dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kupitia serikali, ndipo ilipomdhihirikia ukweli; kuwa alipokuwa akitumiwa kuhujumu EAMWS hakuwa akitumikia serikali kama alivyokuwa akidhani bali alikuwa akilitumikia Kanisa.

Kama kuomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu, aliamua kueleza mchango wake katika kuwahujumu Waislamu na Uislamu ili iwe fundisho na onyo kwa Waislamu watakao kuwa katika utumishi wa vyombo kama hivyo siku za usoni. Kabla ya kufa kwake alieleza masikitiko yake kwa kukandamizwa kwa Waislamu na akatoa mfano wake mwenyewe wa kutopandishwa cheo katika Usalama wa Taifa kwa sababu tu yeye alikuwa Muislamu.

Wajumbe waliohudhuria mkutano ule wa Iringa walikuwa kama mia mbili. Mkutano huu ulihudhuriwa na Waislam waliokuwa na vyeo katika serikali na TANU, Waislam waliokuwa wakuu wa wilaya na mikoa na Waislam wenyeviti wa TANU.

Waislamu wote wenye majina walialikwa, pamoja na Waislam waliokuwa katika halmashauri kuu ya TANU na baadhi ya wajumbe wa mkutano walitoka Zanzibar.

Ulikuwa mkutano wa wanasiasa Waislamu ambao ukitoa majina yao walikuwa hawana chochote katika harakati za Uislamu isipokuwa majina yao. Lakini uzito wa mkutano huu ulitokana hasa na kuwa ulikuwa mkutano ambao ulitawaliwa na Waislam waliokuwa hawapendezi mbele ya macho ya umma wa Kiislamu.

Ni ukweli usioweza kupingika kuwa kama mkutano ule ungelikuwa hasa umetayarishwa kwa ajili ya kumtumikia Allah, ni wazi ungehudhuriwa na Waislamu wa kweli na wenye historia ya unyenyekevu na mapenzi kwa dini yao. Waislamu wa sifa hizi hawakuwepo katika mkutano ule ukimtoa Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo na wengine wachache ambao kwa kutotambua mambo waliitika mwito. Mkutano ulifunguliwa na Karume na kufungwa na Kawawa. Katika hotuba yake ya ufunguzi Karume alisema maneno haya:

Dini haiwezi kuwa nje ya siasa kwa sababu siasa ndiyo damu inayoipa jamii uhai wake. Wakati wa ukoloni wananchi na daini zao zilikuwa chini ya utawala wa wageni. Hivi sasa watu wamevua mabaki ya ukoloni pamoja na kutawaliwa kwa misingi ya dini. Kuanzaia sasa uongozi wa dini lazima uwekwe chini ya wananchi wenyewe bila ya kuongozwa na kiongozi kutoka nje.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook