ZINGATIO muhimu ni kwamba, lugha ni kipaji alichopewa binadamu pekee ili kumwezesha kujifunza, kuwasiliana, kushirikiana katika kujenga utamaduni utakaowawezesha kulifikia lengo la maisha yao. Lugha ni mpangano wa maneno yenye kuleta maana, fikra na kujenga dhana. Manyani, masokwe, mbwa, ndege na wengineo hawana lugha. Wao wana milio ya mawasiliano. Si lugha hata kidogo!
MILIO hiyo ya kinyama huwawezesha kuwasiliana katika kiwango cha chini sana.
Wanadamu pia huweza kuwasiliana kwa kutumia milio. Mathalan, muluzi, au mtoto anapomlilia mama yake. Si lugha hapo inayotumika, kuwasiliana ni milio tu. Ni sawa na mawasiliano kupitia milio ya kengere, honi, ving'ora au goma la mgambo.
Hata kama kuna baadhi ya wanadamu wataowezeshwa kuelewa maana ya milio hiyo ya wanyama kama alivyoijua Nabii Suleiman (a.s.) kamwe milio hiyo haitokuwa lugha. Mathalan, ikiwa kuna mtu anaijua maana ya mlio wa honi, utamwambia "sogea! Gari hiyo!. Hapo utakuwa umempatia tafsiri. Umeweza kufanya hiyo baada ya kujua maana ya mlio huo.
Mwenyezi Mungu mara nyingine huyanukuu maneno yaliyosemwa na watu wa zamani ili kufikisha ujumbe uliomo au kuonyesha udhaifu wake. Na Nabii Suleimain (a.s.) alipata ujumbe mzito kutoka ndege-Hud hud na sisimizi. Yeye ni mtu pekee aliyefahamu maana ya milio yao. Hivyo, kupitia Qur'an, Mwenyezi Mungu alitaka tuupate ujumbe huo. Ndipo akaitafsiri milio hiyo katika lugha.
"Basi hakukaa sana mara Hud hud akasema: "Nimegundua usiloligundua, na nimekujia hivi kutoka Sabaa na habari zenye yakini. Hakika nimemkuta mwanamke anatawala, naye amepewa kila kitu na anacho kiti cha enzi kikubwa. (27:22-23).
Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu na shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia njia, kwa hiyo hawakuongoka. Hawamsujudii Mwenyezi Mungu....... Mwenyezi Mungu hapana aabudiwaye kwa haki ila Yeye Mola wa Arshi tukufu". (27:24-26).
Ni dhahiri kuwa, si Mtume Muhammad (s.a.w.), mimi wala wewe angeliweza kuupata ujumbe huu, kama Mwenyezi Mungu angelinukuu katika milio ile ya asili aliyoitumia Hud hud. Mtu huweza kuwa sahihi anapouliza" mlio wa kengele ya kanisani unaashiria nini. Ama kwa adhana, atauliza kuwa "maneno yake yana maana gani".
Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, amemuumba mtu. Amemfundisha lugha (55:1,3), na Mola wako ni mkarimu sana. Ambaye amemfundisha mtu kwa kalamu. Amemfundisha mtu mambo yote aliyokuwa hayajui. (96:2-5). Na katika kutofautiana kwa lugha zenu na rangi zenu zipo ishara.
AINA ZA WALIMU
Mwalimu wa kwanza wa binadamu na viumbe vyingine ni Mwenyezi Mungu. Matendo yote ya silka kama vile kula, kunywa, kulia, kucheka na mengineyo yamepandikizwa na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye aliyewafunza ndege kutengeneza viota na kutumbuiza kwa muziki wa sauti zao.
Unapokula asali, unaweza ukastaajabu kwa utamu wake, Utamu huo ni matokeo ya mchanganyiko wa vitu mbalimbali kwa utaalamu wa hali ya juu ambao hata mwanadamu na ujanja wake wa kisayansi na teknolojia haweza kutengeneza asali. Pamoja na utamu wake, asali pia ni dawa inayotibu magonjwa. Wanaotengeneza asali ni viumbe vidogo visiyo na ubongo kama wa binadamu.
Na Mola wako akamfahamisha nyuki ya kwamba jitengenezee majumba katika milima na katika miti na katika yale wanayojenga watu. Kisha kula katika matunda (nectar), na upite katika njia ya Moka wako zilizofanywa nyepesi. Kinatoka matumboni mwao kinywani chenye rangi mbalimbali, ndani yake kina ponyo kwa wanadamu. Hakika katika hayo muna mazingatio kwa watu wenye fikra. (16:68).
Bila ya kuchoka wala uzito, nyuki hushirikiana katika kuendesha kiwanda cha kutengeneza asali iliyo katika ubora ule ule. Kwa pamoja, hujikuta wakizifuata kanuni na hatua za utengenezaji wa asali kwa wepesi kabisa. Tendo la kutengeneza haliwahitaji kufikiri. Ni kama binadamu asivyopata ugumu katika kupepesa macho yake.
Hebu tazama ujuzi na wepesi alionao malaika wa mauti. Uwe kwenye gari, ndege, meli, garimoshi, hadharani au mafichoni, huweza kuutoa uhai wako kwa sekunde ile ile. Tumeshuhudia watu walio vipenzi vya watu wakiiaga dunia. Roho zetu hutolewa kwa uharaka wa ajabu sana! Ndani ya sekunde tu mamilioni ya roho za viumbe hutolewa. Kila malaika, amebobea kiujuzi katika kitengo chake.
Sema: Hakika mauti haya mnayoyakimbia, bila shaka yatakufikeni, Kisha mtarudishwa kwa mjuzi wa siri na dhahiri, hapo atakujulisheni mliyokuwa mkiyatenda. (62:8). Popote mlipo atakufikieni malaika wa mauti hata kama mkiwa katika ngome madhubuti (4:78).
Ujuzi na uhodari wa malaika katika kufanya mambo wamefunzwa na Mwenyezi Mungu. Kama inavyoshuhudiwa namna malaika wa mauti asivyochelea kukata tamu ya maisha ya yeyote yule bila ya kujali majukumu na mategemeo kwa huyo mtu, ndivyo malaika wa motoni wasivyokuwa na huruma dhidi ya madhalimu.
Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu, na moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa amri zake, na wanatenda wanayoamrishwa. (66:6).
Malaika hawajigambi kuwa ujuzi walionao unatokana na wao wenyewe. Kwa maneno ya heshima, walikubali wenyewe kuwa wamefunzwa na Mwenyezi Mungu. Tena si mambo yote. Lakini wapo binadamu ambao, akijua mengi katika jambo dogo akawa na shahada au Uprofesa, anavimba kichwa na kudharau wengine.
Wakasema (malaika) "Utukufu ni wako! Hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha. Bila shaka wewe ni mjuzi na ndiye mwenye hikima. (2:32).
Miujiza waliyoifanya Mitume si kutokana na utaalamu wao binafsi. Fimbo ya Mussa (a.s.) iliyameza mazingaombwe ya ujuzi wa kichawi. Ikapasua jiwe na kububujisha mito. Wenye kubweteka bila ya kufikiri wametokea kuwapa uungu Mitume kutokana na miujiza waliyoifanya.
Kutokana na muujiza wa kuzaliwa kwake bila ya baba, Elimu ya juu aliyokuwa nayo, pamoja na miujiza aliyoifanya Yesu, Nabii Issa amevishwa uungu asiokuwa nao. Sifa hiyo aliyopachikwa inatokana na kutokujuwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye chanzo na mwalimu wa fani zote.
Yesu/Issa akawaambia: Nimekujieni na hoja kutoka kwa Mola wenu, ya kwamba nakuumbieni katika udongo kama sura ya ndege, kisha nampuliza, mara amekuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu na wenye ukoma, na ninawafufu waliokufa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu, na ni Mola wenu. Basi mwabuduni. Hii ndiyo njia iliyonyooka. (3:49-51).
Wapo watu waliogundua mambo mbalimbali bila ya wao kufundishwa darasani au kuona mfano wake katika mazingira yaliyowazunguka. Ni Mwenyezi Mungu anayeziongoza akili zao katika ugunduzi wa mambo kupitia ilhamu (intuition). Ugunduzi huo hutegemea na kukua kwa mahitajio ya jamii ya wanadamu.
Kutokana na husuda, mtoto wa Adam (a.s.) alimuua nduguye. Huyo ndiye alikuwa wa binadamu wa kwanza kumuua mwenzake pasipo haki kama vile Waislamu waliouawa na polisi pale Mwembechai. Baada ya tendo hilo, mtoto yule wa Adamu hakuelewa aufanyeje mwili wa nduguye.
Basi nafsi ikamsukuma kumwua nduguye. Akamwua akawa miongoni mwa wenye hasara. Hapo Mwenyezi Mungu akamleta kunguru anayefukua katika ardhi ili amwonyeshe jinsi ya kusitiri maiti ya ndugu yake. Akasema: "Ole wangu! Nimeshindwa kuwa sawa na kunguru huyu nikaisitiri maiti ya ndugu yangu. (3:30-31).
Matendo yote ya mwanadamu hurikodiwa. Kazi hii hufanywa na malaika wenye ujuzi wa kutosha katika kazi yao. Kila tendo na neno alilosema au kulifanya mtu, hudhibitiwa katika maandishi. Huyu alimuuwa ndugu yake wakiwa wawili peke yao. Yawezekana alidhani hakukuwa anayemshuhudia na kwamba ni siri yake binafsi. Alijidanganya!
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Haupatikani mnong'nao wa watu watatu ila yeye huwa ni wa nne wao. Wala wa watano ila yeye huwa wa sita wao, wala wa chache kuliko hao, wala wa wengi zaidi ila Yeye huwa pamoja nao popote walipo. (58:7).
Kwa dhati yake, Mwenyezi Mungu hulishuhudia kila tukio litendekalo usiku wa giza nene, mafichoni, faragha au hadharani, Yeye hafichwi! Kupitia Qur'an anatufunza kuwa yule mtoto wa Adamu alimwua nduguye pasipo haki. Anatueleza mjadala uliokuwepo kabla ya tukio na yaliyofuatia baada yake.
Na wasomee habari za watoto wawili wa Adamu kwa
kweli walipotoa sadaqa ikakubaliwa ya mmoja wao, na ya mwingine haikukubaliwa.
Akasema: "Nitakuua". Mwenziwe akasema: "Mwenyezi huwapokelea walio wakweli".
Kama utanyoosha mkono wako kwangu, kuniua, mimi sitakunyooshea mkono wangu
kukuua. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu. (5:27-28).
--
![]()
|
|