Kuanzishwa kwa TANU katika Majimbo- 2

MAKOPA, Chembera na Mpunga walikubaliana kuwa kabla ya kuanza kufanya kampeni waziwazi kwa ajili ya TANU, lazima wawaandikishe wanachama wachache kama waasisi wa chama. Mpunga na Chembera walimwandikisha kijana mmoja akiitwa Abdallah Faraj na katika muda mfupi waliweza kuwapata takriban wanachama kumi na tano walioridhia kujiandikisha kama wanachama waasisi wa TANU. Endelea

Baada ya kuandikisha wanachama waasisi mkutano wa siri uliitishwa katika Welfare Centre ambako ndiko alikokuwa akifanya kazi Chembera. Chembera aliwaeleza kwa ufupi wale wanachama wa mwanzo kuhusu malengo na madhumuni ya chama hicho kipya cha siasa. Mkutano huo ulichagua kamati ya watu watatu yaani, Makopa, Chembera na Faraj ili kuwakabili Mnonji na Waziri kuwaleza kuwa TAA haipo tena nchini Tanganyika. Lengo lilikuwa kuwasadikishia kuwa ilikuwa kazi bure na kupoteza wakati kujaribu kuihuisha TAA mjini Lindi wakati ambapo Tanganyika nzima ilikuwa ikisonga mbele na TANU. Baada ya mjadala mrefu sana na mkali wa wale vijana watatu na ule uongozi wa TAA wa wazee, walikubaliana TANU lazima isajiliwe mjini Lindi.

Uchaguzi ulifanyika na Shaaban Msangi, kijana wa Kipare akifanya kazi kwa Smith Mc Kenzie, alichaguliwa rais na Ahmed Seif, katibu. Mpunga, Chembera, Mnonji na Idd Toto walichaguliwa wajumbe wa kamati.

Ahmed Seif alikuwa kijana ambaye ndiyo kwanza amemaliza shule, yeye alikabidhiwa kuendesha ofisi kwa niaba ya uongozi. TANU mjini Lindi ilimwajiri ili kukiandaa chama kiweza kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Hassan Mohamed Kinyozi aliajiriwa kama mhudumu wa ofisi. Hawa wawili walikuwa ndiyo wafanyakazi wa kwanza wa TANU waliokuwa wakilipwa mshahara katika Jimbo la Kusini na wakawa miongoni mwa wafanyakazi wachache sana walioajiriwa na TANU kwa wakati ule. Mnonji alitoa nyumba yake katika mtaa wa Makonde kuwa ofisi ya kwanza ya TANU Jimbo la Kusini.

Baada tu ya kuanzishwa kwa TANU, Athumani Mussa Lukundu, kiongozi wa Lindi Dockworkers' Union, aliunganisha chama chake na TANU. Jambo hili, kwa TANU lilikuwa la kuitia moyo sana kwa sababu Dockworkers' Union ilikuwa na wananchama wengi na hatua ile iliongezea TANU nguvu.

Baada ya muda mfupi tu toka kufunguliwa kwa TANU Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TANU wa mwaka 1955 ulifuatia. Tawi la Lindi lilikuwa tayari lina uhusiano na makao makuu ya TANU mjini Dar es Salaam, na lilikuwa likitarajia kuhudhuria mkutano huo na kukutana na Julius Nyerere na uongozi mzima wa TANU pale makao makuu Dar es Salaam. Mpunga, mwanachama muasisi wa TANU, na Ali Ibrahim Mnjale waliteuliwa kuhudhuria mkutano huo kama wajumbe kutoka Jimbo la Kusini. Halmashauri ya TANU ya Lindi iliwaelekeza wajumbe hawa wafikishe ombi rasmi kwa makao makuu ili Julius Nyerere aje kufanya ziara kusini kwanza, kukutana na wananchi na kufanya kampeni kwa ajili ya TANU na pili aje kupambana na propaganda dhidi ya TANU zilizokuwa zikitawanywa na Yustino Mponda.

Mponda akitumia uhusiano wake na serikali ya kikoloni na nafasi yake kama mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kutoka Newala; na vilevile akitumia ushirikiano wake wa muda mrefu na kanisa ambao bila shaka yoyote lilikuwa serikali ndani ya serikali kule kusini, alikuwa ameanza kampeni yake ya kuipinga TANU. Hili lilikuwa likiathiri msukumo wa uanachama. Mponda alikuwa mmoja wa wajumbe waliotumwa na Gavana Twining kwenda Umoja wa Mataifa Februari, 1955 kwa niaba ya serikali ya kikoloni kwenda kuipinga. Uongozi wa TANU huko Lindi ulitaka Nyerere aende kupambana na Mponda akiwa katika uwanja wake mwenyewe, ndani kabisa ya ngome ya Ukristo wa Kikatoliki katika Tanganyika.

Mkutano mkuu wa mwaka wa TANU ulifanyika katika ukumbi wa Hindu Mandal mjini Dar es Salaam. Siku kabla ya mkutano TANU ilimwalika Gavana Edward Twining kwenye tafrija katika Ukumbi wa Arnatouglo lakini alikataa kistaarabu na akamtuma Chief Secretary, Bruce Hutt, kumwakilisha.

Baada ya mkutano, wakati wajumbe wengine wanaondoka kurudi kwenye majimbo yao, Mpunga na Mnjawale walibakia nyuma kukutana na uongozi wa makao makuu wa Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe, Said Chamwenyewe, Oscar Kambona na wengineo. Mpunga na Mnjawale waliwafahamisha viongozi wa makao makuu kuhusu hali mbaya ya siasa Jimbo la Kusini.

Mbali na kampeni za kuipinga TANU za Mponda, katika ziara yake Lindi Gavana Twining aliwatahadharisha Waafriika wa Tanganyika wasijihusishe na 'wafaanya fujo wanaotaka kuzusha vurugu'. Twining alikuwa akitoa onyo hili akiikusudia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa mwaka uliopita. Hotuba hii ya Gavana iliwatisha wananchi kujiunga na TANU. Mpunga na Mnjawale walisisitiza kuwa kuja kwa Nyerere mjini Lindi kulitakiwa haraka sana kukabiliana na vyote viwili, kwanza ile hotuba ya gavana na pili zile kampeni za kupinga TANU zilizokuwa zikiendeshwa na Liwali Yustino Mponda.

Wakati huo Abeid Amani Karume aliyehudhuria ule mkutano alimwalika Nyerere afanye ziara Zanzibar. Kitu cha kustaajabbisha ni kuwa, Nyerere alionekana kuiafiki zaidi ziara ya Zanzibar kuliko ile safari ya kwenda kusini kuiimarisha TANU. Mpunga alimsisitizia Nyerere umuhimu wa yeye kwenda Lindi ambako kunaweza kuwa ndiyo chanzo cha TANU kupata ufanisi Newala, Songea, Tunduru na Masasi ambako kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya TANU. Kanisa lilikuwa likiwazuia Wakristo kujiunga na TANU. Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenye, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe wote waliunga mkono ule ujumbe wa Lindi juu ya suala hili. Baada ya kufikia makubaliano, Mpunga na Mnjawale walipewa barua ya kuthibitisha safari ya Nyerere. Ziara ya Nyerere ilikuwa ianze muda mfupi kutokea hapo kwa kuwa ilikuwa ndiyo siku za mwisho za kiangazi. Barabara sehemu ya kusini ya Tanganyika zilikuwa hazipitiki wakati wa masika, zikiitenga kabisa kusini toka sehemu zilizobaki za nchi. Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani walifuatana na Nyerere kwenda Jimbo la Kusini kuondoa wasiwasi na woga uliozushwa na Gavana Twining na kibaraka Yustino Mponda.

Nyerere na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita, hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori, alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere apate kumuona.

Baada ya Nyerere kumtia Mpunga machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa. Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere.

Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja, Issa bin Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.

Kanisa Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa miaka na WaislamU wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislamu mjini Lindi haukumwamini Mkristo yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.

Jumapili hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa hii 'maalum' ilidumu katika fikra za wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa miaka mingi kwa kuwa tukio hilo liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku akiwa amesimamiwa na Waislam.

DC mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe.

Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine wamesimama katika ya jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia.

Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.

***

Tangu mwaka 1954 tetesi za chama cha siasa kilichoanzishwa Dar es Salaam kupigania uhuru zilikuwa zimepenya na kufika Mikindani, mji mdogo kusini mwa Lindi. Huko Mikindani kama ilivyokuwa mjini Lindi, harakati za utaifa zilianzia kwa wakazi wa mjini, Wamakonde wengi wao wakiwa Waislam. Kinyume na imani ya watu wengi kuwa Wamakonde ni wapagani, Wamakonde pekee waliokuwa si Waislamu walikuwa wale waliokuja kutoka Msumbiji, koloni la Wareno. Hawa ni Wamakonde waliovuka mto Ruvuma kuingia Tanganyika kutafuta kazi katika mashamba ya mkonge kama manamba. Uislamu ulikuwa umeimarika Kilwa na sehemu nyingine za pwani kwa zaidi ya miaka elfu moja. Wamakonde wasio Waislamu wanaweza kutambulika kwa chale walizochanja katika nyuso zao na ndonya kwa wanawake wao. Wamakonde wa Tanganyika kutoka Lindi, Mikindani na Mtwara katika mwambao wa ukanda wa pwani wa kusini ni kabila la Waislamu wengi. Wamakonde Wakristo wanatoka katika maeneo yanayozunguka Masasi ambayo hadi sasa ni eneo la Wamishonari. Wamishonari wa UMCA waliingia Masasi, nchi inayokaliwa na Wamakua na Wamakonde katika mwaka 1876.

Mikindani haikuwa kama Lindi. Lindi ilikuwa kituo cha biashara na utawala wa kikoloni katika Jimbo la Kusini. Lindi ilikuwa na uwanja wa gofu, sinema na kilabu mahususi kwa Wazungu ambayo hakuna Mwafrika au Mhindi aliyekanyaga hapo bila sababu ya maana. Lindi ilikuwa na barabara za lami na mitaa yake iliwashwa taa usiku kuondoa giza. Kadhalika mji ulikuwa na idadi ya kutosha ya Waafrika waliokuwa katika utumishi wa serikali. Wakati huo Lindi ilikuwa manispaa iliyokuwa ikikua na yenye shughuli nyingi. Ikilinganishwa na Lindi Mikindani ilikuwa kijiji kikubwa cha uvuvi kisichokuwa na mambo ya mjini na wakazi wake bado walitumia taa za kandili. Si watu wengi waliokuwa wakihamia Mikindani kutoka sehemu nyingine kuja kutafuta kazi. Uhamiaji wa watu kutoka sehemu nyingine kuja mjini Mikindani ulikuwa katika kiwango cha chini sana. Watu pekee waliokuja Mikindani walikuwa Wamakonde kutoka Newala na Masasi ndani ya Tanganyika na wale kutoka upande wa pili wa mpaka toka Msumbiji. Hawa walikuja kufanya kazi katika mashamba ya mkonge yaliyokuwa yakimilikiwa na ukoo wa Karimjee.161 Hawa Wamakonde wahamiaji walikuwa wakidharauliwa na wenyeji na kwa ajili hii Wamakonde wakiwa hawana dini walijitenga na wenyeji. Hakukuwa na maingiliano baina ya Wamakonde kutoka koloni la Wareno la Msumbiji na Wamakonde Waislam wa Tanganyika. Wakiwa mbali na nyumbani ambako maisha chiini ya Wareno yalikuwa magumu sana hawa Wamakonde waliangukia chini ya ulezi wa Kanisa.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook