Kwanini nimeamua kuwa mgombea Urais- 2
 

Waheshimiwa Wananchi,

Bahari ya Hindi, visiwa vya Zanzibar na Mafia, delta ya mto Rufiji, mbuga za wanyama za Serengeti, Ngorongoro, Lake Manyara, na Selous, Milima Kilimanjaro na Meru na ukarimu wa wananchi wetu na tamaduni zao, vinaifanya Tanzania kuwa nchi ya pekee kwa mapumziko murua kwa wageni watokao nchi za Ulaya, Marekani na Asia. Gazeti la Financial Times la Uingereza limeelezea kuwa Tanzania "offers one of the world's most complete holiday destination." (Ni moja ya nchi inayotoa mapumziko murua yaliyokamilika.). Hata hivyo hatujatumia urithi wetu wa asili kuinua hali ya maisha ya Watanzania.

Tanzania ina vyanzo vikubwa vya nguvu za umeme wa maji lakini gharama zake za umeme ni kubwa kuliko nchi za jirani na ukatikataji wa umeme ni jambo la kawaida. Hili ni jambo la kushangaza kabisa ikizingatiwa kuwa serikali imekuwa ikipata dola za kimarekani siyo chini ya milioni 10 kwa mwaka kutokana na ushuru wa petroli kuchangia mfuko wa nishati. Nchi yetu ina madini mengi ikiwa ni pamoja na dhahabu, almasi, bati, Chuma., Uraninium, phosphate, makaa ya mawe, vito, nickel, chokaa, jasi, chumvi, mfinyanzi na gesi. Madini haya hayajatumiwa kukuza uchumi wa nchi na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.

Maendeleo ya viwanda ni madogo sana nchini. Pamoja na madeni makubwa tuliyolimbikiza katika uwekezaji wa rasilimali katika viwanda, uzalishaji wa bidhaa za viwanda haukuongezeka kwa kasi iliyotarajiwa. Ajira viwandani ni ndogo sana. Katika nguvu kazi ya Watanzania milioni 17, walioajiriwa viwandani ni 145,000 tu. Hii ni chini ya asilimia moja ya nguvukazi yote. Watanzania laki nane tu ndio wenye ajira rasmi katika sekta zote.

Kuongezeka kwa ajira rasmi ni kigezo muhimu cha uchumi unaokua na kupunguza umaskini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba shughuli nyingine zote za kujiajiri zinategemea matumizi ya vipato vya wale wenye ajira rasmi. Mkulima, seremala, fundi cherehani, kinyozi, muuza duka, n.k., wote wanategemea mzunguko wa fedha ambao chanzo chake ni yule mwenye ajira rasmi. Mathalani, kikijengwa kiwanda mahali kinachoajiri wafanyakazi 1000 ambao kwa wastani kila mmoja wao analipwa shilingi 50,000/- kwa mwezi. Kila mwisho wa mwezi kutakuwa na jumla ya shilingi milioni 50 kwenye mikono ya wafanyakazi hao ambazo ziko tayari kutumiwa. Wako wanaohitaji vitanda watakwenda kwa fundi seremala. Wako watakaohitaji suruali au magauni watakwenda kwa fundi cherehani. Wako watakaohitaji mchele, maharage, unga, mchicha, n.k., watakwenda sokoni. Fundi seremala naye ili aweze kuchonga vitanda vya watu atahitaji kununua na kuchaniwa mbao. Fundi cherehani atahitaji kununua vitambaa. Mchuuzi wa sokoni atahitaji mkulima amuuzie, nk., alimradi ajira rasmi alfu moja zinaweza zikatengeneza mlolongo wa ajira tegemezi zinazoweza kuajiri watu wengine hata alfu tano.

Waheshimiwa wananchi, pengine hakuna kitu kinachochangia kuongezeka kwa haraka kwa maendeleo katika nchi kama mtandao mzuri wa mawasiliano. Barabara na reli, usafiri wa majini pale unapohitajika, usafiri wa anga, simu, fax, na hivi sasa Internet. Kuwapo kwa njia za uhakika za usafiri ndani ya nchi kunarahisisha sana usafirishaji wa idadi kubwa ya watu na kiasi kikubwa cha bidhaa toka pande moja ya nchi hadi nyingine. Hili mbali ya kuokoa muda, lina mchango mkubwa katika kushusha gharama za kibiashara na hatimaye bei ya bidhaa. Hali kadhalika linasaidia sana kukuza maingiliano ya watu kwenye jamii na hivyo kufanya watu wa upande mmoja kujifunza kutoka watu wa upande mwingine.

Kwa mujibu wa utafiti wa shirika la mawasiliano la umoja wa mataifa (ITU), mapato ya nchi masikini yanaweza yakaongezeka kwa wastani wa dola za kimarekani 4,000.00 kwa mwaka kwa kila simu moja mpya inayoongezeka ambayo itagharimu wastani wa dola za kimarekani 1,000.00 tu kuiweka. Nchini Tanzania hivi sasa kuna wastani wa laini za simu sita (6) kwa kila watu 1,000. Hali kadhalika kuna wastani wa masanduku ya barua matano (5) kwa kila watu 1000. Huu ni uwiano mbaya sana unaoashiria kuwa wananchi wetu hawatumii tekinolojia kufanya mawasiliano. Watanzania waliowengi wanatumia muda mwingi kutafuta taarifa na kuingia gharama kubwa za usafiri kwa sababu tu ya kukosa mawasiliano mazuri ya simu.

Tanzania kuna tatizo kubwa la mawasiliano. Barabara ziko katika hali mbaya kabisa. Baada ya miaka 40 ya uhuru mtu anayetaka kwenda mikoa ya kanda ya ziwa kwa usafiri wa basi kutokea Dar es salaam, inakuwa ni nafuu kwake kupitia nchi jirani za Kenya na Uganda! Wakati wa masika safari ya kwenda Lindi na Mtwara inaweza ikachukua wiki tatu katika mazingira ya barabara iliyoko hivi sasa badala ya masaa manane. Kielelezo cha ubovu wa barabara zetu si kigeni kabisa kwa wakazi wa miji yetu. Barabara takriban zote alizoziacha mkoloni zikiwa na lami hivi sasa ni vumbi na makorongo matupu. Serikali ya CCM inawajibika kubeba lawama zote. Kila mwaka serikali hii inakusanya kiasi cha wastani wa dola za kimarekani 48 milioni kama ushuru wa barabara unaotozwa kwenye kila lita moja ya petroli na dizeli inayouzwa nchini. Fedha hizi kwa gharama za leo hii zinatosha kujenga umbali wa wastani wa kilometa 320 za barabara imara na ya kisasa. Lazima tujiulize hizi fedha zimekuwa zikifanyia nini iwapo hali ya barabara zetu ndiyo hii tunayoiona.

Waheshimiwa wananchi, Ilani yetu ya Uchaguzi inafafanua kwa undani zaidi azma yetu na mikakati tutakayoitumia kujenga uchumi imara wenye manufaa kwa wote. Hapa nitazungumzia mambo machache ambayo nikiwa Rais nitayasimamia kwa karibu.

1. Kujenga uchumi imara unao ongeza ajira.

Iwapo nitachaguliwa kuwa Rais lengo kuu la sera litakuwa kujenga uchumi unaokua kwa kasi kubwa na kuongeza ajira. Haiwezekani watanzania kuondokana na umaskini bila kukuza uchumi unaoongeza ajira. Katika suala la kukuza uchumi hakuna miujiza. Uchumi unakua kwa kuongeza elimu, ujuzi na utaalamu wa wafanyakazi, ongezeko la raslimali na vitendea kazi, na kuongezeka kwa ufanisi na tija katika uzalishaji na utoaji huduma. Dira ya maendeleo na sera za kutekeleza dira hiyo ni jambo la msingi katika kuleta maendeleo ya muda mrefu. Sera za ukiritimba wa dola katika mambo ya uchumi na kuwabana wananchi, kuwanyang'anya motisha wa kujiendeleza, na kufumbia macho rushwa ya hali ya juu inayoendelea nchini zimeporomosha uchumi wetu. Kwa muda mrefu uchumi wetu umetumikia siasa, badala ya siasa kuweka mazingira mazuri ya kukuza uchumi. Dira yetu ya maendeleo itakuwa ni kujenga uchumi wa soko wenye ushindani halali na unaowashirikisha na kuleta maendeleo kwa wananchi wote. Majukumu makubwa ya dola chini yetu yatakuwa ni:-

Kuasisi utawala unaolinda kikamilifu haki za wananchi, unaozingatia kanuni na kufuata sheria.

Kujenga mazingira yatakayotuhakikishia ongezeko kubwa la ajira mwaka hadi mwaka.

Kuweka mazingira yanayolinda ushindani halali wa biashara, kuepuka mfumuko mkubwa wa bei, na kulinda ushindani wa bidhaa zetu katika soko la dunia.

Kuboresha huduma za msingi za jamii na hasa elimu na afya.

Kujenga au kusimamia ujenzi wa miundombinu mizuri kama vile barabara, reli, nguvu za umeme, simu na maji.

Kulinda na kuhifadhi mazingira.

2. Kilimo.

Ili Tanzania ijinasue katika dimbwi la umaskini ni lazima pawepo na mapinduzi ya Kilimo. Kuendeleza kilimo tunahitaji:-

Kuongeza motisha kwa wakulima wapate bei nzuri ya mazao yao. Hatua za makusudi zahitajika kuboresha huduma za kilimo na kuweka usimamizi wa kuwalinda wakulima wasinyonywe na wafanyabiashara wanaoshirikiana kupunguza ushindani katika soko huria na kwa lengo la kuangusha bei za mazao.

Mfumo wa kodi na ushuru wa mazao ya kilimo kurahisishwa na viwango vya kodi ya mazao kupunguzwa ili kuongeza motisha kwa wakulima kuwekeza katika sekta ya kilimo. Vizuizi vya biashara ya mazao yote ndani ya nchi vitaondolewa.

Mapinduzi ya kilimo kuasisiwa kwa kusisitiza matumizi ya zana na pembejeo bora. Serikali itashirikiana na benki na taasisi nyingine za fedha kuwasaidia wakulima kujiingiza kwenye kilimo cha kibiashara kinachotumia zana na pembejeo za kisasa.

Serikali kushirikiana kwa karibu na taasisi za kimataifa kuboresha utafiti wa kilimo na mafunzo na ushauri kwa wakulima. Serikali itatenga alau asilimia 5 ya bajeti yake kuimarisha utafiti wa kilimo, ushauri na huduma nyingine kwa wakulima.

Kila wilaya kuhamasishwa kutayarisha na kuutekeleza mpango wa muda mrefu wa kujenga na kukarabati barabara ziendazo vijijini. Asilimia 50 ya fedha za ushuru wa barabara unaotozwa mafuta ya magari utatumiwa kuimarisha barabara za vijijini.

3. Barabara.

Mawasiliano mabovu ya barabara ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya uchumi na hivyo ni kizingiti katika vita yetu dhidi ya umaskini. Ni wazi kabisa kuwa utaratibu wa makusudi unapaswa kuwekwa na kusimamiwa kwa karibu kuhusiana na ujenzi na ukarabati wa barabara zetu kuu na za vijijini. Rushwa imekithiri katika Wizara ya Ujenzi na inachangia kwa kiasi kikubwa ukarabati hafifu wa barabara zetu.

Waheshimiwa wananchi, kuweka utaratibu ulio wazi wa kutoa zabuni na kuwajibika kwa watendaji wa serikali na makampuni ya ujenzi kutasaidia sana kupunguza rushwa na kuimarisha matengenezo ya barabara.

Iwapo nitachaguliwa kuwa Rais, serikali itatayarisha mpango kabambe wa miaka kumi wa kujenga barabara muhimu za kitaifa zitakazounganisha mikoa yote ya nchi yetu. Katika mpango huu tutaazimia kujenga kilomita 300 za barabara safi kila mwaka. Ni wazi kabisa kuwa ili mali asili na nguvu kazi iliyoko mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa ya kusini itumike kikamilifu kuinua maisha ya wananchi wa mikoa hii na Watanzania kwa ujumla, barabara kuu ya Mwanza mpaka Dar es Salaam na Barabara ya kusini inayounganisha Mikoa ya Lindi na Mtwara na Dar es Salaam ni lazima zijengwe haraka iwezekanavyo.

5. Elimu

Kukua kwa uchumi wa kisasa wenye uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi kunategemea sana wafanyakazi wenye ujuzi na maarifa. Kwa hakika utafiti unaonyesha kuwa kukua kwa uchumi wa taifa lolote kunashabihiana kwa karibu na kiwango cha kuwekeza katika sekta ya elimu. Hivi sasa Dunia inashuhudia mapinduzi ya teknologia ya mawasiliano ya habari (Communication and Information technology) ambayo yanaleta mageuzi makubwa ya uchumi na biashara ya kimataifa. Uchumi wa kisasa unatumia kompyuta na mtandao (internet). Kwa hakika mtandao umeondokea kuwa ni kisima kilichojaa kila aina ya habari, taarifa, na data ambazo kila mmoja wetu anaweza kujichotea kwa matumizi yake kwa gharama nafuu kabisa. Ili Tanzania ishiriki kikamilifu na ifaidike na uchumi wa ulimwengu inatulazimu kuweka mkakati wa kuboresha na kupanua elimu toka elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu. Pamoja na mambo mengine, iwapo nitachaguliwa kuwa Rais serikali itachukua hatua za makusudi ikishirikiana na taasisi za kimataifa kusambaza matumizi ya kompyuta na mtandao (internet) katika mashule yetu.

Elimu bora ya msingi ni haki ya kila mtoto. Nikichaguliwa kuwa Rais, itakuwa marufuku kumfukuza mwanafunzi kwa kisingizio cha kukosa ada. Serikali itachukua hatua zote zinazowezekana ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wazazi, mashirika ya dini, taasisi zisizokuwa za kiserikali na wahisani wa nje na ndani kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Tanzania anapata fursa ya elimu ya msingi iliyo bora.

Aidha, Serikali itashiriki kwa nguvu zote katika kuongeza na kuboresha shule za sekondari, vyuo vya kawaida na vyuo vikuu. Mafanikio ya hatua hii yatategemea juhudi za serikali katika kuongeza ufanisi na kubana matumizi yasiyo ya lazima ili sehemu kubwa ya matumizi yalenge katika kutoa elimu. Nikiwa Rais nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa ufanisi unaongezeka na kuondoa kabisa matumizi yasiyo ya lazima katika serikali. 
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook