WATU kadhaa wamejeruhiwa baada ya kupigwa virungu na polisi huko Tukuyu.
Polisi hao walivamia mkutano uliokuwa ukihutubiwa na Prof. Lipumba mapema wiki hii katika uwanja wa michezo mjini Tukuyu.
Polisi hao wakiongozwa na OCD ambaye jina lake halikufahamika mara moja waliingilia mkutano huo wakati Prof. Lipumba akiendelea kunadi sera zake na kuanza kuwatawanya wananchi.
OCD huyo aliamuru askari kuzima genereta na kuanza kutawanya watu kwa virungu hali iliyosababisha wananchi kukimbia ovyo na kuumizana.
Baada ya watu kutawanyika, Prof. Lipumba alimhoji OCD huyo sababu ya kuingilia mkutano wake halali na kuwapiga wananchi ambao hawana hatia.
OCD alidai kuwa alifanya hivyo baada ya kuona kuwa imefika saa 12 na mkutano haujaisha.
Hata hivyo, Prof. Lipumba alisema kuwa yeye hafuati sheria za polisi bali za Tume ya Uchaguzi ya Taifa ambayo inabainisha kwamba mwisho wa mikutano ya kampeni ni saa moja kamili na wala sio saa kumi na mbili kama OCD alivyodai.
Alisema, kazi ya polisi ni kulinda na kuangalia usalama na wala si kupanga muda wa mikutano ya kampeni wala ratiba yake.
Prof. Lipumba alibainisha kwamba Tume ya Uchaguzi ilitoa maelezo kwamba mwisho wa kuhutubia wananchi kwa vipaza sauti ni saa moja jioni.
Hata hivyo, OCD huyo alisema, anachojua ni kuwa mikutano ya kampeni mwisho wake ni saa kumi na mbili jioni na kwamba hana taarifa zaidi ya hiyo.
Prof. Lipumba, awali alihutubia mkutano wa kampeni wilayani Kyela ambapo aliwataka wananchi wajikomboe na umaskini kwa kumchagua.
Kabla ya mkutano wa Prof. Lipumba, mgombea Urais
wa chama cha TLP Bw. Augustine Mrema alishambuliwa na polisi na kuondolewa
eneo la mkutano ambapo wananchi kadhaa walijeruhiwa. Bw. Mrema alishambuliwa
mara tu baada ya kuanza kuhutubia wananchi wa Tarafa ya Ilembo wilayani
Kyela.
Wakiongea na gazeti hili wamesema, Dkt. Omar Ali Juma amewasifia sana kuhusu uadilifu wa Rais Mkapa, ila wanachotaka kujua Waislamu nao wamo?
"Wasiwasi ni kuwa sisi Waislamu hatumo. Maana mpaka siku anatusifia uadilifu wa Mhe. Rais Mkapa, bado waliowaua Waislamu wenzetu kwa risasi Mwembechai walikuwa bado hawajakamatwa", alisema Bw. Juma aliyedai katoka Singida wiki hii.
Amesema, anatatizika ni vipi mahali penye uadilifu watu wauliwe kwa risasi na serikali ikatae kuwafikisha mahakamani walioua.
"Serikali inayoshinikizwa na Paroko iwavamie Waislamu kwenye nyumba zao za ibada, iwapige hadi polisi kuua na hakuna kesi, pana uadilifu hapo?" alihoji Bw. Juma.
Naye Jamal akiongea na mwandishi wa habari hizi amesema, anahisi japo katiba na sheria za nchi zinawahusu watu wote, lakini anaona hiyo ni kwa nadharia tu.
"Katiba na sheria za nchi ziko wazi hatua gani zichukuliwe watu wanapouliwa kinyama kama polisi walivyofanya pale Mwembechai. Lakini kwa vile waliouliwa ni Waislamu serikali imefumba macho", alisema na kuongeza, "inavyoonekana Waislamu hatumo".
Bwana Rajab yeye alisema, Waislamu wataendelea kuhoji juu ya mauaji ya Mwembechai mpaka hapo serikali itakapotamka wazi kwamba kikatiba wao hawana haki kama wananchi wengine.
Bwana Rajab na wenzake walifika kwenye ofisi za gazeti hili kuelezea maoni yao juu ya sifa za uadilifu Makamu wa Rais alizomsifu nazo Rais Mkapa huko Manyoni hivi karibuni.
Wamesema, utawala wa Mkapa umeshuhudia tukio lisilo na mfano wake katika historia ya nchi hii.
Katika tukio hilo, Paroko Camillus Lwambano wa Kanisa Katoliki aliishinikiza serikali ikatuma polisi waliowapiga Waislamu, kuvunja Msikiti na kuwapiga wanawake waliokuwa ndani.
Wanawake hao baada ya kudhalilishwa waliwekwa ndani na kuzuiwa dhamana kwa miezi kadhaa.
Watoto kadhaa pia walikamatwa na kuwekwa rumande wakichanganywa na watu wazima.
Ni katika tukio hilo ambapo watendaji wa serikali waliwaamuru polisi wawatwange risasi Waislamu waliokuwa eneo la Mwembechai.
"Piga shaba, piga yule, bado" ni sauti za Makamanda zilizonaswa na mikanda ya video wakiamrisha Waislamu watwangwe risasi.
Kamati ya Kupigania Haki za Waislamu ilipata kusema kuwa ilimpelekea nakala ya mkanda huo wa video Rais Mkapa kama ushahidi wa yaliyotukia.
Hata hivyo, kauli ya Rais Mkapa mpaka sasa ni
kuwa mauaji hayo hayahitaji kuundiwa Tume.
--
![]()
|
|