Jasusi angamizi lipo Dar
Habari za kihisani toka kwa watu wema ambao hawakujitaja majina yao zimetoa fununu zinazodai kuwepo kwa jasusi lililoandaliwa kwa utaalamu maalum wa kuvuruga shughuli za Uislamu na Waislamu kwa kutumia njia na mbinu mbali mbali.

Njia na mbinu hizo zimedaiwa kuwa ni pamoja na kupandikiza vurugu na kuweka viongozi vibaraka katika taasisi za kiislamu ikiwemo misikiti, kufitinisha na kufarakanisha makundi mbali mbali ya Waislamu na kuwazushia kesi.

Mbinu nyingine zimeelezwa kuwa ni kujenga uhasama baina ya Waislamu na wakristo ili waonekane Waislamu wana mgogoro na Wakristo badala ya serikali inayowadhulumu na zaidi ya yote kuangamiza maisha ya baadhi ya Waislamu watakaoonekana kuwa ni "wagumu" kusambaratishwa kwa rushwa au kwa mbinu nyingine.

Habari hizo zilifichuliwa na baadhi ya waumini waliomo katika vikundi kadhaa vinavyoshughulika na maendeleo ya Waislamu na dini yao, ambao hawakupenda kutaja majina yao kwa sababu za kiusalama.

Waumini hao wamedai kuwa wao wamezipata habari hizo toka kwa watu waliodai kuwa ni "wasamaria" wema ambao wamo "jikoni" kunakopikwa njama hizo chini ya mtaalamu huyo aliyepania kufanikisha tenda yake ya kupambana na Waislamu.

Wameelezea zaidi kwamba wao walizipata habari hizo wakati wakifuatilia tukio la kupigwa mapanga muumini mwenzao wiki kadhaa zilizopita huko Mwanza.

Ustadh Ilunga ambae ni mhadhiri maarufu nchini na kiongozi wa jumuiya ya Kiislamu mjini Mwanza, alivamiwa usiku nyumbani kwake na kundi la watu ambao walimshambulia kwa mapanga.

Ustaadh huyo alijeruhiwa vibaya na kulazwa Hospitali kuu ya Bugando, Mwanza.

Ustaadhi Ilunga alieleza kwamba aliwasikia waliomshambulia wakijigamba kuwa "amezidi kidomo domo".

Habari zilizofikishwa na watu hao wema, zinashuku tukio hilo la ustaadh Ilunga kupigwa mapanga na watu wasiojulikana kuwa huenda zilipangwa kwa maelekezo ya mtaalamu huyo aliyechukua tenda ya "kuwashughulikia" Waislamu na dini yao.

Inadaiwa vile vile kwamba hatua za chama tawala na dola kupuuza madai ya Waislamu kuhusu mauaji ya Mwembechai na badala yake kuonekana kupongeza mauaji yale, inatokana na jeuri na kibri ya jasusi hilo na kamati yake kuwa wanazo mbinu za kutosha kuzuia fukuto la wanaodai haki za Waislamu.

Kwa mujibu wa maelezo ya watu hao kwa waumini waliowadokeza habari hizo, zipo dalili nyingi zilizotolewa ambazo zinaonesha kuwa kuandamwa kwa Sheikh Mbukuzi na kesi nyingi pamoja na uzushi aliozushiwa hivi karibuni ni katika kazi zinazofanywa na shushu hilo na kamati yake.

Inaelezwa vile vile kwamba shushu hilo na kamati yake hiyo wanafungu maalum la fedha za kuhonga na kuwanunua Waislamu wanaoweza kutumika katika malengo ya kamati hiyo.

Imefahamishwa pia kuwa mbali ya kujiandaa kwa fungu la kuhonga baadhi ya vyombo vya habari ili viendeshe propaganda dhidi ya Waislamu, kamati hiyo angamizi inadaiwa kuwa tayari imedhibiti baadhi ya wanahabari na vyombo vyao kwa ajili ya kuendesha propaganda.

Kwa mujibu wa maelezo ya waumini hao, wasamaria hao waliwafahamisha kwamba madhumuni makubwa ya njama hizo ni kuandaa mazingira ya kuimarisha mfumo Kristo chini ya uongozi wa wale watakaowahakikishia kuwa kanisa katoliki linaendelea kupewa fursa kubwa nchini kama lilivyoahidiwa na Mwalimu Nyerere.

Kwa mujibu wa kitabu kilichoandikwa na mjerumani Van Bergen 1984, mwalimu Nyerere aliwaahidi maaskofu wa kanisa katoliki katika miaka ya 1970, kwamba aliamua kulipa kanisa katoliki nchini fursa kubwa kuliko taasisi zote.

Imeelezwa na waumini hao kuwa watu hao wema waliwafahamisha kwamba kazi ya kupanga njama hizo inafanywa kitaalamu chini ya kamati maalum zilizopo katika ngazi tofauti, kuanzia juu hadi chini, pasipo kufafanua zaidi juu ya mfumo wa ngazi hizo.

Wameeleza kuwa walijulishwa na wasamaria hao kuwa jasusi hilo katika mfumo huo lipo katika kitengo cha kuwashughulikia Waislamu "wasiofaa" kuongoza taasisi na jumuiya za kiislamu kama vile vyuo, shule, misikiti na kuendesha vikundi kama vile vya kina mama na vijana kwa kuwa vinaonekana kwenda kinyume na mfumo kristo.

Majukumu mengine ya shushu huyo na kamati yake ni kuhakikisha kuwa mihadhara na vikundi vya mihadhara vinakufa, harakati za kinamama zinavurugwa na mipango yoyote ya kuwaendeleza vijana wa Kiislamu nayo pia inavurugwa au kufifishwa hadi kufutika.

Mikakati iliyoandaliwa na kuanza kutekelezwa ni pamoja na kuingilia na kuvuruga uongozi wa misikiti, jumuiya za kinamama, vijana na wanafunzi.

Imo pia ya kuzuia na kuvuruga usajili wa vyama vya hiari vinavyoongozwa na Waislamu na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Waislamu.

Mbinu na mikakati imepangwa pia kuzuia Waislamu kushiriki katika uongozi wa siasa na vikundi vyovyote vyenye sauti ya jamii.

Waumini hao wameeleza kuwa wamefahamishwa na wasamaria hao toka jikoni kuwa kazi ya "shushu angamizi" na kamati yake ilihusika vile vile hivi karibuni na kuandaa mbinu za kuwaondoa wagombea wengi wa kiislamu waliojitokeza katika nafasi za ubunge CCM pasipo kujali uwezo wao au ushindi wa kura za maoni walizopigiwa na wananchi.

Walidai kuelezwa kuwa hatua hiyo ilichukuliwa ili kupunguza zaidi idadi ya Waislamu bungeni ili isije ikaathiri miswaada ya fursa bora iliyoahidiwa tangu awamu ya kwanza.

Imeelezwa kwamba waliambiwa kuwa Waislamu wachache wanaotakiwa kuwemo katika siasa na katika baadhi ya taasisi na idara za serikali ni wale ambao wataonekana "wanafaa" kukubali mambo kama yalivyo pasipo kuhoji dhulma yoyote wanayofanyiwa Waislamu nchini, ikiwemo kuuliwa kwa wenzao Mwembechai kufufatia shinikizo la paroko wa kanisa katoliki.

Aidha imeelezwa pia kuwa kile kikundi cha umoja wa maaskofu na Bakwata kilichoanzishwa hivi karibuni kwa baraka ya serikali ya CCM kinakubalika kama ambavyo Bakwata inavyokubalika mbele ya kamati ya 'shushu angamizi' dhidi ya Waislamu na wapenda haki na maendeleo.

Wanaharakati waliotoa taarifa hizo wamedai kuendelea na uchunguzi zaidi kuhusu shushu hilo na kamati yake na kwamba itakapo kamilika watatangaza baadhi ya habari zake na hatua za kuchukuliwa katika mkutano utakaoitishwa hapo baadaye.

Hata hivyo kwa mujibu wa habari za awali wanaharakati hao wamedai wamedokezwa shushu hilo limepata mafunzo yake Uingereza na Marekani, hakuna uhakika wa dini yake lakini inadaiwa ni Islam.


CCM Songea lawamani

CCM Songea imelaumiwa kwa kuzuia mawaidha na kuchochea vurugu Misikitini.

Habari kutoka Songea zimeeleza kuwa, baadhi ya Maimamu walipewa amri wasiruhusu kutolewa mawaidha katika Misikiti yao mpaka uchaguzi umalizike.

Amri hiyo imedaiwa kutolewa kufuatia mawaidha yaliyokuwa yakitolewa katika baadhi ya Misikiti ambapo zimekuwa zikitajwa dhulma wanazofanyiwa Waislamu na serikali.

Kutajwa kwa dhulma hizo kumeelezwa kuwa kuliwatia hofu wana CCM kwamba kungeikosesha CCM kura Oktoba.

Kufuatia hali hiyo, imeelezwa, kupitia kwa baadhi ya Maimamu, amri ilitolewa mawaidha yazuiwe hadi baada ya uchaguzi.

Imeelezwa kuwa amri hiyo ya CCM ambayo hata hivyo haikuja rasmi, ilikataliwa na waumini.

Imedaiwa kuwa, wana CCM waliopo Msikitini hapo walitumika kuita polisi kwa kisingizio kwamba kuna fujo.

Waumini walipambana na polisi hao kabla ya wenzao 43 kukamatwa na kuwekwa ndani.

Waumini kutoka mjini Songea wameeleza kuwa kuficha aibu, na dhulma hii ya CCM kutaka hata kudhibiti mawaidha Misikitini walitumia baadhi ya vyombo vya habari kueneza propaganda kuwa ilikuwa ni mapambano ya watu wa CUF na CCM Msikitini.

"Vurugu zimeletwa na wazee wa CCM na polisi kama kawaida yao kuwahujumu Waislamu. Kwani hata walipoua Mwembechai kulikuwa na CUF pale?" amehoji muumini mmoja.

Waumini 43 waliowekwa rumande wamekuwa wakiendelea na ibada zao ambapo huamka usiku na kupiga Kiamul-lail hadi alfajir.

Waumini hao awali walipofikishwa gerezani waligoma kuchanganyika na watuhumiwa/wafungwa wengine.

Gereza lililazimika kuwahamisha baadhi ya wafungwa ili kutoa nafasi ambapo waumini hao wangekaa pamoja.

Masiku kadhaa kabla ya tukio hili, baadhi ya waumini waliitwa kwa Mkuu wa Wilaya kuhojiwa. Hiyo ilikuwa baada ya onyesho la kanda ya mauaji ya Mwembechai.

Hata hivyo, mahojiano hayo yalikwama baada ya waumini kutaka wapewe maelezo iwapo ni serikali yenyewe iliwaita ama ilifanya hivyo kwa shinikizo la Kanisa.

Wakati huo huo, waumini kupitia Kamati zao mbalimbali wamekuwa wakiweka mikakati kuhakikisha walioko gerezani wanapata huduma pamoja na familia zao.

Msemaji mmoja wa Kamati hizo amesema ujumbe umekuwa ukisambazwa ili waumini wote waibaini dhulma inayofanywa dhidi ya Waislamu na hatua za kuchukua kuiepuka shari hiyo.


CCM wawapiga mawe CUF

Kundi la wakereketwa wa CCM Jumamosi walilivamia gari lililowabeba wanaCUF, kutoa matusi na kulivurumishia mawe.

Waliokumbwa na mkasa huo ni wanachama wa CUF, Kata ya Mzimuni Magomeni Mapipa.

Kufuatia tukio hilo wana CUF walisimamisha gari ambapo kundi la warusha mawe hao lilitimka.

Binti mmoja ambaye jina lake halikupatikana alinaswa baada ya kushindwa kutimua mbio alipohojiwa alidai kushawishiwa na wana CCM wenzake.

Habari kutoka eneo la tukio zimedai kuwa baadae binti huyo alishawishiwa na kikundi hicho cha wakereketwa kuripoti polisi kuwa alijeruhiwa.

Bwana Ramadhani Uledi miongoni mwa waliokuwa kwenye eneo la tukio alikamatwa na kuwekwa ndani hadi alipotolewa jana.

Watu walioshuhudia tukio hilo walielezea kusitishwa kwao na kitendo hicho cha wanaCCM kupiga gari mawe na kueneza chuki za kisiasa hali ambayo hata baadhi ya wenzao waliilaani.

Mbali na hilo wanachama na viongozi wa CUF tawi la Saratoga wamekilalamikia kitendo cha polisi kukataa dhamana ya Uledi licha ya kwamba mtu aliyeripoti tukio la kupigwa na kujeruhiwa hakuonekana kuumia.

Mwandishi wa gazeti hili alipozungumza na Uledi mara baada ya kuachiwa na polisi jana baada ya wanachama wenzake kuhaha kumdhamini alisema kuwa yeye kama mtu mwenye kuelewa siasa analisamehe tukio hilo ili kuepusha uhasama katika kata yake kati ya CUF na CCM.

Ramadhani Uledi alililaumu jeshi la polisi kwa hatua yake ya kumkamata bila kupata uhakika wa tukio zima.

Wakati huo huo, Mgombea ubunge wa CHADEMA jimbo la Moshi mjini Bwana Philemon Ndesamburo ameshutumu vikali kampeni za CCM kumnadi mgombea wake makanisani.

Bwana Ndesamburo amesema huo ni udini wa dhahiri unaofanywa na chama tawala katika medani ya siasa.

Mgombea wa CCM katika jimbo hilo ni bibi Elizaberth Mara Minde.

Katika mkutano wake wa jumapili huko Pasua, Bwana Ndesamburo alisema kwamba Viongozi wa serikali ya CCM wameshindwa kufanya kazi za wananchi badala yake wanaisifu na kukitetea chama chao.

Amesema madiwani wameshindwa kutetea haki za Wananchi za kurudisha 40% ya kodi zao katika kata.

Alisema hata Wenyeviti wa Serikali za mitaa wanatakiwa wapewe 3% ya kodi lakini hawapewi kwa sababu wanaogopa kudai haki hizo kwa kile walichokiita kukilinda chama.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook