Mtakapokataa fedheha, Waislamu watawapokea
TUNAO Masheikh wengi waliosoma vizuri dini yao. Masheikh wanaofaa kuwa viongozi kwa vile wana elimu ya kutosha.
Hata hivyo wamekosa ujasiri wa kukataa fedheha. Wanaona fahari kwao ni kujitenga na waumini wakakamatana na BAKWATA.
Kwa kuwa mbali na waumini wamefikia hata kutokujua au pengine kujitia upofu, juu ya matatizo na matarajio ya Waislamu nchini.
Wanajua uzuri matatizo ya umaskini. Na wanaijua vyema Hadith ya Mtume juu ya maskini aliyepewa shoka kama mtaji akachanje kuni.
Lakini pengine kwa udhalili walioukubali kwamba wao si sawa na Maaskofu, hawawaelezi Waislamu nani anashoka lao leo na hataki kuwapa.
Muislamu akifungua mgahawa au duka la kuuza vikoi na kanzu Bwana kodi (TRA) yuko mlangoni anataka kodi.
Lakini Muislamu huyo huyo akipanga foleni ya kupewa shoka, ananyimwa.
Shoka la ajira atanyimwa na hata akipewa atapewa butu lisilopandisha cheo.
Foleni ya kuwapa watoto wa Kitanzania mashoka kwenda kusoma vyuoni ndani na nje, wa Waislamu watafanyiwa hiana.
Vijana wangapi wamepewa mikopo ya vioski toka taasisi zinazotambuliwa na serikali mpaka zile za nchi na nje. Je, ni Waislamu wangapi wamepewa mashoka hayo? Au wao hawajui namna ya kuyatumia!
Vijana wangapi wanatembea na nguo mkononi, wakiungua jua kutwa nzima kutafuta rizki? Waislamu wangapi katika hao!
Vijana wangapi wameamua kujitosa katika kazi ngumu ya kuchambua mawe kwenye maporomoko hatari ya udongo au mito ili kujitafutia riziki. Waislamu wangapi kati ya hao?
Angalia wale akinamama wanaonufaika na mfuko wa Fursa Sawa kwa wote, Wizara ya Mama Nagu na NGOs mbalimbali, wamo Waislamu wangapi?
Waangalie wale wanaopika vyakula huku wakitimuliwa na mgambo na askari wa jiji, ni wa dini gani wale.
Tatizo la wote hawa si nadharia na mtizamo wa umaskini. Tatizo ni mfumo unaowanyima shoka.
Mfumo unaokudhalilisheni hata nyinyi Masheikh mjione hamna haki sawa na akina Pengo.
Wenzenu wakipewa fursa TVT na Redio Tanzania, watazungumzia siasa, uchumi, uchaguzi wa Oktoba na hata kutoa maelekezo kwa waumini wao kwamba wawapigie kura wacha Mungu wao.
Nyinyi hamthubutu. Mtaongelea udhu na ndoa. Na hata hiyo ndoa yenyewe hamtathubutu kuiambia serikali kwamba ni dhalimu kwa kuwataka Waislamu waoane Kiislamu wakaachane kikafiri.
Mnajua kuwa BAKWATA haijali maslahi ya Waislamu na sasa BAKWATA wameunda jumuiya lao na Wakristo.
Sasa maadhali mmekosa ujasiri wa kuja kwa Waislamu basi mnapokuja Starlight na "Uwawaru' wenu, mjue Waislamu hawatokuvumilieni. Watakuelezeni ukweli na nyie muwastahamilie.
Waislamu hawana ugomvi na nyinyi na wakati wote watakuenzini mtakapotoka huko. Wanachouliza kila siku ni hiki. Hivi mtakosa nini mkitoka huko? Hawaoni zaidi ya kuwa mtaepuka fedheha.
Zipo taasisi za kimataifa zinazofanya kazi nzuri. Hujenga mashule na kutoa misaada mbalimbali. Taasisi hizo zinajua kuwa zimekabwa na mtandao wa kimataifa. Zinajua kuwa kwa mfano haziwezi kuleta matrekta wakawagawia Waislamu, wakawajengea Waislamu wa Mkuranga kiwanda cha kusindika matunda au kufungua benki ya Kiislamu ambayo itatoa mikopo nafuu isiyo na riba.
Sio kwamba hawana uwezo. Lakini hawatoruhusiwa kama yanavyoruhusiwa mashirika ya Kikristo toka Ulaya.
Hawa tunajua jinsi walivyokabwa kwani hata wakati mwingine tende zao hukwamishwa pale Bandarini zikisingiziwa kuwa ni majambia!
Tunawakumbusha kuwa wawe macho wafanye shughuli zao hizo ambazo wameruhusiwa na kwa bahati wamezifanya vizuri.
BAKWATA wao wenyewe au kupitia Umoja wao waliouunda na Maaskofu, hawawezi kuwaita Waislamu. Wasikutumieni, wakawachonganisha na Waislamu.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |