Kilemile na wenziwe wasambaratishwa

Waislamu Jijini juzi walisambaratisha semina iliyoandaliwa na Masheikh maarufu Jijini wakishirikiana na Bakwata.

Semina hiyo iliyokuwa ikijadili "Mtazamo wa Uislamu juu ya umasikini" ilifanyika katika ukumbi wa STARLIGHT Jijini ilidhaminiwa na shirika moja la kiisamu la kimataifa.

Hamkani iliyosambaratisha semina hiyo ilifumka baada ya mwasilisha mada Sheikh Sulaiman Kilemile kudai kuwa umasikini walionao Waislamu umetokana na wao kutokuwa kuwa na Elimu, uvivu na kuchagua kazi.

Sheikh Kilemile alidai kuwa Waislamu hawana sababu ya kumtupia lawama mwingine bali wajilaumu wao wenyewe kutokana umasikini unaowakabili.

Kufuatia kauli hiyo Washiriki wa semina hiyo waliamka kwa hamasa na kuanza kutoa maneno ya kumshutumu Sheikh huyo wakidai kuwa anatumiwa na serikali.

"Nyamaza wewe, huna la kutuambia, umetumwa wewe, unapoteza muda, tunataka kuchangia, ni baadhi ya kauli zilizotolewa na washiriki hao wakimtaka Sheikh huyo amalize mada yake.

Baada ya kumaliza Sheikh Kilemile, alifuatia Sheikh Doga ambaye nae kama ilivyokuwa kwa Sheikh Kilemile alilazimika kusitisha mada yake baada ya wasikilizaji kuanza kumzomea alipodai kuwa Waislamu wanatakiwa kudumisha amani na utulivu nchini.

Kufuatia mtafaruku huo, mwendesha semina hiyo, Sheikh Mbwana Urari alilazimika kutoa nafasi ya watu kuchangia yale yaliyozungumzwa na watoa mada.

Mchangiaji wa kwanza alikuwa Ustaadh Hashim ambaye aliwataka watoa mada waliangalie tatizo walilotaka kujadili kwa kuujua vyema mzizi wake.

Alisema tatizo la umasikini wa Waislamu na wananchi kwa ujumla wa Tanzania ni mfumo wa ukandamizaji.

Mchangiaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Abubakar aliwalaumu masheikh hao kwa kushindwa kumdhibiti Sheikh Mkuu ambaye alidai anatumiwa kuwavuruga Waislamu.

"Kama mnataka kuondoa Umasikini mwambieni Mufti wenu aache kutumiwa na CCM, alisema kwa jazba kijana huyo huku akitoka nje ya ukumbi huo.

Mwanadada aliyevaa hijabu na niqab na mawani juu ambaye hakufahamika jina aliwashutumu masheikh hao kwa kuwasonta vidole kuwa wanatumiwa na serikali na wamejisalitisha kwa Waislamu.

"We Kilemile wewe, Elimu gani unayohimiza wakati shule yako inatoa maziro kila mwaka, nyie Bakwata umasikini gani mtakaoondoa wakati shule zenu zinakuwa za mwisho, wewe Doga umasikini gani utakaoondoa wakati umepewa vipindi Radio unaeleza mambo ya nikah na kuoga janaba", alisema kwa ukali dada huyo.

Masheikh hao walioonekana kupigwa butwaa walijikuta wakiachwa ukumbini peke yao baada ya mchangiaji mmoja kuwataka wanasemina wote waondoke ukumbini hapo.

"Waislamu wote mlio humu ndani tokeni nje waachieni semina masheikh hawa wa CCM", kauli hiyo ilitolewa na vijana wawili huku wakitangulia kuelekea mlangoni.

Kufuatia kauli hiyo, washiriki hao waliinuka na kutoka nje wakiwaacha mezani Masheikh walioandaa semina.


Baada ya CUF kutawala uwanja wa kampeni:
CCM sasa waenda kwa wapiga ramli, watabiri

MIKUTANO ya chama cha CUF imeonekana kukitia hofu chama tawala ambacho duru zinafichua kuwa kumekuwa na jitihada za kimya kimya za kujitoma kwa wapiga ramli.

Baadhi ya wagombea wa chama hicho nafasi za udiwani katika mkoa mmoja ulio kanda ya mashariki, wameonekana wakiogeshwa hadharani na waganga kwa kile kilichoelezwa kuwa kuwawezesha kushinda uchaguzi.

Katika mfululuzo wa vitendo hivyo vya ushirikina imeelezwa kuwa kamati maalum ya kuhakikisha ushindi kwa chama tawala inasemekana kumtumia mtabiri mmoja maarufu nchini.

Wakati ushirikina huo ukiendelea, baadhi ya wagombea wa chama hicho wamesitisha kabisa kampeni zao kwa madai ya kutaka kujiandaa zaidi.

Wagombea Ubunge wa chama hicho majimbo ya Kawe, Ubungo na Kinondoni wametajwa ni baadhi ya waliolazimika kusitisha kampeni baada ya mikutano yao kuwa ya gharama sana au kukosa wasikilizaji.

Mgombea wa Kigamboni KK, taarifa zinaeleza kuwa muda mrefu hajajitokeza hadharani kufanya mikutano yake ya hadhara.

Hata hivyo imefahamika kuwa Mzee huyo maarufu nchini amekuwa akifanya mikutano ya ndani ambayo ni wanachama wanaofahamika tu ndio hupata fursa ya kuhudhuria.

Haijafahamika ni kwa nini mgombea huyo ameamua kufanya hivyo wala haijaripotiwa huzungumzwa au kupangwa nini katika mikutano hiyo ambayo wafuasi wa vyama vingine wamekuwa wakiita 'mkole' wakifananisha na mafunzo ya siri ya kizaramo apewayo mwari kabla ya kuolewa.

Wakati hayo yakijiri wagombea wa chama cha CUF wa Urais, Ubunge na Udiwani wameripotiwa kugusa hisia za wananchi wengi sehemu mbali mbali nchini.

Mgombea Urais wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba katikati ya wiki iliyopita aliripotiwa kuhutubia maelfu ya wananchi katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.

Wagombea Ubunge na udiwani wa chama hicho katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza na Bukoba wamekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi ambao wamekuwa wakihudhuria kwa maelfu mikutano ya wagombea hao.

Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani utafanyika tarehe 29 mwezi ujao.

Vyama vya CUF na CCM vinaelezwa kuwa ndivyo vitakavyokuwa na ushindani mkubwa katika kinyang'anyiro hicho.


Kesi ya Mbukuzi yaahirishwa tena

KESI inayomkabili Amiri wa Shura ya Maimamu, Sheikh Juma Mbukuzi iliyokuwa isikilizwe Septemba 13 kwa mara nyingine tena imeahirishwa.

Kesi hiyo inayosikilizwa katika mahakama ya Kisutu haikufahamika mara moja sababu ya kuahirishwa.

Sheikh Mbukuzi ameshitakiwa na serikali kwa kile kilichoitwa uchochezi baada ya kuongea na waandishi wa habari katika Msikiti wa Mkwajuni, Kinondoni jijini mapema Aprili 1999 ambapo Amiri huyo aliitahadharisha serikali juu ya dhulma wanayofanyiwa Waislamu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 4, mwaka huu.

Wakati huo huo wananchi wengi waliokuwa mahakamani hapo wamesikika wakilalamika juu ya utaratibu mzima wa uendeshaji wa shughuli za mahakamani hapo zilizojitokeza siku hiyo.

Taratibu walizozilalamikia ni pamoja na kutofahamu ni wapi na kwa muda gani washitakiwa wataitwa kwa ajili ya kesi zao.

Katika ofisi hiyo ya Hakimu, ambamo ndimo palisikilizwa kesi siku hiyo, hapakuwa na nafasi ya kutosha kuingia wahusika wote wenye kesi ofisi ilijaa mawakili na wahusika wa mahaama jambo lililopelekea usumbufu kwa watuhumiwa na mashahidi.

Watuhumiwa wote iliwalazimu kukaa nje ya ofisi ya Hakimu Mkazi na kusubiri kuitwa mmoja baada ya mwingine ndani ya ofisi hiyo.

Aidha, wananchi hao walipendekeza pawepo na utaratibu wa vipaza sauti mahakamani hapo kwa utaratibu maalum ili kusaidia kufikisha ujumbe kwa wakati maalum na kuelewesha ni wapi kesi yake mtuhumiwa itasikilizwa.

"Mimi nilikuwa kule nasubiri kinachoendelea, lakini katika pitapita zangu nashangaa kuona kesi zinasikilizwa katika ofisi ya Hakimu, ssa sielewi kama nimeshaitwa au bado", alisema kijana mmoja ambaye aligoma kutaja jina lake.


Asimamishwa shule kwa kuandika herufi za Kiarabu

MWANAFUNZI Biwaziri Nondo wa shule ya Sekondari Funguni mjini Pangani amesimamishwa shule kwa kosa la kuandika alfabeti za Kiarabu kwenye ubao wa darasa.

Herufi alizoandika na kumfanya atumikie adhabu ya wiki moja mpaka tarehe 1 mwezi huu ni zile herufi za msingi za alifu, bee... ambazo aliziandika nje ya muda wa masomo.

Mwalimu Mkuu, Bwana Togolai J. Makuno aliyetoa adhabu hiyo amelalamikiwa na wanafunzi wa shule hiyo kuwa amekuwa na kawaida ya kulikejeli vazi la hijabu kila asubuhi mstarini kwa kusema "wanaovaa hijabu wanafunika akili, dini yenu inawadanganya", na mengine mfano wa hayo.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook