Vurumai hizo zilitokea baada ya Prof. Lipumba kumaliza kuhutubia mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani humo ambapo mamia ya wananchi walijiunga na chama hicho.
Ili kupunguza vurumai, polisi iliwabidi waingilie kati na kuwapanga watu kwenye foleni ili kuepusha msongamano uliokuwpo. Wazee na wanawake walilazimika kuchukuliwa na wenzao kadi za uanachama kutokana na kushindwa kuhimili msururu wa foleni.
Kabla ya Prof. Lipumba kuhutubia, wananchi wa wilaya hiyo walisoma risala ambayo ilikuwa imeorodhesha matatizo wanayowapata wakazi wa wilaya hiyo. Waliyataja matatizo hayo kuwa ni ukosefu wa barabara zinazopitika kwa msimu mzima, umeme, upungufu wa vituo vya afya, upungufu wa shule za msingi na sekondari pamoja na maji safi na salama.
Wananchi hao walimueleza Prof. Lipumba kuwa hadi hivi sasa kuna shule moja tu ya sekondari kwa wilaya nzima ambayo ni ya kutwa ambayo haitoshelezi mahitaji yao ya elimu ya sekondari.
Baada ya kupokea risala hiyo Prof. Lipumba alisema, CCM ndio chanzo cha matatizo ya wananchi wa wilaya hiyo. Alisema, kwamba fedha nyingi za serikali hazilengi katika sekta muhimu za jamii.
Prof. Lipumba alisema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha anasimamia vizuri matumizi ya serikali yalenge kwenye sekta muhimu na wakati huo huo kurekebisha mfumo wa ukusanyaji wa kodi ambapo makampuni makubwa hayatapewa misahama mikubwa ya kodi kama ilivyo sasa.
Aidha, aliwahakikishia wakulima wa wilaya hiyo kuwa ataondoa ushuru wa mazao kwa wakulima ili kuongeza kipato chao na kupata bei nzuri kwenye masoko.
Alisema kuwa wanunuzi wa mazao wamekuwa wakitozwa kodi nyingi wanapotaka kuuza mazao yao matokeo yake mkulima anapewa bei ndogo anapouza mazao yake.
Wakati huo huo wagombea udiwani kumi wa CUF wilayani humo waliowekewa pingamizi na Tume ya Uchaguzi ya Taifa kwa madai kwamba hawakutimiza masharti ya kugombea nafasi hizo, wamerejeshwa na kuwa wagombea halali baada ya Tume hiyo kutatua matatizo yaliyodaiwa kujitokeza wakati wa kurudisha fomu.
Kutoka Lindi tumearifiwa kuwa wananchi waliamua kumsubiri njiani Prof. Lipumba katika eneo la Mnazi Mmoja huku wakiwa wamejazana kwenye malori yasiyopongua kumi ambapo wananchi wengine walikuwa wamefurika kwenye uwanja wa Ilulu wakisubiri ujio wa mgombea huyo.
Akiwahutubia wananchi, Prof. Lipumba alisema hali mbaya ya uchumi nchini na ukosefu wa maendeleo kwa wananchi wa mikoa ya kusini imesababishwa na sera mbovu za chama tawala.
Alisema, uongozi wa sasa wa serikali ya CCM hawana uchungu na mtu wa kawaida. Amesema wanatumia vibaya fedha za serikali wakati sekta za huduma za jamii zimekuwa zikitengewa fedha kidogo.
Prof. Lipumba alisema kwamba fedha nyingi za serikali mwaka jana zilitumika kukarabati Ikulu ambapo shilingi bilioni 3.2 zilitengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema kuwa baba wa Taifa alipofariki serikali kwa makusudi ilitumia shilingi milioni mia nane hamsini kwa mazishi, fedha ambazo zingesaidia kuboresha huduma za jamii kama vile afya na ujenzi wa barabara.
Prof. Lipumba alisema iwapo atachaguliwa ataunda serikali ndogo na adilifu ambapo safari za Rais nje ya nchi zitapunguzwa tofauti na ilivyo hivi sasa.
Alisema atahakikisha kodi zinasimamiwa vizuri na viwango vyake vinarekebishwa ili ziweze kulipika. Alisema ataondoa misamaha holela ya kodi ambapo makampuni makubwa nayo yalipe kodi na isiwe inawabana wafanyabiashara ndogondogo tu.
Aidha, Prof. Lipumba alisema kwamba atakapochaguliwa
mradi wa kwanza atakaoutekeleza ni kujenga barabara itakayoiunganisha Dar
es Salam ambayo alisema kuwa barabara hiyo si kwa kuwapendelea wananchi
wa Lindi bali ni kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.
WANANCHI mkoani Mwanza wameanzisha staili ya aina yake kwa kuendesha kampeni ya nyumba kwa nyumba kufuatia mgombea wao wa kiti cha ubunge kupata safari ya ghafla Jijini Dar es Salaam.
Wakiongea na gazeti hili jana, wananchi hao wamedai kuwa kutokuwepo kwa mgombea wao hakujaathiri chochote katika kampeni hizo.
Wamesema azma waliyoichukua ni kuhakikisha majimbo yote mkoani humo yanachukuliwa na chama chao.
"Hivi sasa tunapita nyumba kwa nyumba na watu wengi hasa wasiofika mikutanoni wamehamasika sana, tunasubiri siku ya uchaguzi tumpigie Bwana Mbalamwezi", amedai bwana Daud wa mjini Mwanza.
Mgombea ubunge wa jimbo la Mwanza mjini, Bwana Mbalamwezi hivi sasa yuko Jijini kwa shughuli binafsi.
Kwa mujibu wa maelezo yake kufuatia mazungumzo na gazeti hili ilikuwa asafiri kurudi Mwanza Jumamosi iliyopita, hata hivyo mpaka jana alikuwa bado yuko jijini.
Wakati huo huo, wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa na kati hasa Kondoa wametahadharishwa na pesa bandia zinazotumika kununua shahada za kupigia kura.
Tahadhari hiyo imetolewa na baadhi ya watu waliokumbwa na mkasa huo katika mikoa hiyo.
Imedaiwa kuwa awali shahada moja ilikuwa ikinunuliwa kwa beiya shilingi 5000 baadae bei ikapanda na kufikia shilingi 10,000. Hivi sasa shahada moja hununuliwa kwa shilingi 50,000 kwa mapesa hayo bandia.
Aidha wagombea ubunge na udiwani wametakiwa wajihadhari na watu wanaotuhumiwa kutaka kuwateka nyara au kuwarubuni watelekeze wapiga kura wao.
Imedaiwa kuwa imeundwa kamati maalum kuwafuatilia wagombea wanaoonekana kuhatarisha maslahi ya baadhi ya watu wazito nchini.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa zimedai kuwa mgombea mmoja aliendewa na kikundi cha watu waliomtaka ajiondoe katika kampeni na alisema walikuwa tayari kumlipa mamilioni ya mapesa ili akimbie jimbo lake.
Mgombea huyo alidai kuwa watu hao walikuwa tayari wamlipie hoteli moja ya gharama kubwa ili akae humo mpaka uchaguzi utakapopita.
Aidha walimtaka achague nchi yoyote ili akaishi huko na wao wako tayari kugharamia safari na gharama zote zitakazohitajika akiwa huko.
Hayo yamesemwa na wananchi mbalimbali katika mikoa kadhaa nchini, wakati wakitoa maoni yao wakitathmini maendeleo wa kampeni za uchaguzi huo. Kampeni zinatarajiwa kumalizika Oktoba 28.
Wananchi hao wake kwa waume, vijana na wazee, wamesema katika maoni yao kwamba Prof. Lipumba ana nafasi kubwa ya kupata ushindi kwa kuwa ameweza kujieleza na kueleweka vyema na wananchi waliowengi ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu na kwa makini kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini kote.
Wananchi hao waliozungumza na AN-NUUR katika nyakati tofauti hivi karibuni, wametoa sababu nyingine kadhaa zinazowapelekea kujenga maoni yao hayo.
Miongoni mwa sababu walizozitoa ni pamoja na uwezo wa Prof. Lipumba katika kuchambua hali ya nchi ilivyo hivi sasa, hususan shida zinazowakabili wananchi. Shida za umaskini, maradhi na uwezo mdogo wa kuelimisha watoto wao.
Wamesema kwamba mbali ya kuelezea shida hizo na hali duni zinazowakabili wananchi walio wengi hivi sasa nchini, Prof. Lipumba pia ameweza kuchambua hali hiyo kwa kuonesha jinsi chama tawala na serikali zake walivyosababisha matatizo hayo kwa kushindwa kuwaletea wananchi walio wengi maendeleo yanayofaa.
Vile vile wameeleza wananchi hao katika maoni yao kwamba pamoja na yote hayo, Prof. Lipumba anaweza kufafanua na kuainisha kwa ufasaha zaidi kuhusu uwezo walionao yeye na timu yake ya wagombea wa CUF na CHADEMA katika kuiendeleza nchi na hali za wananchi endapo watachaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa maoni yaliyotolewa na wananchi hao ambao wengi wao ni katika mikoa ya kanda ya ziwa, kanda ya ya kusini, kati na mashariki wamesema kwamba Prof. Lipumba na wagombea wengine wa CUF na CHADEMA wapo pia katika nafasi nzuri zaidi ya ushindi kutokana na jinsi walivyopendekezwa na vyama vyao na namna ambavyo wamekuwa wakiendesha kampeni zao.
Wameeleza kwamba tofauti na wale wa Chama tawala, wale wa CUF na CHADEMA hawakukumbwa na mizengwe ya rushwa, ubaguzi wa kijinsia, rangi, udini au chuki binafsi.
Kuhusu namna ya kuwapata wagombea, wananchi hao wamesema kwamba CCM kimejishushia hadhi mbele ya Watanzania kwa kuonesha hadharani jinsi walivyo wabaguzi.
Mbali ya ubaguzi wa kijinsia, chama hicho pia kimelaumiwa na wananchi kwa mizengwe ya ubinafsi, tamaa ya madaraka kwa mizengwe na ubaguzi wa kitabaka ambapo matajiri ndani ya CCM wanawabagua na kuwadharau wanyonge.
Moja ya ushahidi waliotoa kuhusu lawama hizo ni ule wa chama hicho kuweka kiwango cha shilingi milioni kwa fomu ya kugombea Urais.
" Kiwango hicho ni matokeo ya waliojitajirisha ndani ya CCM kuwadharau wanyonge, wanadhani mtu akikosa milioni basi anakuwa hana haki ya kuongoza nchi yake hata kama wananchi wanajua anao uwezo huo na wanampenda", walisema wananchi hao.
Kutokana na mifano walioitoa pamoja na hoja hizo za lawama, wananchi hao walisema kwamba Watanzania wengi hasa wanawake na wananchi walio wengi ambao ni wanyonge wa maisha na kipato, na wale wasiopenda ubaguzi wa kijinsia au kitabaka, watamchagua Prof. Lipumba na wagombea wengi wa CUF-CHADEMA badala ya CCM.
Katika jumla ya maoni yao, wengi wa wananchi hao wameonesha mtazamo wao kwa Prof. Lipumba na muungano wa CUF na CHADEMA katika uchaguzi mkuu ujao kama kiwakilishi kikuu cha mtazamo wa wananchi wengi walioamua kutoipigia kura CCM.
Wakitoa sababu nyingine ya kutoipigia kura CCM, wananchi hao walitaja jinsi rushwa ilivyojitokeza katika chama hicho wakati wa kupiga kura za maoni kwa wagombea wao wa viti vya udiwani na ubunge.
Wananchi hao walisema kwamba kwa kuwa Watanzania wameamua kupiga vita rushwa, hawawezi kuwachagua watu walioonesha kuipenda rushwa. Wameeleza kwamba watu wa aina hiyo watakapoingia madarakani wanaweza kuiuza nchi kwa watoa rushwa wa kimataifa ambao wanaweza kufanya hivyo ili kupata mikataba, kununua mashirika na machimbo ya madini.
Wanaeleza wananchi hao vile vile kwamba hatma ya chama hicho katika kuwachuja baadhi ya wagombea wa Ubunge kumewasikitisha wengi kwa madai kwamba mchujo huo umeonesha dalili za baadhi ya wagombea kuathiriwa kutokana na dini au rangi zao.
Mifano mingine walioitoa kuonesha udhaifu wa chama tawala ni hoja zinazotolewa katika hotuba za kwenye mikutano ya kampeni. Wananchi hao wamesema kwamba hoja za viongozi wa CCM kwamba wapinzani hawana uwezo wa kuongoza nchi, hazina msingi hata kidogo.
Wakifafanua juu ya hilo, wamesema kwamba kwanza wapinzani hawajaongeza nchi na hivyo hawawezi kuhojiwa. Pili, wamesema kwamba wa kulaumiwa na kuhojiwa ni CCM ambao wamekuwepo madarakani kwa miaka 40, wakipokea kodi na mapato mengine kutokana na jasho la wananchi lakini papo kushindwa kutimiza wajibu wa kuwaletea maendeleo wananchi.
Wananchi hao wakifafanua zaidi wamesema kuwa CCM wanahistoria ya uongozi mbovu. Wameelezea jinsi sera na uongozi wa chama hicho ulivyo vuruga vijiji vya ujamaa kwa kuleta tabu na umaskini kupitia operesheni vijiji na operesheni funga maduka. Wameeleza pia jinsi chama hicho kilivyoua ushirika na kuathiri wakulima wa pareto, tumbaku, kahawa na wa pamba ambao mbali ya kuwapa bei ndogo, walikopa mazao yao na wengine kutolipwa kabisa.
Wameeleza jinsi chama hicho kilivyoangusha uchumi wa nchi, kama viwanda na hata kilimo cha mazao ya chakula na hatimaye kuitumbukiza nchi katika umaskini mkubwa. Wamekumbushia jinsi bidhaa zote zilivyoadimika na wananchi kutegemea chakula cha msaada wa unga wa mahindi ya njano ambayo waliuliziwa kwa foleni na bei ya "kuruka" kwenye maduka ya kaya.
Wananchi hao wamesema kuwa wameshangazwa na kauli za viongozi na wagombea wa CCM kujisifu kufutiwa madeni na kukopa madeni mengine pasipo kuona aibu ya kushindwa kuongoza nchi na kutumia vibaya kodi za wananchi kiasi cha kuifilisi nchi na kuitumbukiza kwenye madeni.
Imeelezwa na wananchi hao kwamba mfano mwingine wa jinsi CCM wasivyo na uwezo wa kuongoza, ni ule wa miradi na uwezo wa kuongoza, ni ule wa miradi yao binafsi ya biashara na ufugaji, ukiwemo ufugaji wa nguruwe, chini ya shirika la SUKITA.
Wamedai kuwa miradi hiyo imekufa kwa uongozi mbovu.
Wameeleza wananchi hao kwamba propaganda za kutuhumu wapinzani kwa hoja dhaifu ndicho kinachoifanya CCM idharauliwe na wananchi na pia kuwafanya wananchi hao wamuelewe zaidi Prof. Lipumba ambaye anaonekana kuwa karibu sana na wananchi kwa ukweli wa yale anayoyazungumza.
Wamesema kwa wakati Prof. Lipumba anaeleza udhaifu wa CCM katika kuuza mashirika na viwanda vya umma kwa bei ya "kutupa" na kusababisha wafanyakazi wengi kuachishwa kazi kwa malipo madogo na wananchi wengine, hasa vijana kuendelea kukosa ajira. Mgombea wa CCM anadai kuwa kaleta maendeleo ya uchumi na kuongeza ajira.
Wananchi hao wameeleza kwamba katika hali hiyo, Watanzania wengi lazima watakubaliana na Lipumba na kushindwa kumuelewa Mkapa. Maana wamesema, walioachishwa kazi viwanda vya nguo, bandari, benki na kwingine wapo tena wengi sana na kwamba hao ni dhahiri kura zao zitakwenda kwa yule anayesema yale wanayoyajua ukweli wake.
Wamesema kwamba kitendo cha CCM na mgombea wao kudai kuwa wameleta maendeleo kinyume cha ukweli, ni cha kuwadharau wananchi. Wanatoa mfano jinsi wananchi zaidi ya 40 walivyokufa kwa njaa wilayani Ulanga, Morogoro. Wameeleza kuwa wakati wananchi hao wanakufa Morogoro, mahindi yameachwa yanaoza kwenye ghala la akiba ya taifa. Tena wamedai wananchi hao, wakati mahindi mengine yapo kwa wakulima mkoani Rukwa pasipo soko, serikali ya CCM inawaagiza wafanyabiashara wakubwa nchini kwenda kununua mahindi nje ya nchi.
Wameeleza pia jinsi CCM walivyoshindwa kujibu hoja ya Prof. Lipumba kuhusu suala la ufinyu wa bajeti ya elimu. Wamesema kwamba ni aibu kuona viongozi wa juu wa CCM wanashindwa kutoa kauli moja, dalili ambayo wamedai ni matokeo ya kutaka kuwababaisha wananchi. Wamehoji kama Mkapa anadai bajeti hiyo ni asilimia 38 (38%), Kinana 33% na Malocho ni 15%, nani mkweli!
Katika tathmini yao, wananchi hao wamesema pia kwamba CCM katika hotuba za wagombea wake imekuwa ikiwababaisha wananchi kwa kutofafanua vyema sera na muelekeo wao. Wameeleza wananchi hao kuwa wagombea wao wanapokwenda vijijini wanawaambia wananchi kuwa lazima wajitegemee na kulipa kodi ili wapate maendeleo wanayoyataka. Lakini wagombea hao hao wanapokuwa mijini wanaahidi misaada mingi ya maendeleo kutoka kwa wafadhili.
"Ndio maana wananchi wengi wamevutiwa na sera za "Haki sawa kwa wote", anazozitetea Prof. Lipumba", wamesema wananchi hao.
Suala lingine lililoelezwa na wananchi hao kama kielelezo cha 'undumilakuwili wa CCM ni kuhusu kwamba vijana wengi wanadhalilishwa kwa kukamatwa na kuteswa mahabusu kwa visingizio vya tuhuma za uzururaji katika nchi yao wenyewe.
Wamedai kuwa CCM imefanya hivyo kiubaguzi na kiundumilakuwili. Kwani imeshuhudia vijana wa viongozi wa chama hicho na serikali yake wakipewa ajira, elimu nzuri ndani na nje ya nchi, na wengine kupewa mitaji mikubwa yakujiendeleza katika biashara.
Mbali ya madhila hayo, wananchi hao pia wamedai kuwa chama hicho na viongozi wake wamekuwa wakiwachukulia vijana wengi kama watu wasio na uwezo wa kuelewa mambo ya propaganda. Wametoa mfano wa viongozi walivyotoa ahadi kwa vijana wafanyabiashara za mikononi "machinga" kwamba ingelianzishwa benki ya kuwasaidia na maeneo ya kufanyabiashara lakini hakuna kilichofanyika. Wamedai vile vile kuwa wakati hakuna dalili ya benki hiyo, zipo fununu za mipango ya kuwaondoa kwa nguvu vijana hao toka mijini.
Suala lingine lililoelezwa na wananchi hao kuwa limewashushuia sana hadhi CCM mbele ya wananchi, ni propaganda za chuki kuhusu kwamba CCM imekuwa ikitoa propaganda hizo dhidi ya wapinzani hasa wa chama cha CUF. Lakini wamesema, propaganda hizo zimewarudia wenyewe CCM ambako imedaiwa kuwa ndiko kwenye udini, ukabila na ubinafsi.
Wameeleza wananchi hao kwamba CCM na serikali yake wameshindwa kujibu tuhuma za Waislamu kuhusu mauaji ya Mwembechai, wakati wanadaiwa kuwasikiliza Paroko wa Kanisa Katoliki. Wanadaiwa kuwatesa wahadhir wa Kiislamu na kuwaachia wahubiri wa Kikristo. Inazuia mihadhara na kuruhusu kugawa Biblia kwa wanafunzi wa shule za msingi. Inazuia kitabu cha "Mwembechai Killings" na kuruhusu cha "Kanisa Katoliki na siasa Tanzania Bara".
Chama hicho kimelaumiwa pia kwa kujaza viongozi wa Kikristo wakati kiongozi wake Cleopa Msuya kachukizwa CUF kuongowa na Muislamu, kiongozi wake John Malecela "kumbatiza" Muislamu aliyejiunga na CCM. Chama hicho kutoa propaganda za ukabila dhidi ya wapinzani wakati baadhi ya viongozi wake wanawataka wananchi wawachague watoto wao, marafiki zao, ndugu, jamaa na mashemeji zao kushika nafasi za uongozi.
Viongozi wa chama hicho vile vile wamelaumiwa kwa hotuba za chuki na kauli za propaganda zisizopendeza.
Imeelezwa na wananchi hao katika maoni yao hayo ya tathmini ya hali ya kampeni za uchaguzi na matumaini ya matokeo kwa wagombea, kwamba na matumaini ya matokeo kwa wagombea, kwamba inaelekea viongozi na wanahoja zao nyingi mbele ya wananchi kuwa hoja zao nyingi mbele ya wananchi zimegundulika kuwa ni dhaifu na kutokubalika, waliamua kuingia kwenye propaganda chafu za kumshambulia mgombea wa CUF Prof. Lipumba.
Hata hivyo, wameeleza wananchi hao kwamba propaganda hizo na walizozianzisha walinywea baada ya kugundua kwamba wananchi wengi wanazijua familia za viongozi hao na matatizo yaliyomo kwenye baadhi ya familia za viongozi wengi wa chama tawala ambao ungelifichuliwa hadharani.
Wananchi hao katika maoni yao wameonesha kufurahishwa na mwenendo wa Prof. Lipumba katika kampeni. Wameeleza kwamba wakati viongozi wa chama tawala wanatumia muda mwingi kutoa propaganda dhidi ya wapinzani, Lipumba amekuwa akitumia muda wake wote kuongea na wananchi, akihutubia kujibu maswali na kupokea ushauri wao.
Mwenendo huo wamedai wananchi hao, umemuongezea Prof. Lipumba umaarufu na kufutilia mbali propaganda zinazodai kuwa wapinzani hawakubaliki na ni waroho wa madaraka.
Wamesema kwamba kama ni uroho wa madaraka, basi wanao wale waliokaa madarakani kwa miaka 40, wakaifanya nchi hii miongoni mwa nchi masikini zilizoshindwa kulipa madeni wakaifanya ya pili kwa umaskini duniani na ya tatu kwa rushwa barani Afrika, lakini ikawa bado wanang'ang'ania kuongoza.
Pamoja na maoni yao hayo, wananchi hao pia wameviomba vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi kuielewa hali ya mwelekeo wa kampeni na kudhibiti kauli za vitisho na zile zisizopendeza toka chama tawala pasipo kuwaonea haya ili kujenga mazingira mema yaliyohuru na haki kwa wananchi.
Wananchi hao wameeleza kuwa ni vema vyombo hivyo vikatambua kuwa wananchi waliowengi wameishaamua kuleta mabadiliko katika utawala wa nchi yao. Hivyo, wamesema, ni mategemeo yao kuwa vyombo hivyo, vitaikubali hali hiyo na matakwa ya wananchi kwa njia ya usalama na amani kama ilivyotokea Zambia, Senegal na kwingineko. Wamewaomba kupuuza propaganda za chama tawala kwamba wapinzani wakishinda wataleta vurugu.
Wananchi hao wamesema: "Siku zote mshindi huwa ni mwenye furaha, hizo vurugu zitatokea wapi!"
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |