Watangazaji wawili wa BBC wakabwa na makachero
WATANGAZAJI wa shirika la Utangazaji la Uingereza BBC juzi walifikishwa kituo cha polisi wilayani Nachingwea na maafisa usalama wa Taifa kwa madai kwamba walitaka kuchukua picha za matanazo ya televisheni za mgombea wa Urais kwa tiketi ya chama cha CUF na CHADEMA, Prof. Ibrahim Lipumba bila kibali.

Watangazaji hao ambao ni raia wawili wa Uingereza na mmoja kutoka Kenya waliingia nchini kuchukua picha za matangazo kwenye mikutano ya kampeni iliofanywa na Prof. Lipumba wilayani Nachingwea siku ya Jumamosi.

Watangazaji hao wameanza kusumbuliwa na maafisa usalama walipokuwa wameandamana na Mwenyekiti wa chama cha CUF wilayani humo Bw. Ahmad Matajiri ambaye alikuwa ndiye mwenyeji wa wageni hao.

Maafisa hao wa usalama walimhoji Bw. Matajiri pamoja na watangazaji hao sababu za kuwepo kwao Nachingwea.

Hata hivyo ilibainika kwamba watangazaji hao pamoja na mwenyeji wao hawakuwa na kosa kwani taarifa za kuwepo kwao zilithibitishwa na mkuu wa wilaya ambaye alishapata habari za ujio kwa watangazaji hao toka kwa Waziri Mkuu ambapo pia walisaini kitabu cha wageni.

Lakini hata baada ya Prof. Lipumba kwanza mkutano wa kampeni, maafisa usalama waliendelea kuwazuia watangazaji hao wa BBC kuchukua picha za matangazo hali iliyopelekea mgombea mwenza Bw. Nassor Khamis kuingilia kati na kuwaonya hadharani ndipo walipoamua kukaa pembeni na wapiga picha hao kuendelea na kazi yao. Baada ya mkutano watangazaji hao walifanya mahojiano na Prof. Ibrahim Lipumba.

Kabla ya kuja kwa watangazaji na wapiga picha za televisheni wa BBC, mwakilishi wa shirika hilo Afrika Mashariki Bi Catty Jenkis alimtaarifu Prof. Lipumba kuhusu kuja kwao mkoani Lindi ili kuchukua picha za matangazo ya televisheni ambayo yatarushwa hewani na kituo hiho muda mfupi baada ya kukamilika.


CUF Zenji wafunga kazi, wawaambia polisi:
Ishakuwa ngangari tunataka haki zetu


"HATA mkitupekuwa, Seifu tushamchagua. Hata mkitupiga hatuhamaki".

Hayo ni maneno yaliyokuwa yakitolewa na akinamama na vijana waliokuwa wakiimba na kurukaruka mbele ya polisi Jumamosi huko Kibandamaiti, Zanzibar.

Wakiwa sehemu ya umati mkubwa uliojitokeza katika mkutano wa Maalim Seif, makundi ya akinamama walikuwa wakiwakabili polisi waliojazana uwanjani hapo kuelezea unyama wanaowafanyia.

Huku wakipeperusha bendera za CUF, akinamama hao wakiwemo vikongwe waliwaambia polisi uso kwa macho hata wawapekue sehemu wasizoruhusiwa, hawatahamaki.

Walidai ngangari yao mwaka huu ni kumuingiza Maalim Seif Ikulu na hawatokatishwa tamaa na vitendo vyao (polisi) vya kuwadhalilisha.

Katika mkutano wa Jumamosi, magari yote yaliyoingia Kibandamaiti kutokea njia ya Mwera yalisimamishwa eneo la Uwanja wa Amani na watu kupekuliwa.

Hata hivyo wale waliokuwa wakitokea mjini kwenda Chwaka kwenye mkutano wa CCM, japo walipitia hapo hapo kwenye kizuizi cha polisi hawakupekuliwa.

Bi kizee mmoja jasho likimtoka aliwaambia polisi wapatao watano walioshikilia marungu, "virungu vyenu ndio ubani. Hivi umpige mtu ndio atakupenda. Tupigeni lakini mtu wenu hatumtaki".

Waliotia for a zaidi katika mkutano huo walikuwa vijana mithili ya Kossovo wa Dar es Salaam.

Wao walikuwa wakizunguka uwanja mzima huku wakiimba nyimbo na kuweka kituo pale waonapo polisi wamejazana.

Pamoja na nyimbo nyingi walizokuwa wakiziimba, lakini zaidi walipeleka salamu kwa polisi kuwa wao agenda yao ni kuing'oa CCM na wala sio mapambano nao (polisi).

Kwa mantiki hiyo walikariri mara kwa mara kibwagizo kisemacho "hatamkitupiga, CCM hatuitaki, hatamkitupiga hatuhamaki".

Katika mkutano wa Jumamosi Kibandamaiti mamia ya polisi walikuwa wamemwagwa katika eneo la mkutano.

Pamoja na virungu vya kawaida vya polisi, wengine walishikilia mikwaju, magongo na hata vipande vya kuni.

Mwandishi wa habari hizi aliyekuwa kiwanjani hapo aliwashuhudia polisi wapatao 20 wakiwa na bunduki, wakitembea au kusimama kati ya vikundi vya wale wenye marungu.

Pamoja na nyuso zilizokuwa zinaashiria shari za polisi waliokuwa wamejazana, wananchi walikuwa wakiimba na kucheza bila ya hofu.

Miongoni mwa vibwagizo vilivyokuwa vimetamalaki kabla ya mkutano kuanza rasmi ni kile kilichogeuzwa kutoka wimbo wa TOT wa Maombolezo ya Mwalimu Nyerere:

"...Uchumi umedidimia, nchi inaangamia, ajira imetoweka, twasema..."

"...CCM kwao kiza kimetanda hawana pa kwenda...".

"CCM washasema kwao kiza kimetanda na penye kiza hakukaliki", alisherehesha mkuu wa jukwaa (MC) huku akiwataka wananchi kutowapa kura watu waliodidimiza uchumi na kufanya ajira itoweke.

Akihutubia mkutano huu, mgombea kupitia Chama cha CUF, Seif Sharif Hamad alidai kuwa, uhuru wa Zanzibar ulikoma simu ya 137 baada ya Mapinduzi.

Alisema baada ya siku hizo, ulikuja Muungano ambao ulikuja kwenda kinyume na mkataba wa awali.

Akadai kuwa, Muungano umehujumiwa na uhuru wa Zanzibar kuporwa baada ya mkataba wa Muungano kuongezwa vipengele vyake kufikia 27 toka maeneo 11 yaliyokubaliwa awali.

Maalim Seif alidai kuwa makampuni mawili kutoka Denmark na Marekani yalishafanya uchunguzi na kugundua kuwa Zanzibar kuna mafuta ya kutosha.

Alisema, mafuta hayo yaweza kuchimbwa kwa miakak 80 na kuipatia Zanzbar dola za Kimarekani bilioni 100 kwa mwaka.

Wakati huo huo, Chama cha CUF kimedai kuwa kimegundua mpango unaofanywa kupunguza wapiga kura wa chama hicho.

Taarifa ya chama hicho imeeleza kuwa wapo makachero waliopewa tenda ya kupunguza wapiga kura wapatao 50,000 wanaoaminika kuwa wa CUF.

Hata hivyo, haikufafanuliwa idadi hiyo itapunguzwaje, ila taarifa zinadai kuwa malalamiko ya chama hicho yashapelekwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.


Mkapa aahidi kujenga barabara Singida


MGOMBEA wa Urais Tanzania kupitia CCM, Mh. Benjamin Mkapa ameeleza kuwa Serikali yake imejenga maelfu ya Kilometa za bara bara.

Aidha amesema, katika utawala wake bara bara zenye urefu wa takribani kilomita 5000 zimekarabatiwa baada ya kuharibiwa na mvua za elnino.

Akiongea huko Itigi na Manyoni jana, Mkapa alisema kuwa Serikali yake imetumia shilingi zipatazo bilioni 2.9 kukarabati barabara za Singida.

Aidha amesema mipango ya kujenga barabara ya Singida - Shelui imekamilika na kwamba sasa anatafutwa mkandarasi.

Huko Zanzibar, Bwana Aman Karume amewataka Wazanzibar wachague CCM iliyowaletea amani na utulivu.

Karume alikuwa akihutubia mkutano wa Kampeni huko Chwaka juzi.

Katika mkutano huo Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliwataka WanaCCM wasiwaogope wapinzani akidai kwamba dola ipo imara.

Kutoka Kigoma, Mheshimiwa John Cheyo amesema akichaguliwa kuwa Rais atakaribisha vyama vingine kwenye serikali yake.

Mheshimiwa Cheyo anayegombea Urais wa Tanzania kupitia chama cha UDP alikuwa akizungumza jana mjini humo.

Huko Tanga, mgombea Ubunge Tanga mjini kupitia CCM Bwana Bakari Mwapachu alishindwa kuhutubia jumamosi baada ya kukosa watu.

Bwana Mwapachu aliandaa mkutano wake Tanga kati barabara ya 10, wakati CUF walikuwa barabara ya 11.

Umati wa watu ulifika barabara ya 11 kumsikiliza mgombea wa CUF Bwana Nuru Diwani pamoja na wagombea Udiwani wa chama hicho.

Wakati huo huo, Mgombea ubunge kupitia CCM jimbo la ubungo bwana Charles Keenja amedaiwa kuwa katika wakati mgumu katika kinyang'anyiro hicho kufuatia mikutano yake kuhudhuriwa na watu wachache.

WanaCCM wanaofuatilia kampeni za mgombea huyo mbaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Jiji iliyoundwa na waziri mkuu baada ya kuondolewa madiwani, wamesema mikutano ya Keenja inatia wasi wasi.

Katika mkutano mmoja uliofanyika jumamosi katika eneo jirani na TANESCO mgombea huyo alipata idadi ndogo sana ya wananchi hali iliyopelekea wapambe wake kufanya kazi ya ziada kutafadhalisha wapita njia wasimame kusikiliza sera za mgombea wao.

MwanaCCM mmoja aliyekuwepo katika mkutano huo alisikika akitamka kuwa mwaka huu ni mgumu sana kwa CCM kwa kuwa baadhi ya wananchi wamesusia kabisa mikutano ya chama chao.

"Itabidi tuhoji iwapo CCM itatangazwa mshindi, dalili zote zinaonesha watu hawako nayo, amedai mwananchi mmoja anayeishi Ubungo aliyejitambulisha kwa jina la Ridhwan Juma.

Miongoni mwa mambo yanayotajwa kuiweka CCM katika hali ngumu jimbo la Ubungo ni pamoja na bomoa bomoa ya nyumba na vibanda vya biashara kando kando ya bara bara ya Morogoro.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook