PROFESA Ibrahim Lipumba aligombewa mithili ya mpira wa kona mara baada ya kuwasili eneo la Somanga Wilayani hapa.
Hali hiyo ilifuatia mabishano kati ya wanavijiji wa Kilwa kusini na wale kaskazini ambao kwa pamoja walikusanyika mahali hapo kumpokea mgombea huyo ambaye anaendelea na kampeni zake mikoa ya kusini.
Taarifa zilizotolewa awali na chama cha CUF Wilaya Profesa Lipumba akiwa na mgombea wake mwenza, wangewasili mjini hapa nyakati za mchana, hata hivyo waliwasili eneo la Somanga saa nne za usiku.
Kabla ya kuwasili kwao, mnamo saa 10 jioni wanaCCM walikuwa wakitamba na kuwazomea wananchi hao wakidai Lipumba 'kawatapeli' na asingefika siku hiyo.
Hata hivyo wananchi hao waliendelea kusubiri mahali hapo mpaka saa mbili usiku alipowasili mgombea Mwenza Bwana Nassoro Khamis.
Wakiwa wamewasha mienge ya moto, wananchi hao walioshinda kutwa nzima mahali hapo ghafla waliripuka kushangilia kufuatia kuchomoza gari lililomchukua mgombea huyo mwenza.
Ilipotimu saa nne za usiku Profesa Lipumba aliwasili Somanga tukio lililoamsha hoi hoi kubwa kutoka kwa wananchi waliojazana mahali hapo.
Hata hivyo, mabishano makali yalizuka baina ya pande mbili ambapo kila upande ukidai uwe mwenyeji wa wagombea hao. Hatimaye iliafikiwa kuwa Profesa Lipumba aelekee Kilwa kaskazini na bwana Nassor Khamis aende kusini.
Akiwa Kilwa Kipatimu imeripotiwa kuwa wananchi walikesha wakiwa katika shamra shamra kubwa.
Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika kata ya Kipatimu wilayani hapa, Profesa Lipumba alidai kuwa serikali ya CCM imewapa kisogo wakazi wa eneo hilo kwa kutelekeza rasilimali lukuki zilizojaa ikiwa ni pamoja na gesi ya Songo songo, zao la Korosho, ufuta na matunda.
Alisema rasilimali hizo zingetumiwa vyema na serikali wananchi wa ukanda wa kusini wasingekuwa na hali duni za kimaisha.
Amesema tatizo linalosababisha maisha magumu kwa watanzania ni sera mbovu za CCM.
Aidha aliongeza kuwa serikali ya CCM imeshindwa kutambua umuhimu wa mkoa wa Lindi katika kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kuwepo mali asili hasa gesi ya Songo songo ambayo ni mali ghafi katika kuzalisha nguvu za umeme, mali ghafi ya kutengenezea mbolea na wakati huo huo kutoa ajira kwa wakazi wa mkoa huo.
Naye Mgombea Mwenza Bwana Nasoro Khamis alitoa hotuba iliyowaacha uma uliohudhuria wakiwemo polisi kushangilia kwa nguvu.
Katika mkutano huo zaidi ya wanachama 106 wa CCM walirudisha kadi na kujiunga na CUF.
Mgombea huyo pia alizungumza na wazee wa mji huo
kabla ya kuondoka kuelekea Liwale.
WAFANYAKAZI wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesema hawataka kata tamaa endapo serikali ya CCM haitotoa maelezo ya kutosha juu ya mafao yao wamedai ni kujisaliti wenyewe iwapo wataipa CCM kura.
Pia wamesema kama serikali itafikiria kuwalipa malipo yao ni lazima yafanane na wenzao wa nchi za Uganda na Kenya ambao hawakupewa usumbufu na serikali zao.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya kushughulikia mafao hayo Bw. Idd Maganga akiongea na gazeti hili jana nje ya hoteli ya Starlight amesema, hawatakubali haki zao zipotee bure na kuazimia kuzitafuta na kuzichukua kwa gharama yoyote ile.
Aidha, mjumbe huo amesema, wamegundua njama za serikali katika kuwahujumu kupitia kesi yao walioifungua mahakama kuu mwezi Agosti mwaka huu.
Amesema kuwa walipofungua kesi hiyo Agosti 15, mwaka huu, Jaji wa mahakama hiyo aliipa wiki mbili serikali itoe pingamizi ambapo mwisho ilikuwa Agosti 19, jambo ambalo hawajalitekeleza na kuja kulifanya Septemba 5 na kuonesha kuwa pingamizi limewekwa Agosti 29 kwa kupitia taratibu zote.
"Tunalazimika kutoipa kura CCM iwapo serikali yake haitotupatia haki mpaka Oktoba 28, mwaka huu", alisema mzee mmoja mtumishi wa iliyokuwa jumuiya ambaye hakupenda jina liwepo gazetini.
Baadhi ya wafanyakazi wa iliyokuwa jumuiya hiyo akiwemo Bw. Mohamed Ibrahim, Kassim Mohamed, Thadeus Thomas, Joseph Simbeye pamoja na Ibrahim Bwata wamedai kuwa CCM mhimili wake mkubwa ni wazee, sasa kama wameamua kuwadhulumu basi nao watakipiga pande chama hicho.
"Vijana wengi hawaipendi CCM ambayo kwa kiasi kikubwa inashikiliwa na wazee hivyo tukiamua kuweka mkakati basi hakuna chao", walisema wazee hao ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakifuatilia mafao yao hayo ambapo wengine wakawa wamelipwa shilingi 10, huku wengine wakipewa hundi zenye kuonyesha wanadaiwa.
Katika kesi yao hiyo ambayo inajumuisha wafanyakazi kutoka zaidi ya makampuni 22, wastaafu hao wanatetewana wakili Bishota Diemka. Jana walitarajiwa kukutana katika hoteli ya Starlight kwa ajili ya kuweka mikakati zaidi ya kupambana na dhalimu wao serikali.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |