Na Prof. Abdallah J. Saffari
ASKARI mmoja mwanamke alipigwa na washabiki wa CUF wenye hasira hadi kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi hospitalini. Na katika tukio jingine kijana mmoja alipigwa risasi ya mguu na askari bila ya sababu ya msingi.
Kwa upande mwingine udhalilishaji wa siri siri unaweza kuwa na sura nyingi kwa mfano kuzuiwa kwa vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara bila ya sababu za msingi. Jambo hili limetukia mara zisizo hesabu hasa dhidi ya chama cha CUF na wagombea wake wakuu Profesa Lipumba na Maalim Seif Hamad. Katika matukio ya hivi karibuni tu polisi mjini Sumbawanga walimshusha jukwaani Profesa Lipumba katika mkutano wa kampeni. Polisi walidai muda wa kampeni ulipita, wakati huu ilikuwa saa kumi na mbili. Lakini ukweli ni kwamba muda wa kumaliza mikutano ya kampeni kwa mujibu wa Tume ulikuwa sio saa kumi na mbili bali ni saa moja ya usiku.
Nyakati nyingine kwa makusudi kabisa, polisi huzuia misafara ya washabiki wa vyama vya upinzani na viongozi wao. Matukio ya hivi karibuni kule Kigoma na Rukwa ni ushahidi tosha. Polisi wa Dar es Salaam walidiriki hata kuwakataza hata dereva wa daladala wasikubali kukodiwa na wanachama wa CUF kwenda uwanja wa ndege kumpokea Profesa Lipumba aliporejea kutoka Mwanza ambako alichaguliwa kuwa mgombea wa chama chake. Na polisi hao hao walivamia msafara wa CUF usipite Jangwani kuelekea Uwanja wa Kidongo Chekundu kuhudhuria uzinduzi wa kampeni za chama hicho. Katika kutimiza jambo hilo wakatumia mabomu ya machozi bila sababu ya maana kabisa.
Inachekesha na kwa kweli ni kejeli tupu kusikia vile polisi wanavyowaita waandishi wa habari kutetea vitendo vyao hivyo. La ajabu ni kuwa hatujasikia polisi wakimzuia kiongozi wa CCM wala wafuasi wao hata siku moja licha ya kampeni za matusi na uchochezi zinazoendeshwa na baadhi ya viongozi wao wa juu na vikundi vyao vya sanaa kama vile TOT.
Zaidi ya yote kuna aina nyingine ya udhalilishaji mbaya zaidi. Huu ni kuzusha kesi za uongo dhidi ya viongozi wa upinzani. Kesi hizi zimekuwa ama za madai au jinai. Mpaka sasa viongozi wote maarufu wa upinzani ama walikabliwa au bado wanakabiliwa na kesi za aina hiyo. Wao ni pamoja na Profesa Lipumba, Maalim Seif Hamad, John Cheyo, Augustine Mrema, Leo Lwekamwa na Mchungaji Mtikila. Lakini, kwa mizani ile ile hatujasikia hata kiongozi mmoja wa CCM wala wapiga debe wao 'domo kaya' wakishitakiwa japo kwa matusi!
Aina hizi za udhalilishaji zinalenga kuwavunja nguvu viongozi wa upinzani na mashabiki wao. Pia zina nia ya kupanda mbegu ya ujinga kwa kuhofu kuwa mikutano ya wapinzani itawapa wananchi taarifa sahihi kuhusu kushindwa kwa sera za 'amani na utulivu' hewa ambazo hazimsaidii mlalahoi kupata elimu, matibabu, usafiri wala haki katika vyombo vya sheria.
Lakini zaidi ya yote, vitendo hivyo vinakusudia kuwafananisha wapinzani na wahalifu hivyo kuvunja heshima yao machoni pa Watanzania ambao wanakusudia kuwaweka madarakani.
HOFU
Mwenyezi Mungu anamtaka binadamu ajiepushe na hofu iliyoko moyoni mwake inayoweza kusababishwa na binadamu mwenzake na hata viumbe wasio binadamu kama vile majini. Hekima hii ya Muumba wa viumbe na Mmiliki wa dunia hii ni kuwa hofu ndiyo adui mkubwa wa matendo ya binadamu.
Kuna hofu za msingi ambazo hutufanya tusifanye matendo mabaya kama vile kutoa na kupokea rushwa, kuiba fedha za wananchi au kuiuza nchi hii kwa makaburu na kadhalika. Lakini hofu mbaya ni ile ya kuogopa kujijasirisha kufanya matendo ya mageuzi minghairi ya matendo ambayo tumeyagusia hapo juu punde tu.
Kwa bahati mbaya vyama vyote vikongwe duniani kote ambavyo vimeshindwa kutoa ushahidi wa maendeleo waliyoleta kwa watu wao hutumia hofu kuwatisha watu hao kukataa mabadiliko ili wajikwamue pale walipo. Kuna mbinu nyingi za kutia hofu wapiga kura. Kwa mfano kwa miaka kumi na sita mfululizo Chama cha Mamwinyi Uingereza yaani Conservatives kilikuwa kinakisakama Chama kikuu cha upinzani nchini huko, Chama cha Wafanyakazi, yaani Labour Party. Walikuwa hawajishughulishi na Liberal Democrats Party cha huko kwa vile chama hicho hakikuwa tishio kwao. Basi mbinu kuu ya hofu waliyokuwa wanaitumia ni kudai kuwa chama cha wafanyakazi yaani Labour Party ni chama cha Makomunist, chama cha kutoza kodi kubwa zisizo na msingi ili kuwabana wenye viwanda na mabwanyenye ili kuwapendelea walala hoi. Pia walidai eti sera mbaya za chama hicho zingezua migogoro mipya viwandani na kuwakosesha watu kazi na kupunguza pato la taifa kwa jumla.
Sasa kwa miaka yote kumi na sita Waingereza kweli wakaingiwa na hofu kubwa kuhusu maendeleo yao kutokana na hoja hizo muflisi kabisa. Mpaka pale Tonny Blair alipochaguliwa kukiongoza chama cha Wafanayakazi akatamka katika Bunge la nchi hiyo kwamba silaha kubwa ya Chama cha Mamwinyi ni uongo uliokusudiwa kuwatia hofu Waingereza. Akasema dawa kubwa ni kuwaelimisha Waingereza na kuondoa hofu iliyojikita nyoyoni mwao. Na kweli uchaguzi uliofuatia ukaking'oa madarakani Chama cha Mamwinyi kwa kura nyingi mno. Hivi sasa Uingereza imepata mafanikio makubwa mno chini ya Chama cha Labour kwa muda mfupi tu tangu kushika madaraka.
Silka hii ya kutia hofu nyoyoni mwa Waafrika na hususan Watanzania inabainika katika kauli za viongozi wa CCM kila uchao. Mbiu kauli kubwa hivi sasa ni Amani na Utulivu. Sawa, hakuna asiyejua umuhimu wa mambo haya. Ila amani hii haikuletwa na CCM. Hakika ni wananchi tu wa nchi hii ni watu wenye uvumilivu na subira isiyo na mfano duniani. Tujiulize ni amani na utulivu vimeleta maendeleo gani nchini? Hivi leo nchi hii imepitwa kwa maendeleo na nchi nyingi zilizokuwa vitani kwa zaidi ya miaka ishirini.
Hata Clinton alisema wazi kuhusu vile Msumbiji ilivyoweza kuitumia amani ya muda mfupi kujipatia kasi kubwa ya uchumi katika dunia. Uganda pia ni mfano mwingine. Watu huangalia maendeleo yao kwa kipindi chote cha utawala wa CCM hususan Elimu, tiba, haki, usafiri, na kugundua kuwa mambo hayo yameporomoka vibaya mno. Leo hii idadi kubwa ya Watanzania hawajui kusoma na kuandika. Watu wamerejea kule walikotoka. Maendeleo ni ya wachache mno. Hao ndiyo ambao wana amani na utulivu nyoyoni mwao, siyo walala hoi milioni thelathini wa nchi hii. Sasa ni muhimu wapiga kura kuelewa mbinu zinazowatia hofu na kuamua kuwa jasiri na jabari.
Hitimisho
Sababu kubwa ya kuwa na serikali ni kuhakikisha inaleta maendeleo kwa wananchi wake kama vile ambavyo waliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi. Serikali pia inatakiwa kutekeleza mambo yake kwa uwazi siyo mizengwe. Na ni muhimu iwajibike kwa makosa yake. Wakishindwa kutimiza hayo basi watu waweze kuamua na kuwang'oa madarakani kwa mujibu wa katiba na sheria zinazohusika.
Wimbi la mageuzi tayari limelikumba bara la Afrika na kuzing'oa madarakani serikali na vyama vikongwe huko Zambia, Malawi, Senegal na chupuchupu kufanya hivyo Kenya na Zimbabwe hivi karibuni tu. Mageuzi haya yanatoa mafunzo mawili makubwa. Mosi, ada ya mja kunena, muungwana ni vitendo. Watu wa Afrika na hasa Tanzania wamechoshwa na subira ya ahadi hewa kutoka kwa wanasiasa wachovu na chama chao. Funzo la pili ni kuwa mamlaka ya dola sharti yatumiwe kuleta maendeleo kwa wote sio kwa waroho wachache.
Ila muhimu kupita yote tunajifunza kuwa ujinga ni adui mkubwa wa demokrasia. Hivyo basi elimu ya uraia, upatikanaji habari sahihi siyo za uzushi kutoka kwa vyombo vya habari huru na kutokuwepo kwa udhalilishaji kutoka taasisi za serikali ni muhimu kwa demokrasia ya kweli.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |