Kuisimamisha haki kwa nadharia na vitendo- 3

MZAZI ni aina ya tatu ya mwalimu. Upo msemo wa kuwa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Na Mtume (s.a.w.) amesema, kila mtoto huzaliwa akiwa mnyoofu. Ni wazazi wake watakaomfanya awe Myahudi, Mkristo au Mmajusi. Mtoto huzaliwa akiwa mweupe pasi na tone la uovu.

Pengine tunasikia nadharia zisizo na ukweli. Kwamba kuna dhambi za asili kwa kila azaliwaye. Kama ni kweli, basi dhana ya kila mtu kubeba mzigo wake hupoteza maana. Na ikiwa ndivyo uadilifu wa Mungu utaingiwa doa!

Hata Yesu kasema, tusipokuwa kama watoto hatutorithi ufalme wa mbinguni. Wazazi ni walimu wa kufundisha utamaduni wajamii. Ni walimu wa awali wanapandikiza vigezo vya kujua zuri na baya, haki na batili, wema na uovu pamoja na miiko ya kijamii.

Ualimu wa wazazi kwa watoto unatokana na ujuzi walionao kutokana na uzoefu wa kimaisha. Huweza kuwafunza na kutoa ushauri nasaha utakaowawezesha watoto kuwa raia na viongozi bora wa jamii. Hivyo, wazazi ni miongoni mwa walimu.

Maisha yana utamu na mvuto wa aina yake. Bahati mbaya si mambo yote matamu yana mwisho mwema. Ukweli huu unajulikana kwa wazazi, watoto huwa gizani katika hili. Kwa msingi huu, wazazi huwaokoa watoto kutoka kwenye janga la kupupia kila king'aracho.

Wazazi wasipotekeleza wajibu wao, kuna hatari ya watoto kufunzwa na 'mwalimu dunia'. Katika mazingira ya sasa, mtalaa wa mwalimu dunia ni wa hivyo. Ni kama shimo la choo au pipa la takataka. Hauzingatii wakati, umri wala kuchagua kinachofaa.

Tazama hiyo timu ya walimu dunia. Katika kila pembe wameweka mabango ya kufundishia.. "Urithi wetu, asili yake Tanzania", "Tumia salama" yanasomeka mabango hayo. Wapo wale wanaotumia redio na TV. Sawa nao hufunza kwa namna yao. Ukitaka kulijua chunguza maadili ya watoto wanaolelewa kwa TV.

Wapo wanaofunza kupitia viti vya uongozi. Hao hawasiti kuhamasisha zinaa kwa nembo ya kujikinga na ukimwi. Utashangaa kuona vijana wengi wamekuwa maprofesa katika maovu. Ukweli ni kwamba, wanafunzwa mengi kutoka kwa mwalimu dunia.

Wazazi wanatakiwa kupania kuwaandalia watoto wao mazingira yatakayomwekea wigo mwalimu dunia. Msingi wa wigo huo ni kuhakikisha kuwa rungu la dola halikabidhiwi wagonjwa wa maadili. Kwa kulifanya hilo, mafunzo mema watakayowapa watoto wao yatapata mwendelezo chanya.

Wakipatikana wazazi watakaofuata nyayo za Luqman itapatikana jamii itakayokuwa mnara wa kuongoza utamaduni wa ulimwengu. Yeye anamfunza mwanawe kwamba dhulma, dharau, ubaguzi na kujikweza pamoja na kufumbia macho maovu ndiyo chanzo cha matatizo ya kijamii.

Na Luqman alimwambia mwanae wakati akimfunza. Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Hakika shirki ndiyo dhulma kubwa. (31:13). Ewe mwanangu! Hakika jambo lolote lijapokuwa na uzito wa chembe ndogo sana, likawa ndani ya jabali au mbinguni au katika ardhi, Mwenyezi Mungu humlipa mfanyaji. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyofichikana, yaliyodhahiri. (31:16).

Ipo kasumba ya binadamu kujikweza na kutothamini kazi za wengine. Kwa kasumba hiyo, tofauti za rangi, kabila, taifa na dini hufanywa vya kutoa haki za wanadamu. Hali hii inajenga tabia ya kutowakabili madhalimu kwa kuendeleza uwenzetu.

Ndipo Luqman anatahadharisha kuwa madhara ya kufumbia macho dhulma ni makubwa kuliko manufaa binafsi. Ewe Mwanangu! Simamisha sala, na uamrishe mema na ukataze mabaya na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni mambo ya kuazimiwa. (31:17).

Ipo dhulma inayotendeka nchini. Kitendo cha kuuwa kwa mawe au kumwasha mtu moto kwa tuhuma za ukwapuzi ni dhulma kubwa. Wananchi wenye hasira wamejipa uhakimu wa vichochoroni. Hivyo atakayehisiwa kuiba kuku, viatu au vijisenti huteketezwa kwa mawe na moto. Inashangaza tabia chafu ya zinaa inayoharibu jamii ambayo ingepaswa kuchukuliwa hatua kali zaidi na wananchi wenye hasira ndio kwanza inapewa baraka zote tangu na wananchi wenyewe hadi serikali ambayo imeamua bila ya haya kuweka "vitendea kazi vyake" madukani.

Kuiba ni jambo baya lakini aliyeiba machungwa au hata ndoo ya maji, ni dhulma kumuhukumu kifo, ni dhambi kumuhukumu aliyeiba ndizi au pesa za kumwona mama ntilie, wizi si tabia ya kuzaliwa nayo. Ni tabia anayojifunza mtu kutokana na msukumo wa mazingira. Ni dhahiri kuwa, katika jamii ambayo viongozi wake ni wabinafsi na wanathibitisha vitendo vya ubadhilifu wa mali ya umma, kumchoma mwizi ni dhulma.

Ni wajibu wa wananchi kuzielekeza hasira na nguvu zao kuuvua madaraka uongozi mbovu ulioshindwa kuwajibika. Wawachome moto vigogo wanaowaibia wananchi waliokamata uwaziri na Urais. Hiyo ndiyo hatua ya kwanza na ya msingi inayoondoa mzizi wa tatizo, lisipofanyika hilo inamaanisha kuwa wizi, ujambazi na aina yoyote ya ukwapuzi utakuwa umesababishwa na wananchi wenyewe.

Woga na ujasiri ni katika maumbile ya binadamu. Sambamba na hilo, binadamu hujithamini, hususan maisha yake. Ndiyo maana penye kifo mtu huweza kusamehe mamilioni kwa maslahi ya uhai wake. Ni vipi tena mtu akhiyari kupigwa mawe au kuchomwa moto kwa kutaka mlo wa siku mbili, ni lazima tujiulize.

Kabla ya kuokota jiwe, rungu au kummwagia kibaka mafuta, ni vyema ukajiuliza, kuwa umefanya jitihada gani kuhakikisha kuwa viongozi dhulma wanaondoka madarakani? Ukiwa Muislamu umefanya nini kuhakikisha kuwa zaka inawapa wanaostahiki uwezo wa kujiajiri.

Akiwajibika kwa Mola wake, mzazi, Luqman anamwelimisha mwanae jukumu la kuamrisha mema na kukataza maovu. Ni rahisi kumpopoa mawe kibaka. Lakini, kupambana na viongozi wanaofuja mali ya umma kunahitaji subira na moyo wa ziada. Wao wana nguvu za dola. Ndiyo maana Luqman anasisitiza kuwa, kupigania haki ni jambo la kuazimiwa kwa subira kubwa.

Aina ya mwisho ya mwalimu ni yule anayepatikana kupitia mafunzo maalum. Waalimu hawa ni tofauti na Utume. Wanapatikana kupitia mafunzo ya saikolojia ya elimu. Hujifunza mbinu na njia za kufundishia. Pamoja na mambo mengine hujifunza taratibu za uongozi na namna ya kupima na kutathmini ufikiwaji wa malengo ya ufundishaji.

Ulimwengu kama ulivyo, una chungu ya hazina ya mambo anayotakiwa mwanadamu kuyasoma na kuyagundua kwa manufaa yake. Masomo ya ulimwengu yamejitega kwa namna ya kuichokoza akili ya mwanadamu ajishughulishe kung'amua na kuwepo kwake.

Mwalimu ni mlezi anayeviongoza vipawa vya mwanafunzi vikue katika kujifunza. Kazi yake ni kuwasaidia wanafunzi kujipatia ujuzi, kurekebisha na kuboresha mienendo yao. Mitalaa mingi inayotumika ina upofu wa mwekeleo. Inamuongoza mwalimu kufundisha kwa mtazamo finyu.

Mwalimu ana jukumu kubwa sana. Kuwaandaa wakulima, madaktari, wachumi, wahandisi, wanasheria, makamanda, waandishi, wanafalsafa, wanasayansi na wanasiasa wacha Mungu. Kuwaandaa wataalamu watakaoshughulika kwa kuzingatia mipaka ya Mwenyezi Mungu.

Yawezekana mwanafunzi kuwa mweledi wa masomo kama vile historia, jiografia na masomo mengine ya sayansi, akaishia kujua kanuni na matukio ya kihistoria bila kupata mafunzo. Kazi ya mwalimu ni kumwelekeza aone uhusiano uliopo baina ya binadamu, ulimwengu na yule aliyeanzisha uhai.

Kupitia masomo na uongozi wa mwalimu, mwanafunzi aelewe asili yake, hadhi na lengo la maisha yake hapa ulimwenguni. Aweze kujenga uchumi, siasa na utamaduni utakaomfanya aishi ndani ya mipaka iliyowekwa na Muumba.

Na masomo mangapi yanadhihirishwa mbinguni na ardhini wanayapata bila ya kuyazingatia (12:105). Na katika watu na wanyama wanaotambaa na wanyama wengine, pia rangi zao ni mbalimbali. Kwa hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu.

Muhtasari wa maneno ni kuwa, kuna walimu wa aina nne. Mwenyezi Mungu ni wa kwanza wao. Kisha hufuatia Mitume walioteuliwa. Wao si wana dini tu, bali ni walimu wa harakati za kuipindua mifumo ya dhulma. Wazazi kama Luqman hufanya aina ya tatu, na mwisho ni walimu wa kuandaliwa.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook