Kwani alitegemea raia wa nchi gani ajiunge na vyama vya upinzani?
Ndugu Mhariri
Naomba nami nitoe mchango wangu kwa wananchi kote lisomwapo gazeti hili.
Ninavyofahamu mimi serikali imekubali mfumo wa vyama vingi kama zilivyokubali nchi nyingi ulimwenguni. Lakini kinachonishangaza mimi ni kwamba serikali ilitegemea raia wa nchi gani aanzishe vyama hivyo na raia wa nchi ajiunge na vyama hivyo?
Je, raia wa Kenya, Uganda au Tanzania? Kama ni Tanzania, je inakuwaje mwananchi huyo abughudhiwe kwa sababu tu amejiunga na chama cha upinzani au kwanini ionekane dhambi kwa kiongozi kuonyesha upinzani wa kweli na kuwaeleza wananchi ukweli ulivyo.
Kama lengo lilikuwa kuanzisha vyama hewa ili kuudanganya ulimwengu basi hilo limeshindikana, upinzani wa kweli upo tofauti na ilivyotegemewa na tayari wananchi wameshaona vyama vyenye upinzani wakweli.
Kama ni propaganda zimeshapandikizwa vya kutosha. Suala la Jino kwa jino sasa halina nguvu. Pili suala la udini nalo pia halina nguvu. Wananchi yote wameyapuuza wameshika kamba moja bila kuachia. Sasa kilichobaki ni nguvu ya dola. Naomba serikali itoe haki sawa kwa raia wote.
Dossi Z. Dossi,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi katika gazeti lako ili niweze kumuweka sawa mwandishi wa Makala iliyolenga kumsafisha Rais Mkapa dhidi ya kushiriki kwake katika kuivunja jumuiya ya Waislamu ya Afrika Mashariki (EAMWS) iliyoandikwa katika gazeti moja la Septemba 17, 2000 pamoja na wananchi kwa ujumla.
Nimeamua kutumia gazeti lako (AN-NUUR) kwa kuwa mwandishi wa makala amelishutumu vikali kwa kuchapisha muswada huo unaoandikwa na mwanahistoria maarufu Mohamed Said.
Mwandishi wa makala hiyo iliyosomwa pia katika kipindi cha 'Uchaguzi elfu mbili' cha redio UHURU (Alhaj Haruna) ameshindwa kabisa kuthibitisha kuwa Rais Mkapa hakushiriki kuivunja EAMWS.
Nilitarajia mwandishi katika kujibu hoja angesema wakati EAMWS inavunjwa Mkapa hakuwa Mhariri wa magazeti ya TANU na Nationalist, au alikuwa Mhariri lakini magazeti yote hayo hayakuchochea kuvunjwa kwa EAMWS, lakini yote hayo hakuyakanusha.
Mwandishi anasema Mkapa hakuwa Bukoba ambako mpika 'majungu' aliibukia, hivi mwandishi anataka kutwambia magazeti yaliyoko jijini Dar es Salaam hayawezi kuleta uchochezi sehemu nyingine ya nchi?
Mwandishi anatutaka tusahau historia ya yale aliyoyatenda Mkapa na badala yake tumpime kwa 'uadilifu na uchapakazi wake' aliouonesha ndani ya miaka mitano!
Hata tukimpima katika miaka hiyo bado Rais Mkapa tunamkuta anaendesha mapambano dhidi ya Waislamu.
Mfano ameendelea kuibeba BAKWATA kama chombo pekee cha Waislamu huku akifahamu BAKWATA haipo kwa idhini ya Waislamu na kuna jumuiya nyingine zenye hadhi sawa na BAKWATA lakini hazipewi hadhi hiyo.
Polisi wamewapiga risasi hadharani na kuwaua Waislamu wanne kama nguruwe au swala (hata nao huombewa kibali kabla ya kuwindwa).
Na amekataa kufanyika uchunguzi juu ya kadhia hii.
Hayo ni baada ya kuwadhalilisha mama zetu kwa kuwavua hijabu na kuwapekua sehemu za siri?
Kisha Mwandishi (Alhaj Haruna(?) anatutaka tuyasahau yote haya! Hivi kama waliofanyiwa haya wangekuwa mama yake, mke wake na watoto wake angethubutu kupigia kampeni CCM na Mkapa?
Nilichogundua ni kuwa, mwandishi haifahamu historia ya Tanganyika (Tanzania) au anaifahamu lakini 'mkate' wa CCM unamfanya ashindwe kuwa mkweli. Siku zote kweli itasimama, muacheni Mkapa ajibu kuwa si kweli na atoe ushahidi.
Hamza Japhary,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |