Uchunguzi ufanywe kuhusu shahada hizi
JUZI limetokea tukio ambalo laelekea kutishia hali ya uchaguzi kuwa huru na wa haki.
Watu kutoka vyama vya TLP, CUF na NCCR walivamia ofisi moja baada ya kupatikana habari kuwa palikuwa na zeozi la kugawa shahada za kupigia kura.
Habari zinaeleza kuwa shahada kadhaa na vitabu vya shahada vilivyojazwa majina vilikutwa katika ofisi hiyo.
Aidha, baadhi ya watu waliokamatwa katika eneo la tukio walidai kupewa jukumu la kutafuta wenzao ambao nao watagawa shahada hizo.
Pamoja na tukio hilo kuripotiwa katika vyombo vya usalama, haielekei kupewa uzito wowote.
Imedaiwa kuwa watuhumiwa waliachiwa pamoja na shahada zao.
Haijulikani kama tukio hilo ni pekee au yamekuwa yakifanyika katika maeneo mengine.
Aidha, haijulikani ni shahada ngapi za aina hiyo zishagawiwa kwa wananchi sehemu mbalimbali nchini na ngapi bado zinasubiri kugawiwa.
Yawezekana wanaodaiwa kupewa shahada hizo ni katika wale ambao hawakuwahi kujiandikisha au hata ambao tayari wana shahada zao.
Lakini swali ni je, wanaodaiwa kupewa shahada hizi, wanaingia katika hesabu ipi?
Je, walishaingizwa katika hesabu iliyokwishatolewa na TUME ya Uchaguzi au watajaongezwa baadae?
Ama lisilo na utata ni juu ya nani wanapewa shahada hizo na kwa maslahi ya nani.
Wanaotuhumiwa kutoa shahada hizo ni wana CCM na haiwezi kuwa kwa lengo lingine bali kwa kukiwezesha chama chao kipate ushindi vyovyote iwavyo.
Katika masiku ya hivi karibuni Makamu wa Rais Dk. Omar Ali Juma amewahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa hata kama baadhi ya watu hawataipigia CCM kura, bado itashinda tu. Aidha, Rais Mkapa mwenyewe aliwahi kusema kuwa atafanya kila awezalo kuipatia ushindi CCM.
Katika mazingira kama haya, tunadhani ni busara tukio la Mwanza kuchunguzwa haraka ili kupata ukweli wa kilichotokea.
Kinyume cha hivyo wasiwasi utazidi kujengeka kwamba huenda pasiwe na uchaguzi huru na wa haki bali kiini macho tu cha uchaguzi.
Wananchi wana haki ya kupata maelezo kutoka vyombo vya dola vilivyopelekewa suala hili pamoja na Tume ya Uchaguzi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |