WAKAZI wa eneo la Mdaula wilaya ya Bagamoyo
mkoani Pwani wamewashutumu vikali viongozi wa mbio za mwenge kuifanyia
kampeni CCM na kuwahofisha wananchi kujihusisha na vyama vingine vya siasa.
Wakiongea na gazeti hili hivi karibuni wamesema, uongo waliokuwa wanautumia viongozi wa serikali kutaka wananchi washiriki mbio za mwenge huo kwa madai si wa CCM umebainika na kuamua kukipa mkono wa kwaheri chama hicho kutokana na tabia yake ya ulaghai.
"Jioni wametuwekea hotuba za kampeni za Mkapa kwenye video ambazo zilifanywa na hayati Mwalimu Nyerere 1995 zilizooneshwa sambamba na picha za Rwanda na Burundi huku muongozaji akitutahadharisha tusichague wapinzani", amesema Bw. Ramadhani Ally.
Awali, wakazi hao walidai viongozi wa mbio za mwenge waliwauliza wananchi maswali ambayo wamesema walikuwa wameyapanga na makada wa CCM, "Mbunge wenu nani?... Kikwete, Rais wenu nani?... Mkapa, basi tuendelee hivyo hivyo ili tumuenzi Baba wa Taifa".
Aidha, wamedai kuhuzunishwa na kitendo kingine cha kampeni kilichofanywa na viongozi hao kuweka jiwe la msingi katika zahanati ambayo haijaisha na wala haitegemewi kukamilika hivi karibuni.
"Hawa viongozi wanatuhuzunisha sana, sisi miaka yote hii hatuna zahanati na tukiumwa kutibiwa mpaka usafiri Chalinze, leo wanatudanganya kuweka jiwe la msingi kwenye zahanati hewa ili tuwape kura", alilalamika Bw. Bakari Ramadhani Fundi.
Pia wakazi hao wameonesha kuchukizwa na mgombea ubunge wa jimbo la Chalinze (CCM) Mhe. Jakaya Kikwete juu ya suala la maji ambapo wanadai huyapata kutoka kwenye lambo kupitia mabombani mara moja kwa wiki tena kwa masaa yasiyozidi mawili.
"Kwa kushabikiwa na makada wa CCM, Kikwete kwenye kampeni zake kwa kutumia lugha ya Kikwete anawauliza "mazi mong'wa, nao wanajibu chong'wa", akimaanisha maji mnakunywa nao wanajibu wanakunywa", alisema mzee Khalid Hamisi aliyeonesha kuchukizwa na hali ile.
Walisema kwa kipindi alichokaa madarakani na kushika nafasi mbalimbali za juu serikalini hakupaswa mgombea huyo kufurahia wakazi wake kunywa maji machafu na kukosa huduma muhimu za afya, elimu na uchumi.
Mwandishi wa habari hizi aliyetembelea kijiji cha Mdaula aliwashuhudia kinamama na watoto wakiwa wameweka foleni za mawe, madebe mabovu pamoja na ndoo za bati na plastiki wakisubiri maji yatoke kati ya majira ya saa 8:00 na saa 10.00 jioni.
Uchunguzi uliofanywa na AN-NUUR umebaini kuwa licha ya maji hayo kuwa machafu kutokana na kuwepo kwenye lambo, wananchi hao hulazimika kuyanunua shilingi 20 kwa ndoo moja ambapo fedha hizo zinadaiwa kwenda kwenye mfuko wa maendeleo ya kijiji.
"LICHA ya kuweka shabu ili maji angalau yawe meupe lakini ukweli unabaki pale pale kuwa maji tunayokunywa kutoka kwenye lambo ni machafu yanayotusababishia magonjwa ambayo tunashindwa kujitibu kutokana na kukosekana hospitali na fedha".
Hiyo ni kauli iliyotolewa na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ubena - Zomozi kilichopo wilaya ya Bagamoyo wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wiki iliyopita.
Akiongea kwa niaba ya wenzake, Bw. Andrew Said amesema viongozi wao wanawalazimisha waizoee hali hiyo na waione kama ni ya kawaida.
Mbali ya kijiji hicho kukumbwa na tatizo la maji na hospitali pia wanadai kukabiliwa na kukosekana ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo ambacho ndio tegemeo kwa wakazi wa eneo hilo.
"Kutokana na kukosekana ajira tukafikiria tuingie kwenye kilimo lakini sasa hapa tulipo tupo katikati na maeneo yote yamechukuliwa na wazungu, waarabu, magereza na jeshi la wananchi Kizuka", alisema Bw. Said huku akiungwa mkono na wananchi wenzake waliokuwa wakiongezeka kila dakika ili kuelezea kilio chao.
Akijibu madai ya wananchi hao, Diwani wa kata hiyo Bw. Ahmed Salum Mwinjuma (CCM) amekiri kuwepo matatizo hayo likiwemo la maji na kudai halmashauri ya Bagamoyo iliwahi kuchimba kisima miaka minne iliyopita ambapo maji yake yalishindikana kutumiwa ipasavyo kutokana na kuwa na chumvi nyingi na hivi sasa kisima hicho kimekauka.
Amesema, katika kata yake yenye vijiji sita wamefanikiwa kuweka malambo katika vijiji vinne vya Ubena-Zomozi, Matuli, Mwidu, Tuka na Visasa. Pia amevitaja vijiji ambavyo havina lambo kuwa ni Kaloleni na Visakasi ambapo wanatumia maji ya bwawa la mto Ngerengere.
"Hapa kwetu Bwana haiwezekani kuchimba visima kwa vile maji yapo mbali na yakipatikana yanakuwa na chumvi nyingi na kuwafanya wengi washindwe kuyatumia kwa mahitaji yao ya muhimu", alisema Diwani huyo ambaye anaingia tena kwenye kinyang'anyiro cha nafasi hiyo.
Aidha, Diwani huyo alikiri kukosekana ardhi ya kutosha kwa wakazi wa Ubena na kudai kuwa mwaka huu wakazi wa eneo hilo mbali ya kulima maeneo madogo pia hawakupata chakula kutokana na mvua kukatika mapema.
Akizungumzia elimu katika kata hiyo, Diwani huyo amesema, shule nyingi bado hazitoi wanafunzi waliofaulu na sababu kubwa amedai kuwa walimu wengi waliokuwepo katika shule hizo wana taaluma za chini (UPE).
Hata hivyo amesema kata yake inategemea shule
moja tu ya sekondari ya Magereza ambayo inatoa kipaumbele kuelimisha maaskari
na wanafunzi wachache wanaofaulu katika shule za msingi.
ZAIDI ya vijana 20 waliokuwa wanachama wa CCM tawi la Mwembeni Mdaula wameamua kukihama chama hicho na kuingia CUF baada ya Mwenyekiti wa serikali ya kijiji (CCM) Bw. Mwakawema kuwapelekea polisi kwa kuwatuhumu wahalifu.
Mmoja wa vijana hao Bw. Bakar Ramadhani amesema mpaka sasa hivi leo kaka yake aliyemtaja kwa jina la Hussein Ramadhani "Milo" yuko mahabusu Chalinze kwa kusingiziwa ujambazi baada ya kushusha bendera ya CCM na kusema hawakitaki chama hicho.
"Siku hiyo polisi walifika mchana kwenye tawi letu la Mwembeni na kuanza kuwapiga bakora vijana wote, waliokuwepo na kuwapeleka polisi Chalinze ambapo baada ya kuwapora fedha walizokuwa nazo wakaawaachia", alidai na kuongeza kuwa waliporudi wakaamua waiondoe bendera ya CCM kwa kuwa haiwasaidii.
Ameendelea kueleza kijana huyo kuwa kitendo cha kushusha bendera ya CCM mchana kilimuudhi sana Mwenyekiti wa serikali ya kijiji Bw. Mwakawema ambaye alikimbilia polisi kufungua kesi.
Amesema, usiku askari walifika nyumbani kwao wakamkamata kaka yake wakimtuhumu kuwa ni jambazi na kumuweka rumande.
"Tulisubiri Lipumba apite hapa kutoka Morogoro
tumkabidhi kadi za CCM na atupatie za CUF lakini kwa bahati mbaya alipita
usiku sana, hata hivyo sisi na chama hicho (CCM), basi vyovyote iwavyo",
amesema.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |