Tatu, mwalimu anapaswa kulielewa vyema lengo la maisha hapa duniani. Kupitia masomo, mwalimu husaidia wanafunzi kupata maarifa mapya yanayowawezesha kujenga dhima ya mambo mbalimbali ya kimaisha. Wakiwa katika ujengaji huo wa dhana, wanafunzi wana haki ya kupewa vigezo vya kupimia mambo.
Usahihi wa vigezo vya kupimia dhana zinazowakilisha matendo na maneno katika maisha unategemea ujuzi wa mwalimu katika kulielewa lengo la maisha. Lengo la maisha ya mwanadamu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu. Mwalimu anayelitambua lengo hili kuwapatia wanafunzi stadi na mwelekeo wa kusimamisha ufalme wa Mwenyezi Mungu duniani.
Haiwi kwa ambaye Mwenyezi Mungu amempa kitabu na hukumu na unabii, asema kuwaambia watu: "Kuweni wenye kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu, bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu (3:79). Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu. (51:56).
Kumwabudu Mwenyezi Mungu ni kufanya jambo kwa kutaraji radhi zake. Kutumai radhi za Muumba ndiyo dira ya jitihada zote za mwalimu na mwanafunzi.
Huu ndiyo muhimili utakaomfanya mwalimu kuwa muadilifu wakati wote. Mwalimu anayelifahamu vyema lengo la maisha huwa makini katika kusema na kutenda mambo. Kauli na matendo yake kuwa kigezo bora katika kulifikia lengo.
Kinyume chake, mwalimu asiyelifahamu lengo halisi la maisha huwajenga wanafunzi mtazamo wa kinyama katika kuyaendea maisha. Kwamba lengo la maisha ni kustarehe katika kutosheleza matashi ya kinyama. Kufanikiwa kwa mtu hupimwa kwa mali aliyonayo bila ya kuangalia njia za upatikanaji wake.
Kwa mtazamo huu, wahitimu wa viwango mbalimbali vya masomo huwa na mtazamo wa kibinafsi zaidi kuliko hata ule wa wanyama. Wanapokabidhiwa nyadhifa za kiserikali, hawawi watumishi wanaojali maadili ya kazi. Hata kma wataapishwa, viapo havitakuwa na athari za kiutendaji.
Mathalan, tumewashuhudia viongozi wa serikali ya awamu ya tatu wakila kiapo kuwa wataongoza kwa haki na uadilifu kama inavyoainishwa kwenye katiba ya nchi. Wakiahidi kutobagua au kumpendelea mtu kwa misingi ya rangi, kabila, chama au dini.
Baada ya viapo ikadaiwa kuwa awamu ya tatu ni awamu ya ukweli na uwazi. Walakini, ukweli na uwazi umegeuzwa kuwa hadaa na dhulma dhidi ya Waislamu wa Tanzania. Uwazi unaonyesha kuwa Waislamu wameuawa pasipo haki na ukweli uko wazi kuwa Paroko Lwambano ndiye aliyechochea!
Yote hayo hayazingatiwi, wakiongozwa na Rais, watumishi wa serikali hawaoneshi kama kuna haki za kikatiba zinazowahusu Waislamu. Mpaka leo, wauaji wako huru wana'tesa' na kutanua maisha. Msimamo huu wa kibinafsi na maslahi yake ni ya muda mfupi, tena ni kwa kikundi cha watu wachache. Si kwa maslahi ya taifa.
Ni dhahiri kuwa mwanafunzi ambaye ni zao la mwalimu asiyefahamu lengo la maisha, hategemewi kuwa kiongozi mwadilifu. Atakachojali ni maslahi binafsi au kama atazidisha basi ni kwa kikundi cha waliokaribu naye, wanaomuhusu. Viongozi waadilifu hutokana na wanafunzi waliojengwa mwelekeo wa lengo halisi la maisha, wakizingatia kuwepo kwa Muumba.
Mwaka 1998, Wizara ya Elimu na Utamaduni ililazimika kufuta mitihani ya kidato cha nne. Uamuzi huo ulitolewa baada ya kubainika kuwa mitihani imevujishwa. Hivyo, ikabidi serikali igharamike upya. Tukio hili linathibitisha kuwepo kwa mtandao wa hongo na rushwa unaosukumwa na utashi wa ubinafsi kuliko manufaa ya jamii.
Kutengemaa kwa jamii kunategemea malezi bora hususan kuimarisha mioyo ya wanafunzi iwe hadhiri na uwepo wa Mwenyezi Mungu. Wahitimu hawa watawajibika ipasavyo, wataweza kuondoa kero zote za kijamii. Kwa kutaraji radhi za Muumba, hawatokubali kusalitiwa kama raia au kuwasaliti raia wakiwa viongozi.
Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha haki kwa ajili ya Mwenyezi Mungu muwe mashahidi wa uadilifu. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutowafanyia uadilifu. Fanyeni uadilifu hiyo ndiyo njia ya kufikia kilele cha ucha Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda. (5:8)
Mwalimu kulijua vyema lengo la maisha ni sifa muhimu sana. Ataweza kuwatayarisha wanafunzi watakaokuwa makhalifa wa Mwenyezi Mungu hapa ulimwenguni ndio watakaobadilisha dhulma na umwagaji wa damu uliotapakaa duniani, kuwa haki, uadilifu na amani ya kweli. Ikiwa mwalimu hana sifa hii, matokeo yake ni kuwa na jamii yenye raia na viongozi mafasiki.
Sifa ya nne, ni mwalimu kuzijua mbinu na njia za kufundisha. Kuwa na ujuzi wa somo na lengo la maisha kutakuwa na manufaa zaidi ikiwa mwalimu anazifahamu kinadharia na kimatumizi, njia na mbinu za kuurithisha ujuzi alionao. Kupitia mbinu na njia, mwalimu ataweza kuweka mkakati utakaomtoa mwanafunzi kwenye ujinga na kutojua na kumfikisha kwenye ujuzi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |