KATIBU wa tawi la CCM la shule ya sekondari ya Popatlal ya mjini Tanga, Bw. Rashid Mavumba amerudisha kadi yake pamoja na baiskeli yake ya Ukatibu na kuvikabidhi kwa viongozi wa Chama cha CUF katika mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika wiki iliyopita katika kata ya Makorora.
Bw. Mavumba ni miongoni mwa wanachama 31 wa CCM ambao wamerudisha kadi zao katika mikutano ya hivi karibuni ya chama hicho iliyofanyika katika kata mbalimbali za Manispaa ya Tanga.
Miongoni mwa wananchi waliorudisha kadi hizo ni balozi wa CCM wa mtaa Bw. Mohamed Mwaheri ambaye alirudisha kadi yake katika mkutano wa chama hicho uliofanyika kata ya Mwahako.
Jumla ya kadi 41 za vyama mbalimbali zimerudishwa kwa viongozi wa CUF katika mikutano hiyo zikiwemo kadi 8 za NCCR Mageuzi na 2 za TLP.
Wakati huo huo, imeelezwa kuwa amani na utulivu wa nchi ni hupatikana kwa huduma bora za jamii na nchi kuondokana na umaskini.
Kauli hiyo ilitolewa na mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Bw. Rashid Jumbe katika mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika eneo la Madina mwishoni mwa wiki iliyopita.
Bw. Jumbe alikuwa akijibu madai ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wanaodai kuwa chama hicho kimeleta amani na utulivu.
"CCM wanataka wachaguliwe tena eti kwa sababu wameleta amani na utulivu. Amani na utulivu katika nchi ni kuondokana na umaskini", alisema.
Amesema, vitendo vya uhalifu ukiwemo ujambazi ambao ulisababisha hadi hivi majuzi mkuu wa mkoa wa Dodoma na viongozi wengine kutekwa na majambazi unaonesha kuwa nchi hii si ya amani na utulivu.
Bw. Jumbe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa vijana Taifa alilikosoa zoezi zima la kupunguza watu makazini na kueleza kuwa litachangia kuongezeka kwa uhalifu na nchi kuzidi kukosa amani.
Amewataka wana CCM kuwa waungwana kwa kukiri kuwa wameiingiza nchi katika umaskini na kwamba amani na utulivu havipo.
Naye Katibu wa chama hicho wilaya ya Muheza, Bw.
Abdulrahmani Hassan akizungumza katika mkutano huo alisema, endapo wananchi
watakichagua chama hicho kitaunda serikali adilifu, itakayojenga uchumi
ulio imara.
CHAMA cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi vimefanya 'mauaji makubwa' baada ya kuzoa wanachama wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Kikole.
Hatua hiyo inafuatia kwa vyama hivyo kufanya mikutano yake ya kampeni kuwanadi wagombea wake Ubunge na Madiwani katika jimbo la Kilwa Kusini hivi karibuni.
Mgombea Ubunge kupitia chama cha CUF, Bwana Mwichande Kalyoma amesema kuwa umaskini walionao wilaya hiyo siyo laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bali ni mipango iliyokuwa imepangwa kwa makusudi na viongozi wa Chama tawala (CCM). "Wananchi wenzangu wa Kilwa umaskini wetu ni wa kupangwa kwa makusudi na viongozi waliopo madarakani, siyo laana ya Mungu", alisema Kalyoma.
Kalyoma amesema kuwa Kilwa ina utajiri mkubwa sana, lakini utajiri huo unawanufaisha wachache na kuwafanya walio wengi kubaki maskini na kuwafanya wazazi kushindwa hata kuwasomesha watoto wao.
Amesema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo la Kilwa Kusini atahakikisha anashirikiana na wananchi wakiwemo na Wabunge wa mikoa ya kusini kupinga gesi kwenda kusafishwa Dar es Salaam na badala yake uzalishwe umeme ndani ya mkoa huo ili wao wanufaike na raslimali iliyotokana ndani ya mkoa wao.
Kwa upande wa wakulima na wavuvi, Kalyoma amesema kuwa atahakikisha wataalamu waliopo wilayani humo wanakuwa karibu zaidi na wananchi badala ya kushinda maofisini pekee. "Nitahakikisha wataalamu wa kilimo na uvuvi hawakai maofisini kama walivyokuwa sasa, wote watakuwa mashambani kuwaelekeza wakulima kilimo cha kisasa", alisema Kalyoma.
Katika kampeni hizo wanachama kadhaa wa CCM kutoka vijiji vya Migeregere, Ruhatwe na Kikole katika kata hiyo ya Kikole walirudisha kadi za CCM , NCCR na TLP na kujiunga na vyama hivyo vya CUF na CHADEMA na kuwaacha viongozi wa CCM pekee, wakiwa na bendera zao.
WANACHAMA wengine wawili wa Chama cha Wananchi (CUF) wilayani Kilwa mkoa wa Lindi, Hamisi Salumu Mwichande na Abubakar Kama Ally wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na kosa la kujenga kikuta cha wakereketwa kwenye eneo linalodaiwa kuwa ni la mtu binafsi.
Akiwasomea shitaka lao mbele ya Hakimu Said Mbung'o wa mahakama ya mwanzo ya Kivinje, Askari polisi No. 8734 Godwin Kolimba alidai kuwa wanachama hao wamejenga kikuta hicho kwenye eneo la Bwana Hamisi Yasini lililopo kijiji cha Singino bila ya ridhaa yake.
Washitakiwa wote wamekana shitaka na wapo nje kwa dhamana ya shilingi 10,000 kila mmoja hadi Oktoba 10 mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena.
Hii ni kesi ya tatu kuwakabili wanachama wa chama hicho, kwani mwezi Julai mwaka huu, wanachama wanane wa mjini masoko wanakabiliwa na kesi ya kuonyesha video ya mikutano ya Profesa Lipumba bila ya kibali.
Mwezi Agosti wanachama watano wa mji Mkongwe wa Kivinje akiwemo Mwenyekiti wake Bwana Selemani S. Bungara wana kesi wakidaiwa kumfanyia fujo mkuu wa Wilaya hiyo Bwana Wilfred Ligubi.
Wakizungumza mara baada ya kutoka mahakamani, Bw. Ally amesema kuwa ameshangaa na madai yaliyotolewa na mlalamikaji Bwana Yasini kuwa eneo hilo ni la kwake, jambo alilolielezea kuwa si la kweli.
"Eneo tulilojenga kikuta hicho ni eneo la wazi ambalo tayari walishapewa na kampuni ya TANESCO na MECCO, sasa eneo lake yeye lipo wapi?" alihoji kwa mshangao Ally.
Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa imekuwa ni desturi kwa wazee wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanapoona CUF inakuwa na nguvu wao huzusha visa ambapo hatima yake huangukia polisi na hatimaye mahakamani.
Akiungwa mkono na mwanachama mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Zally yeye alisema kuwa hata kama watapelekwa wote jela katu hawatahama chama hicho.
"Sisi tunajua hii ni mbinu za kutaka kuturudisha nyuma ili wapinzani tusiwe na nguvu, lakini tunasema katu haturudi nyuma hadi kufa", alisema Bi. Zally.
Chama cha Wananchi (CUF) tangu kionekane kuwa
ni tishio kimekuwa kikikubwa na migogoro mingi hasa kwa wanachama wake
kutiwa ndani ikiwemo na kufikishwa mahakamani. ,mpaka sasa jumla ya wanachama
15 wanakabiliwa na kesi wilayani Kilwa pekee.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |