"KILA kitu na wakati wake. Wakati wa CCM umekwisha".
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na mgombea Ubunge wa jimbo la Ilala kwa tiketi ya CUF na CHADEMA, Mhe. Ahmed Omar Mnyanga alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Misheni Kota kwenye mkutano wa kampeni.
Mhe. Mnyanga aliwataka wakazi wa jimbo la Ilala kunusuru uchumi wa nchi uliodidimia kwa uleta mabadiliko ya kisiasa katika ngazi zote za utawala wa nchi.
Mhe. Mnyanga alieleza zaidi kwamba chama cha Wananchi (CUF) na wagombea wake wa ngazi zote ndiyo wenye majawabu ya matatizo ya Watanzania wa leo ambapo uchumi ndiyo siasa:
"Ndiyo! CCM imeleta uhuru wa nchi hii, lakini tatizo la leo la Watanzania siyo kupambana na wakoloni bali kuinua kipato cha wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla", alisema Bw. Mnyanga.
Aliongeza kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) hakina sera wala mwelekeo unaokidhi mahitaji na matakwa ya Watanzania wa leo.
Aidha, mgombea Ubunge huyo aliendelea kusema kwamba watu wasiotaka mabadiliko na wanaong'ang'ania siasa zilizopitwa na wakati za CCM ni kichekesho kwa jamii yenye kujitambua.
Akijibu hoja za CCM kwamba vyama vya upinzani bado vichanga kwa hiyo havina uwezo wa kutawala nchi, Mhe. Mnyanga alikuwa na haya ya kusema:
"Kuna baadhi ya matunda kama matango na bamia yanatakiwa yaliwe yakiwa machanga, yakishakomaa hayaliki. CCM ni bamia iliyokomaa na sisi ni bamia changa".
Awali, akimnadi mgombea Urais kwa tiketi ya CUF na CHADEMA, Prof. Ibrahim Lipumba, mgombea Udiwani wa kata ya Temeke, Mhe. Haji Kinjekitile alisema Prof. Lipumba ndiye Ris anayefaa kwa karne hii.
Aidha, Bw. Kinjekitile alidhihirisha upendeleo wa wazi uliomo ndani ya CCM kwa kutaka kumpa umama wa Taifa mama Maria Nyerere badala ya Bibi Titi Mohammed.
Bw. Kinjekitile aliwakumbusha kwamba Bibi Titi Mohamed ni mwanamke pekee katika miaka ya 50 aliyezunguka nchi nzima akihamasisha wazalendo kupinga ukoloni.
WANAFUNZI wanaosoma shule za sekondari na msingi mjini Masoko wilaya ya Kilwa mkoani Lindi wamewashutumu vikali walimu wao kwa vitendo vya kuwazuia wasiende kuhudhuria mikutano ya vyama vya upinzani na kukiita kitendo hicho ni kuwanyima haki yao kikatiba.
Habari kutoka ndani ya shule hizo zinaeleza kuwa, imekuwa ni desturi kwa wanafunzi hao kunyimwa haki za za msingi ya kuhudhuria mikutano hiyo, na badala yake hutakiwa kwenda ile ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pekee.
Septemba 14, mwaka huu, wanafunzi wanaosoma shule ya msingi na sekondari ya mjini Masoko walizuiliwa kwenda kusikiliza mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) uliokuwa unahutubiwa na mgombea Mwenza, Bwana Nassoro Khamis, na wale ambao walikiuka amri hiyo walipewa adhabu ya kulima shamba la shule na wengine kupigwa viboko.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni huko Kilwa, baadhi ya wanafunzi hao ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini kwa kuhofia usalama wao, walisema kuwa walimu wao wamekuwa na tabia ya kuwazuia kwenda katika mikutano ya wapinzani kwa kisingizio cha kuwapa kazi ilimradi wasipate nafasi ya kutoka shuleni hapo.
"Hawa walimu wetu wana agenda ya siri, mikutano ya CCM hutolewa darasani hata tukiwa katika vipindi vya masomo, lakini mikutano ya wapinzani tunaambiwa tusitoke hata tukiwa hatuna kazi ya kufanya, ilimradi tusitoke tu", walilalamika wanafunzi hao.
Wanafunzi hao waliendelea kusema kuwa inapofanyika mikutano ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hulazimishwa kukatisha masomo yao kwa kuelezwa waende kuhudhuria kusikiliza sera za chama hicho kwani ni haki yao kwa mujibu wa katiba ya nchi.
"Hivi haki hii ya katiba ipo kwenye mikutano ya CCM tu, kwenye mikutano ya mageuzi hapana, tuna wasiwasi na walimu wetu", walisema wanafunzi hao.
Naye mwanafunmzi anayesoma darasa la sita shule ya Msingi Masoko amecharazwa viboko sita na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ally Saidi kwa madai ya kuiimbia kwaya Chama cha CUF kwenye mkutano huo wa kampeni uliokuwa umefanyika Septemba 14, mwaka huu kwenye viwanja vya Miembeni mjini Masoko.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni huko Kilwa Masoko, mwanafunzi huyo amesema ameshangazwa na kitendo hicho na kukiita ni cha uonevu.
Chama cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni kilifanya mkutano wake wa kampeni mjini Masoko, uliokuwa umehutubiwa na Mwenyekiti wake Rais Benjamin Mkapa na kuhudhuriwa na watazamaji wachache wakiwemo na wanafunzi wa shule mbili za msingi na sekondari.
Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Kilwa, Bw. Ally M. Mng'umba alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya shutuma hizo alikanusha kwa kusema kuwa si kweli, na hajawahi kufanya kitu kama hicho.
"Mmimi sijawahi kufanya hivyo kwani ninaelewa demokrasia na kuna wengine washatimia wakati wa kupiga kura hivyo kuwazuia ni kuwanyima haki zao kikatiba", alisema na kuongeza "kipindi cha masomo sijawahi kuwatoa wanafunzi darasani kwenda katika mikutano ya CCM na hayo ni maneno ya uzushi tu", alisema Mwalimu Nng'umba.
Mwandishi wa habari hizi alipotembelea shuleni hapo Septemba 15, mwaka huu aliwakuta wanafunzi hao wakipalilia mashamba yao ya mikorosho huku wengine wakipanga mawe kuzungusha majengo ya shule hiyo.
AKINAMAMA wajawazito katika kata ya Ubena-Zomozi wilayani Bagamoyo hukosa huduma wakati wa kujifungua kutokana eneo hilo kukosa hata zahanati na usafiri wa uhakika.
Hali hiyo hupelekea wakati mwingine akinamama hao kujifungulia njiani wakipelekwa hospitali ya Lugoba.
Hayo yameelezwa Jumamosi iliyopita na Afisa Mtendaji wa kata hiyo Bi Mwanahamisi Mdugwa wakati akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake.
Amesema, mara nyingi kinamama wanakumbwa na hali hiyo kutokana na umbali uliopo kutoka kijijini hapo mpaka Lugoba ambapo wakati mwingine magari yanakuwa yameshapita na kulazimika kutumia machela.
"Hapa wagonjwa wa aina hiyo wanapokaribia kujifungua hususan nyakati za jioni na usiku lazima watazalia njiani kwa vile hakuna mabasi wala magari ya kukodi zaidi ya machela ambazo huwachukua watu zaidi ya masaa matano hadi manane kufika hospitalini", amesema Afisa huyo.
Ameendelea kusema mbali ya kuwapeleka Lugoba pia amedai wagonjwa wengine hulazimika kwenda kutibiwa Chalinze au Morogoro, jambo ambalo amesema wakazi wengi wa eneo hilo hawana uwezo nalo na kuamua kutumia tiba za kienyeji na kupelekea wengine kupoteza maisha.
Bi Mdugwa amesema, katika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo, ofisi yake kwa kushirikiana na Diwani wa kata hiyo inatafuta wahisani ili kununua hospitali ya mtu binafsi iliyoachwa na Bw. Mwitula aliyeshindwa kuiendesha.
Hata hivyo, Afisa huyo amesema, wakazi wa eneo hilo kwa sasa wanasaidiwa kwa kiasi fulani kupata huduma ya afya katika hospitali ya binafsi inayomilikiwa na Bw. Mohamed Mura ambayo ni mahususi kwa ajili ya wafanyakazi wake wa shirika la mkonge.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliohojiwa na gazeti hilo wameonesha kuhuzunishwa na hali hiyo ambayo wamedai inawaweka katika mazingira magumu ya kuishi na kuwatupia lawama viongozi wao akiwemo Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
"Sisi hapa tuna hali ngumu sana kimaisha, kazi yetu ni kuuza maji, ndoo ni shilingi 50, tumejitahidi sana kwa siku tumeuza ndoo 10 hadi 15, ukirudi nyumbani hoi unaumwa, kwa hiyo fedha uliopata yote unawaagizia watu wanaokwenda Chalinze wakununulie dawa", amesema kijana Issa Bakari.
Aidha, wananchi hao wamekema vikali tabia ya viongozi wao kuwanyima nafasi ya kutoa kilio chao kwa viongozi wa juu wa serikali wanaobahatika kupita kijijini hapo na badala yake wenyewe wanatengeneza risala walizodai ni za uongo zenye kuonesha hawana matatizo yoyote.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |