Udini ulivyoathiri utendaji wa Nyerere

KATIKA uchaguzi wa mwaka 1995 katika kumpitisha Mkapa ni vizuri ikaelezwa kuwa katika wagombea wa CCM lilikuwapo jina la Profesa Malima, Muislam pekee katika orodha ya wagombea.

Ili kuweza kulitoa jina la Profesa Malima alihitajika apatikane Muislamu mwingine ili jina lake lichukue nafasi ya jina la Profesa hivyo majina yatakayokwenda mbele kupigiwa kura na Mkutano Mkuu lisiende jina la Malima bali la Muislamu mwingene.

Hatari ya kulipitisha jina la Profesa Malima kwenda Mkutano Mkuu na mathalan pamoja jina la Mkapa na Msuya ni kuwa pangelikuwa na uwezekano wa yeye kupitishwa jina lake na hivyo kugombea nafasi ya urais. Kitu kama hiki ingekuwa ni kwa CCM kujitafutia matatizo.

Mwaka wa 1992 Profesa Malima aliwahi kuangushwa na Mkutano Mkuu alipogombea moja ya nafasi 20 katika Halimashauri ya Kamati Kuu ya CCM katika mkutano wa Chimwaga Dodoma.

Lakini mwaka wa 1995 hali ya siasa ndani ya Tanzania ilikuwa imebadilika sana na Profesa Malima alikuwa kipenzi cha Waislamu. Ilibidi Kikwete aingizwe kwenye kinyang'anyiro dakika za mwisho ili ipatikane fursa ya kuondoa jina la Muislamu Malima kwa kupatikana Muislam "mwingine'.

Halmashauri Kuu ya CCM iliondoa jina la Profesa Malima kama ilivyotegemewa na kupitisha majina ya Kikwete, Mkapa and Msuya kwenda mbele ya Mkutano Mkuu kupigiwa kura ili jina moja la mgombea urais wa Tanzania lipitishwe.

Kabla ya mkutano Kikwete alilalamika kuwa Dr Lawrence Gama Katibu wa CCM alikuwa akihujumu kampeni yake ya kugombea nafasi ya urais kwa misingi ya udini. Hivi ndivyo siasa za Tanzania zilivyo. Muislamu ni Muislamu hata ikiwaje. Gama kama Mkapa alikuwa ni Mkatoliki na walikuwa wanatoka sehemu moja. Nyerere hakufanya lolote kuhusu shutuma zile dhidi ya Gama.

Kwa muda ilielekea kuwa CCM ilikuwa inataka kuingia katika janga kubwa la kumnyanyasa Muislamu anaewania nafasi ya urais. Na Janga lenyewe linawahusu viongozi wa juu kabisa wa CCM.

Mwimbo wa kuwa CCM haina ubaguzi wa dini ni maarufu masikioni mwa wengi. Kuibuka kwa hisia za udini kati ya Mkatoliki Gama na Muislamu Kikwete lilikuwa jambo zito. Hata hivyo CCM ilitoa taarifa kuwa Dk Gama amemtaka radhi Kikwete. Kikwete hadi leo hajasema ni kitu gani alichofanyiwa na Dk Gama hadi ikabidi CCM imuamrishe Gama kuomba radhi.

Katika duru ya mwanzo Kikwete aliongoza kwa kura akifuatiwa na Mkapa na Msuya. Kura ilirudiwa na Mkapa akashinda. Kwa hakika jinsi Kikwete alivyoingia katika uchaguzi wa mwaka 1995 na jinsi Mkapa alivyoingia madarakani ni somo ambalo linahitaji lipewe muda kwa sasa. Wakati wa kulitafiti haujafika. Lakini itoshe kueleza kuwa kulikuwapo na mbinu na mizengwe ya hali ya juu katika kupitisha jina la Mkapa katika Halmashauri Kuu ya CCM.

Nyerere alimfanyia kampeni Mkapa na akachaguliwa kuwa rais wa tatu wa Tanzania. Ushahidi katika utafiti wa kimazingara unaonesha kuwa Nyerere toka mwanzo kabisa alikuwa na mtu ambae alitaka achukue nafasi ya Rais Mwinyi.

Hivi ndivyo Mkapa alivyokuja kuwa rais wa Tanzania na akarithi nchi ambayo Waislamu walikuwa wana manung'uniko ya muda mrefu dhidi ya serikali ya kubaguliwa kwa ajili ya imani yao.

Hayo yote tuliyoeleza hapo juu yatakuwa hayajakamilika hadi tueleze jinsi udini ulivyoathiri utawala wa Nyerere.

Historia ya karibuni na ya wazi ya Nyerere kuchanganya dini na siasa inaanza mwaka 1970. Mwaka 1970 Nyerere alikuwa na mazungumzo Ikulu na Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Kanisa Katoliki (Tanzania Episcopal Conference) Fr. Robert Rweyemamu.

Pamoja nae walikuwa Mwakilishi wa Papa Tanzania Mgr. Giovano Cerrano. Nyerere aliwahakikishia viongozi hawa wa Kanisa Katoliki kuwa yeye atafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa Ukatoliki unakuwa juu Tanzania kwa kuupa upendeleo maalum.

Mwalimu Nyerere alitimiza ahadi yake kwa kwa vitendo. Alipoondoka madarakani waumini hao wa dhehebu moja walikuwa wameihodhi serikali barabara. Katika Bunge la Muungano ambalo lina viti mia na sitini na nane (168) vya Tanzania Bara, Waislamu walikuwa na uwakilishi wa viti arobaini na moja (41). Hii ni sawa na asilimia ishirini na nne nukta nne (24.4%). Viti hamsini na tano vilikuwa vimekaliwa na Wazanzibari ambao wote ni Waislamu.

Katika mawaziri wa serikali wanne (4) tu walikuwa Waislamu. Hii ni sawa na asili mia ishirini na mbili (22%). Katika mawaziri wadogo kumi na mbili (12) wawili tu (2) walikuwa Waislam.

Katika Makatibu Wakuu kumi na tisa (19) watatu tu (3) walikuwa Waislamu. Katika Wakuu wa Mikoa ishirini (20) watano (5) tu walikuwa Waislamu. Hii ni sawa na asili mia ishirini na tano (25%). Katika Wakuu wa Wilaya mia na kumi na nane (118) wanane tu (8) walikuwa Waislamu. Hii ni sawa na asili mia sita (6%). Jambo muhimu na la kuzingatia ni kuwa katika mgao huu wa madaraka Wakatoliki walikuwa wamehodhi asili mia sabini (70%) kati ya asili mia sabini na tano (75%) viti vyote bungeni dhidi ya Waumini wa dini ya kiislamu na waumini wa madhehebu nyingine za Kikristo

Hivi ndivyo ndivyo Nyerere alivyoendesha nchi bila ya udini wala ubaguzi katika serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Matokeo ya hali hiyo ni kuwa na serikali na Bunge lenye lenye chuki, uonevu na ubaguzi dhidi ya waumini wa dini nyingine. Ukisikia Nyerere anasifiwa kuwa alikuwa hana ubaguzi wa dini huu ndiyo urithi wetu Waislamu na kwa Muislamu kuhoji hali hiyo ni 'kuchanganya dini na siasa' au kuleta udini au 'kutopenda amani na utulivu'.

Katika hali kama hii hupatikana Waislamu wakapewa nafasi katika magazeti ya CCM na radio yake kuwalaumu Waislamu wenzao ambao wanajaribu kuiasa serikali kutopuuza madai ya Waislamu. (Angalia: Mzalendo 17 Septemba 2000 ; Vilevile Uhuru 19 Septemba 2000).

Hivi sasa CCM ina kazi kubwa sana ya kujaribu kuiweka vyema historia ya Nyerere iweze kupendeza kwenye masikio ya Waislamu. Kazi hii imekuwa ngumu kweli. Magazeti ya 'mfumo katoliki' yakiandika wema wa Nyerere na 'ubaba wa taifa' na kuwa hakuwa mbaguzi wa dini, Waislamu wanachapisha historia ya Nyerere iliyo kinyume na hivyo.

Hili ndilo jinamizi lililoundwa na chuki ya serikali dhidi ya Waislamu na Uislamu na jinamizi hili ndilo leo linaipa wakati mgumu CCM nchi nzima katika Uchaguzi Mkuu wa 2000.

Katika kujenga chuki hii hakuna aliyesalimika. Nyerere amechangia, Bunge limechangia, serikali imechangia, maaskofu wamechangia na hata Bakwata wamechangia.

Kwa bahati mbaya sana hii leo badala ya CCM kuangalia wapi wamejikwaa ili waondoe kikwazo wanalaumu walipoangukia na kukimbiza upepo huku wakisingizia kuwa chuki dhidi yao inatokana na Waislamu 'kuchanganya dini na siasa'.

Inashangaza sana ni kwa nini CCM haijiulizi huu udini wa Waislamu unaolalamikiwa ulianza lini na nani anambagua nani. Ni kweli Waislamu wanabagua wananchi wenzao kwa ajili ya dini yao? Katika hali hii ya udhalili waliokuwanao Waislamu, kweli wanaweza kuwa na uwezo wa kumbagua mtu? CCM inashindwa kuelewa kwa nini leo takriban zaidi ya miaka arobaini ya kujitawala Waislam bado tunajihesabu tunapigana na ukoloni wa aina mpya na tunadai haki sawa.

Hii sura mpya inayojitokeza Tanzania inapaswa kuwa fundisho kwa nchi za Kiafrika kuwa pale jamii moja itakaponyanyaswa na nyingine kwa misingi yoyote ile, ama ya kabila, dini au nasaba basi wasitegemee chochote ila kuleta mfarakano kwa misingi hiyo hiyo ya ubaguzi. Wanaobaguliwa watatafsiri hisia zao kwa njia tofauti hata kwa mapambano ya wazi.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook