Kama kweli tunataka amani iendelee, basi tuupige vita ubinafsi

UBINAFSI kama ulivyo dhambi na sumu mbaya sana dhidi ya umoja. Katika dini ya Kikristo moja ya mafundisho muhimu katika Injili ya Yesu au Falsafa ya Bwana Yesu ni kwamba mtu akitaka kumfuata Yesu basi kwanza ajikane mwenyewe (aushinde ubinafsi wake) na ajitwishe msalaba wake mwenyewe (yaani ajitwike jukumu kamili katika jamii yake) na amfuate.

SEHEMU nyingine Yesu anasema wazi kwamba mtu aikane nafsi yake. Sasa kwa bahati mbaya ni rahisi sana kuihubiri Injili ya Yesu lakini ni vigumu sana kuitekeleza Injili hiyo kwa vitendo. Ndiyo maana kati ya wahubiri mia waweza kukuta watendaji (ama watekelezaji wa kile wanachokihubiri) ni mmoja au wawili tu.

Walioweza kuushinda ubinafsi ni wachache sana. Ubinafsi unaweza kuwa katika ngazi ya mtu mmoja au katika kundi ama katika taasisi. Mtu anaweza kujikuta anatetea ubinafsi pasipo kujua. Mtu anaweza kujikuta anatetea ubinafsi wa kundi au taasisi huku akijua kwamba anachokitetea siyo ukweli bali ni ubinafsi mtupu.

Mfano hai ni kitabu kilichotolewa hivi karibuni ambacho nia yake ni kuwashawishi wapiga kura wairudishe CCM madarakani. Katika jitihada za kufunika malengo ya kisiasa, na maslahi ya binafsi, kitabu hicho kimepewa jina la "tittle" ya "Amani katika Tanzania italindwa kwa kutenganisha dini na mamlaka ya nchi".

Mwandishi kwa kuficha ubinafsi wake anadai amekitoa kwa niaba ya Halmashauri ya Maaskofu, lakini ndani ya kitabu chake hakutoa orodha ya Maaskofu walioidhinisha maandiko hayo.

Neno Askofu katika dini ya Kikristo na katika jamii ya Tanzania linabeba uzito mkubwa hivyo haitegemewi kweli Maaskofu wenye elimu ya kiroho na elimu ya kidunia na pia wenye mzigo na jamii yaani mzigo wa kuona haki inatendeka katika maisha ya watu, kisha wakakutanika na kutoa tafsiri finyu ya neno dini kwa kusema eti dini ina maana ya itikadi au imani inayohusiana na mambo ya kiroho baina ya binadamu na Mungu. (Mwisho wa kunukuu).

Wajuayo neno itikadi au "ideology" watakiri kwamba "ideology" inatokana na neno "ideas" yaani mawazo au fikra za binadamu kuelekea suala fulani. Sasa dini inapofinyangwa na kushushwa hadi kwenye daraja la ujamaa au socialism, communism, ubaguzi au racialism, ubinadamu au humanism, ubinafsishaji au privasation, utandawazi au globalisation, indegeonisation na kadhalika basi Uaskofu wa watu hao ni wa kutilia shaka.

Lakini kinachoufunua ubinafsi wake na kuukweka wazi zaidi ni ile "content" ya kitabu hicho au yale maandishi yenyewe yaliyomo ndani yake na ujumbe halisi wa kitabu.

Mambo yanayozungumzwa ni yale yale ambayo siku zote yanazungumzwa ama kuandikwa na gazeti la moja litokalo kila jumapili, ambalo linaendeshwa na mtu asiyekubali mawazo ya watu wengine, pia wanaolengwa na kitabu hicho ni wale wale yaani Waislamu.

Mtu yeyote anayeitakia mema nchi hii hawezi kutumia lugha ya kugawa watu kama vile kuanza kuwaita wengineo wao, na wengine sisi ndani ya nchi moja. Hii ni kwa sababu kitu kiitwacho Tanzania, ni mkusanyiko wa watu wa makundi mbalimbali, yaani kutoka kabila mbalimbali, dini mbalimbali, na rangi mbalimbali, na hali tofauti za kiuchumi na maendeleo. Kwa ajili hiyo lugha za kusema wao Waislamu, na sisi Wakrsito hizo ni lugha chafu za kukemea, kwakuwa zinamong'onyoa umoja wa kitaifa na kuchochea mgawanyiko ambao hauna msingi.

Pili kitendo cha watu wajiitao Halmashauri ya Maaskofu wa Kipentekoste kujibu hoja za Waislamu kwa niaba ya serikali inabidi kilaaniwe kwa sababu serikali ina msemaji wake na ndiye anayestahili kujibu kikatibua, kisheria na kisiasa, lawama zote ama maswali yote, au madai yote yanayodaiwa dhidi ya serikali kutoka katika jumuia ya Waislamu na wala siyo watu kimbelembele tena kwa kutumia Biblia.

Mimi ni mfuatiliaji wa madai ya Waislamu tangu miaka ya 1987 hadi sasa 2000, lakini sijaona popote pale ambapo Waislamu wanadai kwamba "Wakristo" wamewanyima haki, ama wamewadhulumu hiki au kile, badala yake wanasema wazi kwamba serikali ya TANU na hatimaye ya CCM ndiyo imewafanyia kadha wa kadha ambayo hawaridhiki nayo.

Kimsingi madai yote ni dhidi ya serikali siyo dhidi ya Wakristo. Hata vurumai za Mwembechai za 1998, hazikugusa kanisa lolote licha ya kwamba jirani kabisa na Msikiti huo wa Mwembechai lipo kanisa la Kristo, kando ya barabara liko kanisa la Sabato, na mkabala wa barabara hiyo ya Morogoro lipo kanisa la Anglikani, mbele yake mita chache kipo kituo cha Kanisa Babtisti.

Sasa kama kweli Waislamu walioamua kuwa "vocal" wana uchungu au donge lolote miongoni mwao dhidi ya Wakristo ilikuwaje wasishambulie makanisa bali magari yenye nembo za serikali tu?

Ukweli ni kwamba wanaidai serikali na kwahiyo hekima ya kimungu ni kuicha serikali ijibu na ijitetee yenyewe na kama itashindwa na wimbi hili basi ni kuiacha CCM ivune ilichokipanda katika miaka 40 ya utawala wake. Vinginevyoj inatia shaka kwamba Maaskofu wa Kipentekoste wana maslahi gani na serikali ya CCM hadi waamue kuwa mawakili wa kuitetea inapodaiwa au kushutumiwa?

Lakini inavyoonesha ni maslahi ya binafsi ya mwandishi ndiyo yanayomsukuma kujipa uwakili wa kuhami "dhambi" ya CCM dhidi ya Waislamu wa nchi hii.

Mwandishi anapata matangazo mengi ya biashara kutoka idara za Serikali, Tume ya Uchaguzi na Tume za Serikali na hivyo kulifanya gazeti la Msemakweli kuweza kustawi kiuchumi.

Pili, mara zote aingizapo kompyuta zake na vitu vingine kutoka nje ya nchi hupata manufaa ya msamaha wa kodi na ushuru. Ni maslahi ya aina hiyo hiyo yanayomfanya kuhofia mabadiliko. Kwamba ikija serikali nyingine kuna uwezekano wa kuyakosa hayo na kwahiyo kuamua kuipigia kampeni CCM lakini kampeni yenye hila maana lugha inayotumika ni ile ile ya amani wakati nia ni kuonyesha ama kutisha wananchi kwamba CCM isipoendelea na madaraka basi amani iliyoko itatoweka.

Ndani ya kitabu chake habainishi waziwazi amani italindwa vipi ama itatoweshwa vipi. Wala hatoi mifano hai kwamba zile nchi zenye machafuko kama Rwanda, Burundi na Somalia ni nani aliyechanganya dini na mamlaka ya nchi hadi kusababisha Wanyarwanda na Warundi, na Wasomali wafarakane, badala yake anatoa mfano wa Vatican kwamba ni tofauti kabisa na OIC.

Hakuna anayeweza kubisha kwamba Vaticani siyo OIC, lakini ni nani aliyedai kwamba CCM ikishindwa basi itaundwa Jamhuri ya Kiislamu hapa Tanzania? Je siyo wana CCM kama kweli anayatazama mambo kwenye uhalisi wake!!

Neno jingine linaloonyesha ni kauli zake za siku zote za kudai tusichanganye dini na siasa, hata jina la kitabu chake eti ni kutenganisha dini na mamlaka ya nchi, sasa wote walio wakweli mbele ya nafsi zao wanaweza kujiuliza hiyo Vaticani anayoitetea imeweza kweli kutenganisha dini na mamlaka ya nchi? Ni kiongozi gani wa kidini katika nchi hii ambaye hupewa heshma ya Ulinzi wa dola anaposafiri mikoani zaidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki? Wao Maaskofu wa Kipentekoste ni watu ambao serikali haiwajali wala haioni umuhimu wao ndiyo maana hata hotuba zao huwa hazitangazwi na Redio Tanzania wala ITV kwa kifupi hawana kauli yoyote serikalini na hawafanani kabisa kwa uzito na Maaskofu wa Kikatoliki.

Sasa inakuwaje wawe mstari wa mbele kujibu kisha wahusika wakuu (Wakatoliki) wao wakae kimya? Ndiyo maana nasema ujumbe wa kitabu hicho ni mawazo tu ya mtu binasi mwenye nia na lengo la kuhami maslahi ya kimwili.

Mfuasi yeyote wa kweli wa Yesu hawezi kutetea dhulma hata siku moja, hata ikimpasa kukosa kila kitu na kupata hasara mia kwa mia katika dunia hii bado mfuasi wa Yesu hawezi kuipiga teke haki na ati akatetea dhulma chini ya kisingizio cha amani.

Mimi nimefanya utafiti karibu miaka 17 (tangu 1983-2000) katika nchi nyingi za Kiafrika kuhusiana na suala hili la Amani, nimefikia kiwango cha kutoa kitabu kiitwacho Peace and Conflicts in Africa. Mnamo 1997 niliwasilisha muswada wangu au "synopsis" ya kitabu changu Umoja wa Mataifa New York, na ulikubaliwa.

Nasema kwa uhakika kabisa kwamba katika nchi zote zenye machafuko kama vile Rwanda, Burundi na Somalia "Ubinafsi" wa watawala aidha waliotangulia ama waliopo umechangia sana kuziingiza nchi zao katika vita na wala siyo tatizo la udini ama ukabila kama propaganda zilivyoenezwa.

Ni ubinafsi ndio uliopelekea ukiukaji wa haki za msingi za binadamu na ndio siku zote umesababisha vita. Ndiyo maana nasema kwa uhakika kwamba tukitaka amani ya kweli, tuupige vita ubinafsi wa makundi. Ni ubinafsi ndio unaowafanya watu wengine kukwepa kodi kwa njia ya kupewa misamaha na mamlaka zilizo "corrupt" katika nchi hii kisha watu hao baada ya kunufaika na hizo njia haramu ndipo hugeuka kuimba wimbo wa kwamba "vya Mungu mpe Mungu na vya Kaisari mpe Kaisari, kamwe msichanganye dina siasa" huku walengwa wakijua wazi kwamba mahubiri hayo hayawahusu, bali yanawalenga walalahoi ambao wanakamuliwa kodi pasipo huruma.

Ni ubinafsi ndio unaowafanya wengine waibe kura na baadaye waibe mamilioni ya fedha za umma na kujenga makasri maeneo ya matajiri lakini watu hao hao wanakuwa mstari wa mbele kuchoma vibaka pindi wanapodokoa chochote toka ndani ya gari zao au nyumba zao. Aidha, ni ubinafsi tu ndio unaowafanya wengine wageuke kuwa mawakili wa kutetea wizi wa kura na udanganyifu mwingine wote unaofanywa na tabaka la watawala na kulaani msimamo wa jino kwa jino huku mioyoni mwao wakiafikiana na mauaji ya vibaka.

Chonde chonde! Ubinafsi ni sumu ya Amani.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook