Kashmir na Waislamu wa Tanzania

KUMEKUWEPO vitendo vya kinyama ambavyo Waislamu wa Kashmir hufanyiwa. Waislamu wamekuwa wakiteswa, kuuawa na wengine kufungwa. Aidha, wapo wanaoteseka na kufa njaa kutokana na kuporwa mali zao na mamlaka ya India.

Kwa zaidi ya miaka arobaini na nane, Waislamu wa Kashmir wanataliwa kinyume cha ridhaa yao. Sasa, uchumi na masuala ya kijamii huongozwa kutoka Delhi. Kiuchumi Kashmir inafanywa kuwa tegemezi kwa serikali ya India, katika hali hiyo upatikanaji wa mahitajio muhimu unategemea usambazaji kutoka India.

Waislamu wa Kashmir wamebanwa sana katika elimu. Pamoja na uwingi wao ni asilimia ishirini na sita tu ya jumla ya wananchi wote waliosoma. Vile vile pato la mtu kwa mwaka ni dola mia mbili sitini ($260). Hii ni tofauti na wakazi wa Kashmir huru (Azad Kashmir) ambapo idadi ya waliosoma ni asilimia hamsini na sita na pato la mtu kwa mwaka ni dola mia nne na hamsini.

Waislamu wa Kashmir wameelemewa na ugumu wa maisha, umasikini umewaganda. Umaskini na ukosefu wa elimu ni matokeo ya ukandamizaji wa serikali ya India. Si kwamba nchi yao ina uhaba wa rasilimali, kutokana na hali hii Waislamu wajitokeze katika namna tofauti ikiwemo maandamano kupinga uvamizi.

Mwaka 1990, umati wa Waislamu ulitanda mitaa ya Srinagar wakiwa katika maandamano ya amani wakishika mabango yanayotaka utawala wa kivamizi wa India uondoke katika ardhi ya Kashmir. Wakiwa kwenye maandamano hayo, Waislamu waliwasilisha madai yao kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa.

Katika kulinda maslahi ya kinyonyaji, serikali ya India haikuwacha kuwapaka matope waandamanaji hao. Ikasema kuwa umati huo wa Waislamu uliojumuisha wanawake na watoto kuwa ni kikundi cha siasa kali na magaidi.

Kati ya Januari 1990 hadi 1993, majeshi ya India yakawavamia Waislamu na kuwapiga vikongwe, wanawake na watoto. Katika operesheni hiyo kwa uhache Waislamu arobaini na mbili elfu waliuawa. Katika vijiji, majeshi ya India yalifanya ufisadi mkubwa, mbali ya kuteswa, wanawake wa Kiislamu wapatao elfu tano walibakwa. Mnamo Febuari 23, 1991 wasichana wadogo na watu wazima wa eneo la Kunan Pushpora walibakwa.

Idadi ya waliobakwa na kufanyiwa vitendo vichafu ni zaidi ya wanawake mia moja. Miongoni mwao alikuwemo Zarifa Bano ambaye alikuwa na uja uzito wa miezi tisa. Askari watatu wa India walimbaka kwa zamu, siku nne baadaye alijifungua mtoto ambaye mkono wake wa kushoto uliathirika.

Kila walipovamia, askari hao waliziteketeza nyumba za Waislamu kwa moto. Inakisiwa kuwa zaidi ya nyumba 14,000 zilichomwa kwa madai kuwa majeshi ya India yamekuwa yakiwaua Waislamu kisirisiri, miili ya mashahidi hao huchinjwa kwenye maghala ya serikali baadaye kufukiwa au kutupwa mtoni.

Akielezea unyama unaofanywa na majeshi ya uvamizi dhidi ya Waislamu huko Kashmir, Dkt Ghulam Nabi Fai, anasema, askari ishirini na tano wa Kiislamu waliuawa na miili yao kutupwa mtoni. Miili kumi na tano ya mashahidi hao ilipatikana. Aidha, amesema, kuna Waislamu wanaonyongwa, kisha majeshi hayo hulazimisha Waislamu kuwazika usiku ili kuficha mauaji.

Tangu Waislamu wa Kashmir waanze kudai uhuru wao wamekuwa wakikamatwa, kuteswa na kuuawa mpaka sasa zaidi ya Waislamu 45,000 wanasota magerezani. Wengi wa waliofungwa ni vijana wa kike na wa kiume wa Kiislamu. Kati yao Waislamu 12,000 wamewekwa kwenye kambi za mateso. Wale waliodhaifu katika wanawake na wanaume huvuliwa nguo na kupigwa picha wakiwa katika hali hiyo.

Wakati hayo yakiendelea huko Kashmir, Waislamu wa Tanzania nao wananyanyasika ndani ya ardhi yao. Uhuru na haki zao vimeporwa. Ni kama ndugu zao wa Kashmir. Tangu waanze kudai haki zao za kikatiba wamekuwa wakijibiwa kwa vipigo, mateso, na kuswekwa mahabusu.

Yamewakuta hayo akina Bibi Titi Mohammed, marhumu Sheikh Hassan bin Amir, marhuum Sheikh Kassim bin Juma. Ni hivi karibuni marhuum Sheikh Abdallah Chata Kidagaa alikamatwa na kuwekwa kizuizini bila kosa. Akadhoofu huko na kuwa sababu ya kifo chake.

Kama ilivyo kwa Kashmir, Waislamu wa Tanzania wamezoroteshwa kielimu kutokana na hilo kumekuwepo uduni wa maendeleo katika maeneo wanamoishi. Hili linajidhihirisha katika miji mikongwe ya kihistoria kama vile Kigoma, Tabora, Bagamoyo, Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kilwa na mingineyo.

Ukweli wa kihistoria unaonyesha kuwa, wa mwanzo kujua kusoma na kuandika ni Waislamu waliokuwa wakazi wa maeneo hayo. Hata Wajerumani wakati wa utawala wao waliwatumia Waislamu waliojua kusoma kuandika. Kulikuwepo na mahakama za Kiislamu. Hata Wajerumani walijenga shule za mwanzo Tanga, Bagamoyo, Dar es Salaam, Pangani na Lindi.

Kule Kashmir Uingereza inalaumiwa kwa kitendo cha kupandikiza utawala wa Kihindu. Ni Uingereza hiyo iliyoasisi "udini" wa kuwakandamiza Waislamu. Katika kitabu "The Missionary Factor in East Africa", Bwana Roland Oliver anasema: "Ni ajabu kwamba si kanisa bali ni serikali ya Uingereza iliyoona hatari ya kuenea kwa Uislamu katika himaya za Uingereza, na ndiyo iliyochukua hatua za kuudhibiti. (1965:206).

Hali hii ya kudhibitiwa ndiyo iliyowasukuma kuanzisha harakati za kuung'oa ukoloni wa Kiingereza. Hivyo, Waislamu kama kina Abdulwaheed Sykes, Jumbe Tambaza, Tewa Said Tewa, Suleiman Takadiri, Zuberi Mtemvu, Sheikh Hassan bin Amir, na wengineo wakaanza kuyatekeleza mafunzo ya Qur'an ya kuchanganya dini na siasa kama alivyofanya Mtume (s.a.w.) na maswahaba zake.

Inapotajwa TAA na TANU katika harakati za kuikomboa Tanganyika (Tanzania) majina hayo yanawakilisha mali, nguvu, muda na jitihada za Waislamu katika kuuondoa utawala wa kikoloni. Walakini uhuru ule umetekwa nyara na kanisa, hususan Katoliki. Ubaguzi ule ule unaendelezwa.

Mfano wake ni kama ule wa Kashmir. Waislamu wa huko walisimama kupambana na ukoloni wa Kimahajarah uliosimikwa na Uingereza. Hatima yake ikawa kama kubadlishana. Ukang'oka Umaharajah ikaingia serikali ya chama cha Kihindu (National Congress).

Huko Kashmir, serikali ya Chama cha National Congress imetwaa mamlaka yote. Waislamu wanadhibitiwa, sheria za Kiislamu hazitekelezwi tena. Hakuna mahakama zinazotumia sheria za Kiislamu, kwa maneno mengine, hata kurithiana Kiislamu kumezuiliwa.

Dkt. Ghulam Nabi Fai akiielezea hali ya Kashmir anasema, utungaji wa sheria, usimamizi wake na huduma za kiutawala vimehodhiwa na serikali ya Kihindu "Judiciary and Administration services at higher level under the total control of the government of Delhi".

Mnamo tarehe 1Machi, 1972, katika mahojiano yake na "The Christian Century", mwalimu Nyerere alinukuliwa akisema jitihada zake za kujenga ujamaa wa Kiafrika nchini Tanzania zinawakilisha dhamira yake ya kutafsiri kimatendo mafunzo yaliyondani ya Injili ya Yesu.

Ndiyo kusema kuwa wakati miguvu ya dola inatumika kuung'oa Uislamu pasina kificho, Ukristo Katoliki unapewa fursa ya kuongoza sera za chama na serikali kwa mlango wa nyuma. Hii ndiyo sababu ya kufutwa kwa mahakama zilizokuwa zikitumia sharia kutatua masuala yaliyohusu Waislamu. Mara tu baada ya Tanganyika kuwa huru, mahakama hizi zikatoweshwa.

Sambamba na hilo, zimekuwepo jitihada za makusudi zilizoasisiwa na serikali katika kuitokomeza sheria ya Kiislamu kuhusu mirathi. Itakumbukwa kuwa Tume ya Mwaikasu ilivyopewa uwezo wa kuzunguka nchi nzima kwa madai ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuwa na sheria moja ya mirathi.

Ili kudhibitisha kilio cha Waislamu wa Kashmir kisisike ulimwenguni, serikali ya Kihindu imedhibiti mtandao wa habari. Waandishi na vyombo vyote vya habari visivyo vya mlengo wa kiserikali vimetiwa kufuri. Lengo kuu ni kukata mawasiliano yatakayoibua huruma za Waislamu wa nje. Misaada ya kielimu, kiuchumi na mingine isiwafikie.

Katika Tanzania, hili limefanyika kwa namna yake. Jumuiya ya Waislamu ya Afrika Mashariki (EMWS) ikatolewa nchini. Ikatangazwa rasmi kuwa jumuiya hiyo haitambuliki tena kisheria. Hivyo ikabatilishwa na kufungiwa nje ya mipaka ya Tanzania.

Ni wazi kuwa malengo ya serikali ya Kihindu dhidi ya Waislamu yanarandana na serikali ya Tanzania. Yote yana lengo kuwadhoofisha Waislamu. Iwakandamize bila ya kufurukuta wala kupumua. Kusudio hilo likaifanya serikali iwaundie Waislamu jinamizi liitwalo BAKWATA.

Mali zote za Waislamu chini ya East Africa Muslims Welfare Society zikakabidhiwa BAKWATA. Ule mpango wa kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu ukafa. Leo hii Waislamu wa Tanzania wamedumazwa kwa asilimia kubwa katika elimu. Hali hiyo ni kama ndugu zao wa Kashmir.

Kuteseka kwa Waislamu wa Kashmir kunatokana na hujuma zinazofanywa na serikali ya uvamizi. Angalia wao wanasikika kimataifa na inajulikana na huko Umoja wa Mataifa kuwa kuna ukoloni wa Kihindu ulijikita Kashmir. Dhulma wanayofanyiwa takriban inajulikana pia katika ulimwengu wa Kiislamu.

Tanzania inafahamika kuwa ni nchi huru. Ni nchi inayojitangaza kuwa ya kidemokrasia ambapo katiba yake inalinda haki za binadamu. Inadaiwa kuwa heshima, uhai na utu ni vyenye kulindwa, kwamba mbele ya sheria vyombo vya sheria hakuna upendeleo.

Uzoefu walionao Waislamu wa Tanzania kuhusu serikali ya Chama tawala ni kama ule wa serikali ya Chama cha National Congress kule Kashmir. Polisi wa serikali ya CCM walivamia Msikiti wa Mwembechai, wakapiga Waislamu wake kwa waume. Baya zaidi ni kile kitendo cha "ubakaji" cha polisi wa kiume kuwapekuwa wanawake wa Kiislamu sehemu za siri.

Tukio hili la kuwadhalilisha wanawake ni kama lile la Kunan Pushpora la Februari 23, 1991 ambapo zaidi ya wanawake mia walipigwa na kubakwa na askari wa India huko Kashmir. Lililo kubwa katika yote ni kuuawa Waislamu kama wanyama.

Tunafahamu kuwa, marehemu Muhammed Omar alikuwa miongoni mwa waliokamatwa, kukakamatwa kwake kulihalalishwa na tuhuma za "wanaotuhumiwa" "siasa kali" zilizotolewa na viongozi wa serikali. Mnamo Mei 18, 1998, Muhammed Omar alifariki akiwa gerezani. Na kuzikwa bila uchunguzi. Hii ni sawa na serikali ya Kihindu inavyoshinikiza kuwazika usiku, Waislamu inayowaua.

Hayo yanawafika Waislamu kwa sababu ya Imani yao. Hakuna dhulma waliyofanya. Lakini wenzetu wa Kashmir wanaendelea kufanya jitihada za kukataa kudhulumiwa. Walianza harakati zao tangu mwaka 1931.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook