Hatujutii kuwa Waislamu katu
Ndugu Mhariri
NAFASI hii naiomba kwako kwa minajili ya Tahariri yako ya tarehe 8 Septemba iliyochukua kichwa cha habari kisemacho "Kibri hii inatoka wapi? Mnajuta kuwa Waislamu?"
Mimi naanza kwa msemo wa hapo juu ya kwamba Waislamu katu hatujutii. Yale uliyoyaona wewe pamoja na watazamaji wengine kwenye TVT pia mimi nimeyaona, bali sikuyaona tu ila na kuyasikiliza vyema sana.
Mtiririko wa maswali ya kijana Paschal Mayala ulionyesha dhahiri kuwa kama hakuandaliwa yeye kwa mashambulizi basi ni yeye mwenyewe alikuwa amejiweka vyema kwa matusi yale.
Ndugu yangu Mhariri pamoja na wasomaji wa gazeti hili kwa ujumla wenu, napenda niwahakikishie wazi kuwa Uislamu ulitukanwa vizuri sana zama za Mtume (s.a.w.) kisha na watukanaji wenye kujua lugha za matusi, wamepita, wakaja wengine kama hao nao pia wakapita tena kwa fedheha kubwa.
Sasa isiwe hoja kwa mtu mdogo sana kuwadharau wavaaji vibandiko kwa kuwaamanisha na Waislamu, hilo si jambo bali alichotusaidia kijana huyu ni kwamba tuwe macho na mtazamo wa watu kama yeye kwenye maeneo yote hapa nchini.
Jibu alilompa muulizwa swali yaani ndugu Lipumba, lilimtosha sana na hata alipopewa nafasi na muongoza kipindi ili aulize tena hakuwa na kitu.
Kama ninavyosema awali hatostaajabu kule Nigeria akiona kwenye mikutano ya siasa kuna majoho na vibandiko kwani mavazi hayo hayo yanaonekana kwenye maofisi mahospitali na kwingineko. Tuvae ipasavyo watujue ipasavyo. Sasa cha kumwambia Mayalla ni kuwa hao wenye vibalaghashia ndio walioifanya nchi hii leo kuwa kama ilivyo na yeye leo akaweza kutangaza TVT.
Kwa faida ya Pascal Mayalla na wale wenye mawazo kama yeye ni kuwa TANU chama ambacho kilizaa CCM pamoja na vyama vyote avionavyo yeye kwa sasa waanzilishi wake ni hao hao wenye vibaraghashia ambavyo Mayalla havitaki viwe kwenye harakati za siasa na kuendesha nchi. Pia kwa Waislamu wenyewe huu ni wakati muafaka kabisa kujitambulisha kwa akina Mayalla kwamba kuvaa hijab au baraghashia haukuzuii kutenda shughuli yoyote ya kujenga nchi hata kwenda vitani. Kwani hatuoni kwenye TVS watu wa nchi nyingine Waislamu wanapatikana kwenye nyanja zote hali vichwa vina baraghashia?
Basi Mungu atuwafikishe mema tuyashike na mabaya tuyaache kwa kutarajia radhi za Mola wetu mtukufu.
Alhaj Abuu Rashid Marjeby Kibaha
S.L.P. 7319,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
JUMANNE ya tarehe septemba 12, mwaka huu hapa Morogoro ulifanyika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu ambao utafanyika tarehe 29 mwezi huu.
Mkutano huo wa Chama cha Wananchi (CUF) ulifanyika katika uwanja wa shule ya msingi Kiwanja cha Ndege na kuhutubiwa na mgombea kiti cha Urais kupitia vyama vya CUF na CHADEMA, Prof. Ibrahim Lipumba.
Nikiwa mmoja miongoni mwa wengi waliohudhuria mkutano huo, nimeshangazwa na kitendo cha kituo cha Televisheni cha Abood (ATV) cha hapa Morogoro kueleza habari za mkutano huo tofauti na ilivyokuwa.
Katika taarifa yake ya habari ya usiku huo, Abood TV haikuelezea chochote juu ya yaliyosemwa katika mkutano huo.
Hata picha ya umma uliohudhuria mkutano ule haikuoneshwa, badala yake mtangazaji wa Abood TV amesikika akitangaza ya kwamba mkutano wa CUF umetawaliwa na fujo!!
Fujo gani hizo ambazo ATV waliziona? Cha kushangaza hata mtangazaji alipokuwa akitangaza habari hizo, alikuwa akisizoma tu bila ya yeye kuonekana kwenye "screen". Kwenye screen kulikuwana maandishi tu ya kueleza "FUJO ZA CUF".
Kila fani ina maadili yake, fani ya habari nayo ni hivyo hivyo. Moja ya kazi ya vyombo vya habari ni kufikisha habari kwa jamii. Hivi sasa tumo kwenye kipindi cha kampeni za uchaguzi.
Wananchi wanahitaji kufikishiwa habari za wale wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi ili wapime uwezo wao na kusikia sera zao. Ikiwa Abood TV kwa sababu moja au nyingine hawataki watazamaji wake waone na kusikia habari za baadhi ya wagombea, basi waishie hapo tu.
Ikiwa Abood TV itaendelea na mtindo huo wa kushabikia baadhi ya habari na kupotosha nyinginezo, kuna hatari ya kupoteza imani ya wananchi kwa kituo hicho cha TV.
Kwa kumalizia nawaasa watangazaji wa Abood TV kushikamana na maadili ya kazi yao. Wao ndio walio karibu na watazamaji. Habari yoyote ya kupotosha itaonekana kana kwamba inatoka kwao binafsi.
Muda wa kujisawazisha bado upo. Ni vizuri waangalie maadili ya utangazaji ili kurudisha imani ya wananchi kwa kituo hicho cha TV.
Salim Omar,
Morogoro.
Ndugu Mhariri
Naomba japo nafasi kidogo ili niweze kuwaasa polisi. Ni majuzi tu ambapo Mkuu wa Polisi Bw. Omar Mahita alionyesha ukereketwa wake pale alipokutana na polisi jijini Dar es Salaam.
Huku akionyesha kukerwa mno na mwelekeo wa kisiasa ambao unabashiri hatima yake mwenyewe na CCM hapo Oktoba 29.
Mheshimiwa Mahita alionesha jinsi alivyopania kuchochea jeshi la polisi dhidi ya raia ambao wana shauku ya kuleta mabadiliko na kurejesha matumaini katika nchi hii.
Ama kweli inashangaza pale kiongozi anapoonesha jeuri na ukatili namna ile dhidi ya walipa kodi.
Kodi za hao anaoagiza waburuzwe kwa marungu, mabomu hata risasi za moto ikibidi, ndizo zinazomwezesha yeye binafsi kuishi maisha ya kifahari kama vile kutumia helkopta kuja Morogoro kuwasalimia ndugu zake licha ya gharama za safari hizo kuwa ni kubwa kuliko angelitumia gari.
Morogoro sio kisiwa kiasi cha kulazimu matumizi ya usafiri wa helkopta. Huku ni kulewa madaraka na kweli inabidi Oktoba 29 iwe ni mwisho kwa viongozi ambao wameshajigeuza miungu katika nchi hii.
Polisi msilaghaiwe na wakubwa zenu kumwaga damu za raia ambao mnapaswa kulinda haki zao. Nyie ni mashahidi wa hali zenu za maisha pamoja na baba zenu, mama zenu, watoto zenu, dada zenu, jamaa zenu, jirani zenu na Watanzania wote kwa ujumla. Umaskini, ujinga na maradhi vimekuwa ni sehemu ya maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Muelewe wazi kuwa nyie ni sehemu ya Watanzania, ndugu zenu wa damu tunaishi nao mitaani, uzee unawajia hivyo tunawasubiri mstaafu na mtarejea uraiani na upolisi si urithi mtakapowapa watoto zenu na wajukuu zenu, kwa hali yoyote ile bado nyie ni raia wa nchi hii na upolisi ni kazi tu. Msihadaiwe mkakiuka maadili ya kazi zenu.
Abu Salma,
Morogoro.
Ndugu Mhariri
NAOMBA japo nafasi kidogo katika gazeti lako ili kuwaasa Waislamu wenzangu.
Tunafahamu dhulma tunazofanyiwa na serikali ya CCM. Sisi kama jamii ya Watanzania tunazo haki za kimsingi ambazo hatupewi kama Watanzania wa dini nyingine, hasa Wakatoliki.
Tunayo haki ya kutokichagua chama ambacho kimeshindwa kutoa haki sawa kwa wote na kuondoa umaskini, ujinga na maradhi kwa Watanzania.
Sisi Waislamu tunayo sababu ya kuiondoa CCM ili tuinusuru nchi yetu na dhulma.
Abu Salma,
Morogoro.
Ndugu Mhariri
HOTUBA ya kampeni ya Rais na mgombea wa CCM hapa Singida ni ya uwazi na ukweli hasa. Hongera mgombea. Mkapa ametueleza katika miaka yake mitano ametumia bilioni mbili na nusu kwa ajili ya mkoa wa Singida hasa katika barabara.
Lakini katika miaka hiyo mitano ni bilioni ngapi zimetumika kupaka rangi Ikulu (ukarabati)?
Ukarabati wa Ikulu na mkoa wa Singida upi umetengewa bajeti kubwa katika miaka hiyo mitano?
Hivi Singida na Ikulu ni ipi inahitaji pesa zaidi kuikarabati?
Laurin Marwa M.,
S.L.P. 21984,
(Chafosa Cheygoda CUF 2000),
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |