TAHARIRI

Polisi isiwagawe wananchi

"Wana CCM wawili wa-Kizanaki wakamatwa kwa mauaji ya Mwembechai".

"Wana CCM watano kutoka Butiama wakamatwa kwa kumpofua macho mwana TLP huko Arusha".

"Mwanzilishi wa CCM kutoka Musoma aua huko Pemba".

Jaalia unasikia au kusoma habari kama hizi katika vyombo vya habari: Lakini pia vikakueleza kuwa taarifa hizo wanakuletea kama zilivyotolewa rasmi na msemaji wa Jeshi la Polisi.

Ni wazi kuwa lengo la taarifa kama hizi sio kuarifu juu ya uhalifu uliotokea.

Bali lipo lengo la ziada ambalo laonekana kuwa muhimu zaidi.

Msisitizo wa kabila na sehemu wanayotoka watuhumiwa unalenga kuwafungamanisha na uhalifu na hivyo kuwachonganisha na jamii.

Lingine ni kujenga hisia kwamba chama husika (kwa mfano huu CCM) ni cha Wazanaki na Wazanaki ni watu wa shari.

Mtoa habari anachotaka kupata ni kuwafanya Watanzania wengine si kukichukia tu chama hicho bali na wanaodaiwa kuwa wenye chama chao.

Hata mwanasiasa akiwa jukwaani hana dharura wala kibali cha kutumia maneno kama haya.

Lakini yaweza kuwa nafuu kidogo kwani wanasiasa wengine waweza kuwa maadhura wasiojua kuchagua maneno.

Inastaajabisha maneno kama hayo yanapotamkwa na polisi tena akiwa msemaji wake mkuu.

Hapo ndipo utajiuliza, kwani lengo la jeshi la polisi ni nini? Kuwagawa wananchi! Kujenga chuki baina ya Watanzania! Kujenga ubaguzi au kushughulikia wahalifu?

Kama ni kushughulia wahalifu, kusema kuwa polisi wamewakamata wana CUF wawili kutoka Pemba wakifanya fujo inakujaje.

Tunahoji kwa sababu hivi karibuni vyombo vya habari vimemnukuu msemaji wa jeshi la polisi Bw. Aden Mwamunyange akitoa taarifa kama hizo. Taarifa zilizodai kuwa Wapemba hao wakiwa wana CUF waanzilishi kufanya fujo baada ya mkutano wa kampeni Manzese. Navyo vyombo vya habari utadhani vilipewa maagizo rasmi vikautilia shada huo Upemba.

Ungoni, Uzanaki na Upemba wa mtu unahusika vipi na uhalifu hata usisitizwe kwenye ripoti ya polisi?

Hatudhani hayo ndiyo maadili ya utendaji kazi wa polisi kitaalamu.

Tungedhani ni vyema polisi wakazingatia majukumu yao na kuepuka yale ambayo hayaisaidii nchi bali kuibomoa.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook