Janja ya CCM kupora shahada yakwama

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeshutumiwa kwa kuanzisha tabia ya kuwalaghai wananchi wanaonekana kuwa upande wa upinzani kwa kuwachukulia shahada zao za kupigia kura, imefahamika.

Tabia hiyo ambayo imeanza kugunduliwa kata ya Yombo Vituka Manispaa ya Temeke inadaiwa kuongozwa na wajumbe wa nyumba kumi wa CCM ambapo wananchi walio wengi bado wanajuwa ni vingozi wa watu wote.

Shutuma hizo zimetolewa juzi na Katibu, kata ya Yombo Vituka wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Kaisi R. Kaisi alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake.

"Mwishoni mwa mwezi uliopita mjumbe wa nyumba kumi wa CCM, Bw. Chihembe alichukua shahada ya mke wa Bw. Hamad Seleman ambapo alipomueleza mumewe, aliambiwa akaifuate na mjumbe huyo aliitoa huku akimuomba samahani", amesema Bw. Kaisi.

Amesema, CCM wameanzisha mbinu hiyo baada ya ile iliyokuwa inatumiwa na polisi wanapowakamata wanachama wa CUF na kuwachana shahada wanazowakuta nazo. "Tumewaelimisha wanachama wetu wasitembee na shahada zao jambo ambalo limesaidia kutopoteza kura zetu".

Amesema, wanachama wake walipoenda tena kesho yake kufuatilia kesi yao wakaambiwa anayesimamia kesi yao ameshahama kituoni hapo siku nyingi hivyo wakatakiwa waondoke na hawana kesi ya kujibu.

Katika kuendeleza ubabe dhidi ya CUF, Bw. Kaisi amesema, Septemba 29, mwaka huu, walinzi wa CCM waliwashambulia wanachama wanne wa TLP na wawili wa chama chake kabla ya kuwafikisha polisi ambapo waliachiwa baada ya kusota rumande siku tatu.



Kampeni za chama cha CUF:
Ujio wa Mkapa Bukoba mateso kwa wananchi

WATU kadhaa wamekamatwa na kuwekwa ndani, kufuatia ziara ya kampeni ya Rais Mkapa mjini Bukoba.

Imeelezwa kuwa kabla ya mgombea Urais wa CCM kuingia Bukoba, CCM walifanya zoezi la kushusha bendera za vyama vingine vya siasa na kuchana picha za wagombea wao.

Pamoja na taarifa hizo kufikishwa polisi, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.

Kinyume na matarajio, walioripoti matukio hayo walikamatwa na kuwekwa mahabusu.

"Hii ni ishara ya kushindwa na kukwama kisiasa", ameeleza mkazi mmoja wa Uswahilini akielezea tukio hilo.

CCM Bukoba inakabiliwa na upinzani mkali kutoka chama cha Wananchi CUF na inadaiwa sasa inatumia vitisho kama silaha ya mwisho.


Sikonge wafanya sherehe kubwa


WANANCHI wa Sikonge juzi walifanya sherehe kubwa kama ishara ya kuwakubali na kuwapa kura wagombea wa Chama cha CUF na CHADEMA.

Sherehe hizo zilIzofanyika katika kijiji cha Idakawiro ziliambatana na ngoma za Kinyamwezi na Kisukuma.

Aliye mgombea Mwenza Bw. Nasor Khamis alikuwa kijijini hapo kwa mikutano ya kampeni akimnadi Prof. Lipumba na Bw. Kassanga Tumbo anayegombea Ubunge.

Ni baada ya kumaliza kuhutubia, ng'ombe walichinjwa watu wakala na kucheza.

Katika hotuba yake Bw.Nassor Khamis aliahidi kuwa serikali ya CUF itajali shida za wananchi na kuhakikisha kuwa vipato vyao vinakidhi matarajio yao.

Alisema, watumishi wa serikali ambao vipato vyao ni duni kama polisi wataangaliwa na hali zao kuboreshwa.

Baadaye Bw. Nassoro alimnadi mgombea Ubunge wa CUF-CHADEMA katika wilaya ya Sikonge Balozi Kassanga Tumbo ambaye wananchi wengi walidai kwamba ndiye mgombea pekee wanayemwamini kuwa ana uwezo wa kuwaletea maendeleo kwani alionesha uhodari wake tangu Tanzania ilipopata uhuru.

Wananchi hao walidai kuwa walishuhudia balozi Kassanga Tumbo akiwekwa kizuizini kijijini kwake na serikali ya awamu ya kwanza kwa muda wa miaka 18 huku akiwa na ulinzi wa polisi ambapo hakuruhusiwa kutoka nje ya mkoa wa Tabora.

Wananchi hao wanasema kuwa Balozi Kassanga Tumbo alipata shida zote hizo kwa ajili ya kuwatetea Watanzania hasa wa eneo lao hivyo wana sababu ya kumchagua kuwa mbunge wao.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook