Hotuba ya Maalim Seif Z'bar

Hotuba ya mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad katika mkutano na waandishi wa habari -Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, Zanzibar -Jumamosi 16 Septemba 2000

Mada: Mwelekeo wa CUF katika sekta ya Elimu

UTANGULIZI:

Waheshimiwa waandishi, kama nilivyoahidi siku nilipozindua Kampeni zangu tarehe 23 Agosti 2000, leo hii tunaendelea na programu yetu ya kukutana ili kuweza kuzungumzia sekta muhimu zinazogusa maisha ya Wazanzibari.

Katika kutimiza ahadi hiyo, leo nimepanga kuzungumza nanyi juu ya Mwelekeo wa CUF katika Sekta ya Elimu hapa Zanzibar. Nimeipa mada hii umuhimu wa pili baada ya ile ya Uchumi, kwa sababu naamini Elimu ni uti wa mgongo wa maendeleo ya Taifa lolote lile Ulimwenguni ikiwemo Zanzibar.

Waheshimiwa, kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, Wazanzibari wamekuwa wakishuhudia kuporomoka taratibu lakini kwa uhakika kwa Sekta ya Elimu. Kabla ya hapo Zanzibar ikijivunia kiwango chake cha elimu kwani kilikuwa kivutio kikubwa kiasi kwamba Watanganyika na Wamalawi waliona fahari kuja Zanzibar kwa kupata kusomea Ualimu. Sifa hizo zilikuwepo kwa sababu ya kujengeka msingi madhubuti (solid base)ya mfumo wake wa Elimu kwa jumla. Hadi kufikia mwaka 1958, Zanzibar iliweza kuvunja rekodi kwa kuwa nchi ya kwanza katika mafanikio ya wanafunzi kati ya nchi zote za Jumuiya ya Madola ambazo zilikuwa zinafanya Mitihani ya Cambridge Certicicate Examination. Wazanzibari waliobahatika kupitia mfumo huo wa Elimu wamezagaa duniani kote na ni wasomi wanaosifika. Wamo Maprofesa, Madaktari bingwa, wahandisi na wataalamu wa fani nyengine.

KUSHUKA KWA VIWANGO MBALI MBALI:

SERA YA ELIMU

Eneo la msingi ambalo halikutiliwa mkazo ni kule kutokuwepo mwelekeo unaoeleweka wa madhumuni ya Elimu ambayo ilitarajiwa kumjenga Mzanzibari aliyetakiwa kwa nyakati zote. Tumeshuhuduia katika kipindi hicho maamuzi yaliyokuwa hayazingatii kwamba Elimu hupangwa na kutekelezwa kwa kuzingatia utamaduni wa watu, sosholojia na Elimu nafsi ya watu. Kwa mara ya kwanza jaribio la kuwepo kwa sera ya Elimu lilijitokeza mwaka 1982.

Sera hiyo ya Elimu ndiyo iliyozaa Sheria ya Elimu ya mwaka 1982. Sheria hiyo iliweka utaratibu wa kutoa Elimu, uendeshaji wa Sekta ya Elimu na mambo mengine yakiwemo Kanuni na taratibu za Elimu nchini. Kwa bahati mbaya, sheria hiyo haikupewa nafasi iliyokusudiwa na kwa hivyo utekelezaji wake ukazidiwa na maamuzi ya kisiasa.Hivyo basi, kuwepo kwa sheria hiyo hakukusaidia kuzuia Elimu kuporomoka. Maamuzi ya kisiasa yalipopewa nafasi kubwa zaidi ya ushauri wa kitaaalamu, hali hii tunayoiona wakati huu, ya vurugu katika sekta hiyo ndiyo matokeo yake. Madhumuni ya Elimu hayajulikani, Mfumo wa Elimu unabadilika mara kwa mara na hata nyanja nyengine hazieleweki zinavyoendeshwa.

MIPANGO YA ELIMU

Katika kipindi cha miaka 36, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichoweza kufanya katika Sekta ya Elimu ni kuwaruhsu wananchi kujijengea mabanda ya skuli. Serikali imewashawishi wananchi hao bila ya Serikali yenyewe kuzingatia mahitaji mengine yatakayowezesha mabanda hayo kuwa skuli. Kwa namna hiyo, mabanda hayo yamejengwa kiholela bila ya kuzingatia vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa. Si ajabu mijini na vijijini kukuta mabanda yaliyojengwa kwa madhumuni ya kuwa skuli lakini hukuti nyumba za walimu, vyoo, uwanja wa kuchezea au maabara. Wakati mwengine, Serikali imefikia hatua ya kuyatumia mabanda ambayo yalikusudiwa kufanyiwa Maonesho ya Kibiashara kuwa skuli za praimari na sekondari. Hali kama hiyo inaonekana waziwazi katika sehemu ya Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi Unguja ambako hali ni mbaya, inatisha, inasikitisha na kukatisha tamaa.

Huko vijijini, hali ni mbaya zaidi. Mtu yeyote hatosita kuishutumu Serikali kwamba haithamini Elimu hata kidogo. Watoto wanaosoma katika mazingira hayo ni wale wa wazee maskini. Haya yote yanatokana na ama kutokuwa na mipango madhubuti ya Elimu au kama ipo basi haitekelezwi na badala yake maamuzi ya kisiasa ndiyo yaliyopewa kipaumbele zaidi.

Ya kukatisha tamaa zaidi ni kukosekana kwa walimu wanaofaa. Kwa sababu kazi yenyewe ya Ualimu imepuuzwa na walimu kutothaminiwa, matokeo yake ni ama waliosomea Ualimu hutafuta kazi nyengine zinazoonyesha hadhi au mapato mazuri au wanafunzi husomeshwa na walimu wasiofaa kwa kiwango kinachotakiwa. Si ajabu hata kidogo kukuta walimu waliokusudiwa kufundisha skuli za praimari wanafundisha wanafunzi wa sekondari. Lakini hata taaluma ya Ualimu yenyewe haijaweza kupewa nafasi inayostahiki. Unapata mashaka makubwa unapohakikishiwa kuwa huwezi kupata nafasi ya kusomea kazi ya Ualimu endapo Sheha wa Shehiya unayotoka hajatoa ushauri wake kwamba mhusika ni mkereketwa wa CCM. Hivyo, katika hali kama hiyo, mtu anatarajia Elimu katika Zanzibar iweje?

Wingi wa wanafunzi darasani halikadhalika unatisha. Walimu siku hizi hawaoni ajabu kusomesha wanafunzi 109 katika darasa moja. Hiyo ni miongoni mwa sababu zinazowalazimisha walimu wasiweze kuwashughulikia wanafunzi vile inavyotakiwa. Mwalimu hapati hata ushawishi wa kuwapa wanafunzi wake mazoezi ya nyumbani kwani akifikiria kusomesha masomo mawili tu kwa darasa hilo basi kazi ya kuyapitia kwa kuyasahihisha madaftari 140 kwa siku hawezi akaikamilisha kwa ufanisi.

Siku hizi vitabu vya kiada (text books) havipatikani maskulini. Isitoshe, hata madaftari ya kuandikia hayapatikani kama ilivyo kwa vifaa nyengine ambavyo mwanafunzi analazimika avipate kuweza kujisomea vizuri. Serikali ya CCM hapa Zanzibar haikuweza kuthamini hata misaada iliyokuwa ikiipata kutoka kwa Wahisani wa Nje na ambayo ilikuwa isaidie Sekta ya Elimu hapa Zanzibar. Katika kipindi cha kama miaka 10 iliyopita, Shirika la Misaada la Sweden liliipatia serikali msaada wa kutengeneza madaftari ya kuandikia pamoja na makaratasi ya kuchapishia vitabu vya kusomea. Mradi huu haukuthaminiwa na Serikali ya CCM ikachukua maamuzi ya kisiasa kiasi kwamba mradi huo ukafutwa. Kwa sababu Serikali haikujali kufutwa kwa msaada huo, matokeo yake hivi sasa wanafunzi wanalazimika kununua madaftari wao wenyewe,jambo ambalo linawapa ugumu mkubwa wazazi wao.

Mradi mwengine ambao uliathiriwa na maamuzi ya kisiasa badala ya kuzingatia kuwaondolea watoto wa maskini shida ya mazingira mabaya ya kusomea ni ule wa kuzitengeneza Skuli za Sekondari. Mradi huo ulikuwa unasimamiwa na Shirika la Misaada la Denmark (DANIDA) na ulipangwa udumu kwa muda wa miaka 12. Mradi ulifutwa baada ya miaka mitatu (3) tu ya uhai wake. Mradi huu ulikuwa wa manufaa makubwa sana kwani katika kipindi hicho kifupi baadhi ya maskuli yaliyokwishaanza kuanguka yaliokolewa. Jee, kufutwa kwa mradi huo kumesababisha hasara iliyoje kwa nchi hii? Ni dhahiri kwamba watawala hawakuwa wakiwajali watoto wa wananchi wa kawaida.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook