Mbukuzi aitahadharisha Tume ya Uchaguzi

AMIR wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Salim Mbukuzi amerudia nasaha zake kwa Tume ya uchaguzi kufanya uadilifu katika kusimamia zoezi la upigaji na utoaji wa matokeo ya kura.

Sheikh Mbukuzi amesisitiza usemi huo alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake Mburahati Jijini jana.

Amesema, kitu ambacho kila mtendaji wa Tume hiyo angepaswa kukizingatia ni maslahi ya nchi na wananchi wake.

Kwa ajili hiyo sheikh huyo ambaye mara kadhaa amekuwa mstari wa mbele kuitahadharisha serikali na hali zinazotishia kuigawa jamii amesema, Tume isimamie na hatimaye itoe matokeo sahihi ya maamuzi ya wapiga kura.

"Kusiwepo na hila za kumtangaza mshindwa badala ya mshindi au kutoa fursa kwa chama fulani kujipigia kura kinyume na utaratibu na kura hizo zikajumuishwa na zile za halali, kuwepo na uwazi katika kupiga na kuhesabu na kutoa matokeo", amesisitiza Amir huyo wa Shura.

Aidha ameshauri kuwepo uhakiki wa idadi ya waliojiandikisha utakaosaidia kuwajua vyema wapiga kura wote.

Amesema, zoezi hilo litaondoa wasi wasi walionao baadhi ya watu kuhusiana na idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura.

"Kufanya hivyo kutaondoa dhana kwamba huenda kulikuwa na ongezeko la kimya kimya la idadi ya waliojiandikisha kupiga kura katika idadi iliyotangazwa na Tume", ameasa kiongozi huyo wa Waislamu.

"Katika kipindi hiki kilichobakia Tume iwaagize watendaji wake kwa kuvishirikisha vyama kuhakiki idadi, gharama si kitu mbele ya suala nyeti kama hilo ambalo pindi ikijitokeza dosari hugharimu maisha ya watu na kusambaratisha nchi ", ameongeza Sheikh Mbukuzi.

Amesema, Tume itakuwa imetimiza wajibu ambao historia ya nchi hii itaurekodi iwapo itajiepusha na harakati za wachache wanaotaka kujitwalia nyadhifa kinyume na ridhaa ya walio wengi.

Kuhusiana na kauli ya Kamanda wa polisi Bwana Omar Mahita kuwa mara tu mtu atakapopiga kura aondoke haraka kituoni, Sheikh Mbukuzi amesema hizo ndizo dosari zenyewe ambazo Tume ya uchaguzi inapaswa kuzishughulikia mapema.

Amesema kama kisheria ni haki ya wananchi kusubiri mita chache kutoka kituoni mpaka wajue matokeo ya kura walizopiga vipi Kamanda Mahita atoe amri inayopiga marufuku Haki hiyo ya Mwananchi.

"Polisi ni chombo cha Serikali ni kinyume na Katiba ya nchi kuwazuia raia wasitumie haki yao hiyo, nini kimepangwa mpaka wazuiwe wananchi kushuhudia zoezi hilo mwanzo mpaka mwisho", amehoji Mbukuzi

Amelitaka jeshi la polisi litekeleze wajibu wake kwa kujiepusha na hatua zinazolenga kukisaidia chama fulani.

"Ni jambo la kushangaza kumuamuru mtu atumie dakika moja kujiamulia namna atakavyoishi kipindi cha miaka mitano, huyu ndiye atakaevuna matunda ya uamuzi wake wa kura kwa miaka hiyo kama ni matatizo atakumbana nayo yeye na kama kinyume chake ni yeye kwa nini asitumie siku nzima au hata mbili kwa ajili ya hiyo", amedai Amir Mbukuzi.

Aidha amevitaka vyombo vingine vinavyolinda usalama wa nchi kutotumika kufanya hila kukisaidia chama fulani kishinde badala yake isiwe tu viseme viko pembeni na vitakuwa tayari kumtii mshindi atakayetangazwa bali vihakikishe uadilifu unakuwepo katika kupiga kura na kutangazwa matokeo.

Ameviomba vyombo hivyo vitumie mitandao yake kuhakikisha wananchi wanakuwa huru kutekeleza haki yao hiyo na kudhibiti hatua zozote za uonevu, unyanyasaji, vitisho na ukiukaji wa sheria utakaojitokeza miongoni mwa wale watakaokuwa na dhima kulinda amani na usalama siku hiyo.

Zimebaki wiki mbili kabla ya watanzania kuingia katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani na wawakilishi katika serikali za Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.

Wagombea Urais katika kinyang'anyiro hicho ni Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF na CHADEMA, Benjamin Mkapa wa CCM, Agustino Mrema wa TLP na John Cheyo wa UDP.

Kwa mujibu wa Ratiba za Vyama vya CUF, CCM na TLP kampeni hizo zitamalizikia Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Jangwani, Karume na Mnazi mmoja.

Wakati huo huo, Wasimamizi wa Uchaguzi majimbo ya Mbeya mjini na Vijijini wamelalamikiwa kwa kuongeza idadi ya wapiga kura.

Chama cha Wananchi (CUF) kimetoa malalamiko hayo juzi ambapo kimedai orodha iliyokuwepo mpaka agosti 28 ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya uandikishaji ilionesha jumla ya watu 37, 390.

Katibu wa chama hicho Wilaya amedai kuwa hivi sasa ina ongezeko la watu 1000 katika orodha hiyo ambao haijulikani waliandikishwa lini na wapi.

Amedai kuwa Wasimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo wameshindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusiana na ongezeko hilo.

Wilayani Rungwe, Mwandishi msaidizi wa wapigaji kura wa eneo moja wilayani humo ameripotiwa kufikishwa mahakamani baada ya kudai kupoteza kitabu chenye orodha ya wapiga kura.

Mwandishi huyo amehukumiwa kulipa faini ya shilingi 10000 kutokana na upotevu huo.

Hata hivyo haikuelezwa ni hatua zipi zitachukuliwa na Wahusika kuzuia usumbufu au hila zozote zitakazotokana na upotevu huo.

Mkoani Mwanza imeripotiwa watu kukutwa wakigawa shahada za kupigia kura katika mja ya ofisi zilizoko mjini humo wiki iliyopita.

Katika uhalifu huo waliwekutwa Mwanasheria wa Manispaa na Mgombea wa CCM.

Mpaka sasa Tume ya Taifa ya uchaguzi haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na dosari hizo ambazo zimeelezwa kutishia uwezekano wa kuwepo kwa haki na uadilifu katika uchaguzi mkuu ujao.

Aidha kumekuwa na taarifa zinazotuhumu kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya watu iliyotangazwa na Tume ya uchaguzi kinyume na hali halisi.

Baadhi ya watu Jijini wametuhumu ogezeko hilo kuwa huenda ni la wapiga hewa walioongezwa ili kujenga mazingira ya ukiukaji wa uadilifu utakaolenga kukisaidia chama tawala.

Tume kwa upande wake haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na tuhuma hizo ambazo hivi sasa zimezagaa nchi nzima hali inayoashiria uwezekano mkubwa wa kuvurugika kwa amani.


Maji kizaa zaa Ubungo

Tatizo la maji limeendelea kuwakumba wakazi wa Ubungo ambapo kwa majuma mawili sasa wananchi hao wamekuwa wakihangaika usiku na mchana.

Mpaka jana wananchi hao waliendelea kuhangaika huku na kule kusaka maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Mwandishi ameshuhudia msururu mkubwa wa watu waliokuwa wakisubiri kujaribu bahati ya kupata maji katika kisima kimoja jirani na shule ya msingi Ubungo Kisiwani.

Wananchi hao walikuwa wakitoa shutuma kali dhidi serikali ya CCM kwa kushindwa hata kusambaza maji kwa wananchi.

"Kazi yao kuomba kura waendelee kutawala, hawana wanachokifanya hata kuchimba visima wanashindwa viongozi gani hawa", amelalamika dada mmoja aliyefahamika kwa jina la mama Daudi huku akiwa ameshikilia ndoo nne za plastiki.

Akizungumza na Mwandishi kuhusu tatizo hilo, Baba Maryam mkazi wa muda mrefu eneo hilo amesema siku za nyuma kulikuwa na utaratibu wa maji kutoka kila siku za jumatano na Alhamis lakini hivi sasa utaratibu huo haupo.

"Tunaweza kukaa zaidi ya wiki moja bila ya mabomba kutoka maji, tunategemea visima vya watu, maji ya eneo letu hili ni mizengwe mitupu", amedai Baba huyo.

Aidha aliwashangaa viongozi wa serikali iliyopo madarakani kudai rekodi zao za utendaji ziko wazi kinyume na madai ya wapinzani.

"Hizi ndizo rekodi zao za kushindwa kusambaza maji Jijini?, amehoji Mwananchi huyo.

Afya za wananchi hivi sasa ziko hatarini kutokana na ukosefu huo wa maji ambao huwalazimisha watu kutumia mabaki ya maji yaliyo kwenye madimbwi na miferejini.

Katika Shule moja ya sekondari iliyopo eneo hilo uongozi wa shule umelazimika kununua maji kutoka maeneo mengine kukabili tatizo hilo.

ANNUUR ilishuhudia baadhi ya wakazi wa nyumba zilizo jirani na shule hiyo wakilazimika kupanga ndoo zao katika moja ya magari yaliyokuwa yakisombelea maji kuleta shuleni hapo.

Mkuu wa Shule hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini amesema tatizo la maji eneo hilo ni la muda mrefu hali iliyoulazimisha uongozi wa shule kuchimba visima kadhaa ambayo navyo vinakauka kutokana na mahitaji kuwa makubwa.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org

An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook