AMA kweli mfanya maji haachi kutapatapa. Kadri anavyofurukuta, ndivyo anavyojaza maji tumboni na kujimaliza nguvu. Hii ndiyo hali halisi inayoikabili CCM. Sasa maji yako shingoni, kila inapolalama kutaka msaada wa wananchi, inazidi kubugia mafunda ya kujizamisha majini.
Mwaka 1995, CCM iliwatambulisha wananchi inachokusudia kuwafanyia kupitia Ilani yake kama wataiweka madarakani. Ikaahidi mengi ya maendeleo watakayonufaika kwayo wananchi pindi wakiipa kura ya ndiyo. Kumbe zilikuwa ahadi hewa kama ilivyokiri yenyewe baada ya 'kuchaguliwa.
Leo inakuja tena kwa wananchi katika sura ile ile ya maneno matupu. Katika Ilani yake inayoonesha mwelekeo wa sera katika miaka kumi ijayo inasema, kilimo cha kisasa ndiyo ufunguo wa maendeleo ya uchumi wa wote wa nchi yetu. Kauli hii ni ya kweli. Lakini je, CCM itawezazje kuifikisha nchi kwenye kilimo cha kisasa kwa miaka kumi? Ingekuwa ni wa kweli wangetenda hayo miaka 40 waliyoifuja.
Kiwango kikubwa cha ukulima wa Tanzania, ni ule wa kujikongoja kwa jembe la mkono. Kutokana na uduni huo, idadi kubwa ya wakulima ni wale masikini wa kutupwa.
Vyombo vya habari vimekuwa vikithibitisha hili kupitia taarifa zinazoeleza kufa kwa njaa kwa wananchi wengi. Kwa hiyo CCM haijaweza kuonesha kivitendo imani yake kuwa, kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.
Vyama vya ushirika wa wakulima vimekuwa mafuvu na mifupa mitupu. Vikiwa chini ya serikali ya CCM vimewanyongesha wakulima kwa kuwakopa katika kiwango cha kuwakatisha tamaa. Ni wakulima wachache wanaojiweza kumudu gharama za pembejeo; hili linatokana na ukweli kwamba mkulima asiyemudu hata kwa chakula, atawezaje kununua pembejeo?
Katika Ilani yake, CCM inakiri kuwa kwa kipindi chote ilichotawala haikuwafanyia wakulima lolote la maendeleo zaidi ya kuwanyonya na kuwakandamiza kwenye dimbwi la umaskini. Inaahidi kuweka kilimo cha kisasa kitakachoongeza tija na ziada. Kwamba ongezeko la tija na ziada ya mazao litakuwa na matokeo ya kupungua kwa umasikini uliokithiri vijijini!
Tafsiri ya maneno haya ni kwamba, kwa kipindi chote cha utawala wake, CCM imekuwa ikiweka na kusimamia sera zilizowaongezea wananchi umaskini. Hii ndiyo maana ya "umasikini uliokithiri vijijini". Kauli ya umaskini uliokithiri vijijini kimantiki inaonesha kuwa kabla ya CCM kutawala, wananchi vijijini walikuwa na nafuu.
Hivyo itakuwa hakuna kasoro ikisemwa kuwa, lile azimio la Arusha limewarusha wananchi kutoka kwenye umaskini nafuu kwenda kwenye umaskini hohehahe. Chama cha Mapinduzi kikaja kuwapindua. Badala ya wananchi kuwa watwana na viongozi kuwa watumishi wa wananchi, ikawa kinyume chake.
Walipogeuzwa kuwa watumwa, wananchi wakasukumwa katika vita vya Kagera. Kabla wananchi hawajapumua 'wakafungwa mikanda' kwa ahadi ya kuburuzwa katika dhiki kwa miezi kumi na nane. Katika kipindi hicho, CCM ikawavisha wananchi viatu vya matairi ya gari, nguo za magunia na viroba. Misululu ya foleni kusubiri unga, sukari na mafuta ya taa.
Si mijini wala vijijini, wananchi wengi walishona viraka nguo zao. Kule kijijini kwetu ilikuwa ukimlilia mtu shida yako hakuambii "sina kitu", atakuambia kuwa mwenzako viraka vinaulizana. Hivyo CCM inasema kweli kuwa umaskini umekithiri vijijini. Kwa maneno megine, inawafahamisha wananchi kuwa CCM ndiye adui yao.
Leo CCM eti ina mkakati wa mapinduzi ya kilimo. Inasema mipango ya ufundishaji wa ng'ombe wa kilimo ifufuliwe na ienezwe kwenye wilaya zenye mazingira muafaka. Inasema kuwa, suala la kueneza kilimo cha matrekta litafutiwe mkakati na kwamba vituo vya utafiti wa kilimo vifufuliwe.
Tazama wanavyojisuta! Utafiti wa kilimo ufufuliwe, kilimo cha matrekta kitafutiwe mkakati wa kuenezwa. Je, ni nani aliviua hivyo vituo vya utafiti wa kilimo kama si serikali ya CCM yenye sera butu za kilimo? Ni nani walizembea kuweka mkakati wa kueneza kilimo cha matrekta? Ina maana hii teknolojia ya matrekta imeibuka mwaka huu wa 2000?
Utawala wa serikali ya CCM ilitaifisha mali zote ilizodai kuwa ni za makupe. Iliyafanya hayo kwa nembo ya Azimio la Arusha na uhujumu uchumi. Mali hizo zikafanywa kuwa ni za "umma". Ukweli wa mambo unabaini kuwa neno "umma" limenufaisha kikundi cha wachache walioshika hatamu za uongozi.
Si husuda, majungu wala chuki, lakini hajapatikana kigogo aliyekufa masikini. Mheshimiwa Kingunge Ngombale -Mwiru ambaye kada mkongwe wa CCM aliwahi kuwatahadharisha makada wenzake kuhusu kasi ya kuongezeka kwa kundi la wananchi maskini. Kwa hiyo ni wazi kuwa kukithiri kwa umasikini matokeo ya CCM kuwepo madarakani!
Hivi sasa serikali ya CCM inaendelea kuuza nchi kwa anuani ya uwekezaji na kubinafisha. Kila kukicha mashirika ya "umma" yanauzwa. Zimekuwepo hoja kuwa "yanajiendesha kwa hasara". Ukweli ni kwamba serikali ya CCM imefanya ubadhilifu wa kuyafilisi.
Serikali hii ya Chama tawala imekuwa ikicheza danadana mali ya wananchi. Ruashwa imekithiri miongoni mwa vigogo. Imefikia kiwango ambacho hata kuunda Tume ya Rushwa ni sawa na kiini macho tu. Kuna kulindana kwa kiasi kikubwa mno! Katika mazingira haya, ubinafsishaji wa mashirika ya "umma" ni kama kuuza au kuuziana kwa maslahi ya vigogo. Wananchi, wao walie tu!
Sera za CCM ni za ubabaishajik kuzuga na ulaghai mtupu. Wakati wote huo wamekuwa wakiuza na kuuziana mashirika ya "umma" pasina ushirikishwaji wa wananchi. Kwa sasa Ilani yake inasema iko haja ya kuwashirikisha Watanzania katika ubinafsishaji wa mashirika ya umma yaliyobaki.
Inasikitisha kuona kuwa, Watanzania hawa ambao wazee wao walijinyima na kumng'oa Muingereza mwaka 1961, wanaingia kwenye karne ya sayansi na teknolojia wengi wao wakiwa kwenye giza la adui ujinga na ukata wa umaskini. Hali hii inawazuia kufanya shughuli za uchumi katika karne hii yenye mitandao ya kisasa.
CCM na serikali zake vinahusika kwa kutekeleza sera zilizowaviza na kuwadumaza Watanzania kiasi cha kuwafanya wawe "washamba" katika shughuli za uchumi wa kisasa. Ilani ya CCM inathibitisha kuwa Watanzania walio wengi hawana maarifa na uzoefu wa kuendesha shughuli za uchumi wa kisasa.
Inasema, mipango ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ni lazima iambatane na mipango ya elimu na mafunzo ya menejimenti ya aina mbalimbali za uchumi wa kisasa. Maneno haya yanaonyesha wazi namna CCM inavyojikanyaga.
Uchumi huu wa kisasa haukuibuka kwa ghafla. Ni mabadiliko ya taratibu ambayo lau kama serikali ya CCM ingelikuwa na mipango, sera na mikakati inayotekelezeka, ingeweza kuwatayarisha wananchi kielimu wakawa ni wenye kumudu kuziendesha shughuli za uchumi kwa mlengo wa kisasa.
Kushindwa kwa serikali ya CCM kuwaandaa Watanzania kuwa na elimu na ujuzi wa angalau kusimama dede katika karne hii ambayo uchumi wa kizamani umefutwa kwa mapinduzi ya kisayansi na teknolojia, kunathibitisha ubovu na uchovu wa Chama hicho, na ujima wa sera zake.
Kwa sifa zake hizo za ubovu, uchovu na ujima wa kisera, CCM haistahiki uongozi wala haitaweza kuwaletea maendeleo wananchi kama wanavyojieleza katika ndoto zake za mchana inazozifafanua ndani ya ilani yake ya uchaguzi. Ni muhali kwa chama chenye ulemavu wa menejimenti iliyopambika rushwa kuweza kuwaandaa vyema wananchi kwa mapinduzi ya uchumi wa kisasa.
CCM inajishitaki yenyewe kwa wananchi. Si hivyo tu bali inatoa vidhibiti vya uhakika vya kuifungia uongozi na kutolewa Ikulu.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |